24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Watendaji wanaojigawia viwanja vya raia kitanzini

         Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema ameibua ufisadi wa viwanja 1,125 vilivyotakiwa kupewa wakazi wa Kipawa waliohamishwa kupisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kiamataifa wa  Julius Nyerere (JNIA).

Akizungumza katika majumuisho ya ziara yake aliyoifanya katika kata 35 za nanispaa hiyo jana, Mjema alisema Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) ilipima viwanja 5,096 kwa ajili ya kuwahamisha wananchi waliotakiwa kupisha lango la tatu la uwanja huo (terminal III).

Alisema kati ya viwanja vilivyopimwa kwa ajili ya wanananchi hao ni viwanja 3971 pekee vilivyogawiwa.

Alisema mpaka sasa wakazi 514 waliohamishwa katika eneo hilo hawajapata viwanja huku TAA ikitafuta viwanja vingine kwa ajili ya kuwapatia.

“Suala hili tumelikabidhi kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa ajili ya kuvitafuta viwanja 1125,” alisema Mjema.

Alisema mgogoro huo una sura tatu, moja ikiwa ni wamiliki wa mashamba yaliyotwaliwa kutokulipwa fidia na kutopewa viwanja kama ilivyokuwa katika makubaliano na wengine kupewa viwanja katika maeneo ambayo hayajapimwa.

“Katika mgogoro huu Mkurugenzi wa TAA aliunda kamati ya uchunguzi na matokeo ameonyesha kuwapo  ukiukwaji mkubwa wa taratibu na ndiyo kuwa chanzo cha migogoro,” alisema Mjema.

Aliitaka Takukuru kufanya uchunguzi wa haraka ili haki iweze kutendeka na wahusika kuchukuliwa hatua stahiki.

Alimwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kuvilinda viwanja vingine 212 nilivyopimwa kwa ajili ya huduma za jamii vilivyopo Kigilagila na Kipunguni.

Katika hatua nyingine Mjema alisema baadhi ya michakato wa urasimishaji ardhi inafanywa na kampuni ambazo hazijasajiliwa jambo linalosababisha wananchi kutapeliwa fedha zao.

Aliwataka watendaji wa manispaa hiyo kutumia akaunti isiyohusisha kandarasi.

Alisema wakandarasi wamekuwa wakidai gharama kubwa tofauti na thamani halisi ya ujenzi wanaoufanya.

“Kuanzia sasa marufuku kuwatumia watu hawa kwa kuwa wamekuwa wakijenga kwa gharama kubwa huku kilichojengwa hakilingani na thamani ya fedha,” alisema Mjema.

Mkurugenzi wa Manispaa hiyo,  Msongela Palela, alisema asilimia 70 ya barua zinafika ofisini kwake ni za migogoro na matatizo ya ardhi.

“Tutakapogundua mfanyakazi wa halmashauri hii atakayegawa kiwanja kimoja mara mbili atafukuzwa kazi mara moja,” alisema Palela.

Alisema kuanzia wiki ijayo, watapita katika kila mtaa kuangalia miradi ya muda mrefu ambayo haijakamilika (viporo) na kuikamilisha.

Hata hivyo Palela alishangazwa na vikundi vya wanawake, vijana na walemavu kushindwa  kuchukua mikopo ambayo ni asilimia 10 ya mapato ya manispaa hiyo.

“Mpaka sasa kuna Sh bilioni tatu ambazo zinasubiri wanawake, vijana na walemavu kukopa na kwa vijana tunatarajia kuwakopesha bajaj na pikipiki,” alisema Palela.

Alisema tayari Serikali imeingiza katika akaunti ya manispaa hiyo Sh milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Kivule huku manispaa hiyo ikiongeza Sh milioni 250.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles