Na Kadama Malunde, Shinyanga
WATOTO 10 waliobainika kuwa na matatizo ya vichwa vikubwa na mmoja mgongo wazi wamefanyiwa upasuaji na madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Mifupa Moi, kati ya 35 mkoani Shinyanga.
Upasuaji huo, umefanyika siku tatu zilizopita katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, ambapo jopo la madaktari bingwa wakishirikiana na watalaamu wengine kutoka Shirika la GSM Foundation.
Mbali ya upasuaji huo, watot 25 wamepewa matibabu ya kawaida.
Akizungumza baada ya kumaliza upasuaji huo, kiongozi wa jopo hilo kutoka Taasisi ya Moi, Dk. Josephat Kahamba, alisema kati ya watoto 35 wenye matatizo, 10 wamefanyiwa upasuaji na hali zao zinaendelea vizuri.
Alisema katika upasuaji huo, walikumbana na changamoto kubwa ya baadhi ya watoto matatizo yao yalikuwa yamekomaa.
“Naishauri jamii, iache kukumbatia matatizo haya, ikiona mtoto ana tatizo waende hospitali wapate tiba,”alisema.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela aliipongeza taasisi hiyo kwa kutoa tiba bure kwa wakazi wa mkoa huo.
Alisema wazazi wengi mkoani humo, wameshindwa kuwapatia matatibu watoto wao kutokana na kushindwa kumudu gharama za matibabu.
Alisema kutokana na tatizo hilo, atawasiliana na wizara husika kuona namna ya kupeleka madaktari zdi ili watoe tiba kwani mahitaji bado ni makubwa.
Mmoja wa wazazi wenye watoto waliopatiwa tiba hiyo, Anastazia Peter aliwashukuru madaktari hao kwa kutoa tiba na kuitaka Serikali iangalie namna ya kufanya hivyo mara kwa mara.