23.1 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

Watoa huduma ya maji ngazi ya jamii Maswa wapigwa msasa

Na Samwel Mwanga,Maswa

Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu  wameendesha mafunzo kwa watoa huduma ya maji ngazi ya jamii lengo likiwa kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao ya msingi katika utoaji na usimamizi wa huduma ya maji kwenye maeneo yao.

Baadhi ya Washiriki wa Mafunzo ya Watoa Huduma ya Maji ngazi ya Jamii wilaya ya Maswa wakiwa kwenye mafunzo kwenye ukumbi wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Maswa(Picha zote Na Samwel Mwanga).

Kama inavyofahamika kwamba Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs) ni vyombo vya kijamii vilivyoundwa na kusajiliwa kisheria kwa ajili ya kuendesha na kusimamia miradi wa maji ili iweze kutoa huduma ya maji endelevu kwa wananchi waishio maeneo ya vijijini.

Watoa huduma ya maji waliopatiwa mafunzo hayo ya siku tatu ni kutoka katika miradi ya maji ya Nguliguli-Mwamanenge, Isulilo-Ilamata, Mwabulimbu, Shishiyu na Jija.

Miradi mingine ni pamoja na Sayusayu, Njiapanda, Isagenghe na Sengwa-Mwasayi-Masela.

Akifungua mafunzo hayo leo Juni 7, 2022 Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge amewapongeza RUWASA kwa kuona umuhimu wa kuendesha mafunzo hayo kwa Watoa huduma ya Maji Ngazi ya jamii wilayani humo.

Amesema ili wananchi waweze kupata maji safi na salama katika maeneo ya vijijini ni vizuri watoa huduma hao wakafanya kazi kwa uadilifu,uwazi na kushirikiana na serikali za vijiji.

“Ni lazima mfanye kazi zenu kwa uadilifu,uwazi na kushirikiana na wenzenu wa serikali za vijiji kwenye maeneo yenu naengo ni kumpatia mwananchi huduma ya maji safi na salama.

“Kwa sasa serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya kugharamia miradi ya maji na hivi juzi tu Rais Samia Suluhu ameshuhudia mkataba wa utiaji wa saini ya fedha kwa ajili ya sekta ya maji hapa nchi kwa miji 28 hivyo basi tumuunge mkono kwa kuhakikisha mnatimiza majukumu yenu kwa uzalendo mkubwa,” amesema Kaminyonge.

Amesema azima ya Serikali ya Awamu ya sita ni kutekeleza ilani ya CCM katika sekta ya maji kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2025 huduma ya maji inafikia asilimia 85 hivyo ni vizuri Watoa huduma ya maji hao wakaenda kufanya kazi kwa ubunifu mkubwa na nidhamu ya hali ya juu kwa sababu wanatoa huduma muhimu kwa wananchi.

Naye Meneja wa RUWASA wilaya ya Maswa, Mhandisi Lucas Madaha alisema kuwa kumekuwa na mwingiliano mkubwa wa utendahi wa kazi kati ya Watoa huduma hao na Viongozi wa serikali za vijiji katika maeneo yao na kusababisha wananchi kukosa huduma ya maji safi na salama kwa kiwango cha juu.

Alisema kufuatia mafunzo hayo ana imani migogoro ambayo ilikuwepo hapo siku za nyuma itakwisha kwani kila mmoja atafanya kazi kwa kuzingatia mipaka yake ndiyo maana wamewashirikisha Madiwani Watendaji wa Kata na Watendaji wa vijiji kwenye mafunzo hayo ambao pia ni wajumbe katika maeneo yao yenye miradi ya maji.

“Tunachohitaji mfanye kazi kwa kila mmoja na mipaka yake msiingiliane ili huyu mwananchi tunayemlenga apate huduma bora ya maji safi na salama na ninyi mtapata mapato mazuri na matamanio yetu siku za usoni mjitegemee muwe Mamlaka za Maji,” amesema Mhandisi Madaha.

Awali, Afisa Maendeleo ya jamii wa RUWASA wilayani humo, Willison Magaigwa alisema kuwa wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo wanayotoa huduma ya maji kuacha kutumia maji ya kwenye visima na madimbwi ambayo si safi na salama na badala yake watumie maji ya bomba yanayotolewa na Ruwasa kwa bei nafuu ya Shilingi 50 kwa ndoo moja kwenye maeneo yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,717FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles