31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Watendaji waliotafuna Milioni 700 Chemba kufikishwa mahakamni

Na Ramadhan Hassan, Chemba

WATENDAJI Kata katika Halmashuri ya Chemba waliotafuna zaidi ya Sh milioni 700 kutokana na makusanyo katika minada wanatarajiwa kupelekwa mahakamani mara baada ya uhakiki wa madeni yao kukamilika.

Hatua hiyo imekuja kufuatia baadhi ya watendaji wa kata za Halmshauri ya Chemb  kutafuna zaidi ya Sh milioni 700 ambazo zinatokana na makusanyo ya minadani ambapo mara baada ya Halmashauri kuwabana wameweza kurejesha zaidi ya Sh milioni 100.

Kutokana na hali hiyo Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo limeitaka Halmashauri ya Wilaya hiyo kuwachukualia hatua kali ikiwemo kuwafikisha Mahakamani, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),Polisi pamoja na hatua za kinidhamu ziweze kuchukuliwa kwa watendaji hao ambao wametafuna fedha hizo.

Akiwasilisha taarifa ya kamati ya fedha, uchumi na mipango katika kikao cha Baraza la Madiwani mwishoni mwa wiki Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chemba, Said  Sambala amesema kila mwaka Halmashauri hiyo imekuwa ikifanya vibaya katika ukusanyaji wa mapato ambapo amedai baadhi ya sababu ni pamoja na watendaji ambao wamekuwa sio waaminifu katika ukusanyaji wa mapato.

Sambala ambaye pia ni Diwani wa Mondo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) amesema mwaka jana walipata hati yenye mashaka kutokana na baadhi ya watendaji wa kata kutafuna zaidi ya Sh milioni 700 ambazo zipo mikononi mwao watendaji hao.

Amesema mara baada ya kuwabana watendaji hao ambao fedha hizo walizikusanya katika minada mbalimbali na kushindwa kupeleka banki baadhi yao wameweza kurejesha Sh milioni 108 katika akaunti ya Halmashauri ya Wilaya ya Chemba.

“Baadhi walikiri kwamba walikuwa wakikusanya fedha na hawazipeleki banki na wengine walikuwa hawakusanyi kwa kutumia mashine ya kukusanya mapato za   Poss,sasa tumewabana na hatutaki mchezo tunataka hii fedha yote irudi,” amesema.

Amesema kinachoendelea ni kujua kila mmoja anadaiwa shilingi ngapi   na  anatakiwa kulipa kiasi gani na Mkurugenzi wa Halmshauri hiyo atakutana nao ambapo baada ya hapo zitafuata hatua za kupelekana Mahakamani,Polisi pamoja na Takukuru pamoja na baadhi kuachishwa kazi.

Mwenyekiti huyo amesema kuanzia Septemba mwaka huu kamati ya fedha itaanza kufanya uhakiki  wa vyanzo vyote vya mapato katika Halmashauri hiyo halafu wataanza kulinganisha na mapato ya sasa ili wajue walikuwa wakiibiwa wapi.

Vilevile amesema hivi karibuni wataanza ukusanyaji wa   mapato kwa kutumia mawakala kwani baadhi ya watendaji wamekuwa sio waaminifu.

Naye,Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma ambaye alihudhuria kikao hicho, Dk.Fatma Mganga amesema katika Halmashauri hiyo kuna mambo hayaendi vizuri ndio maana ameenda katika kikao hicho.

Amesema watendaji wa Halmashauri hiyo wanatakiwa kulibadilisha jina la Chemba kwani midomoni mwa watu halitamkwi vizuri kutokana na mambo kutokukaa vizuri hivyo wanatakiwa kumpa ushirikiano Mkurugenzi mpya wa Halmashauri hiyo kwani peke yake hataweza.

“Mkurugenzi (Siwema Hamoud Jumaa) kuwa mkali katika matumizi unatakiwa ujue bei ya kila kitu maana utakusanya halafu watu watakuja wanataka fedha ulizokusanya hivyo jua bei ya kila kitu,”amesema.

Amewataka Madiwani hao kusimamia suala la upatikanaji wa mapato kwani Halmashauri hiyo ni tajiri lakini mapato yake ni kidogo.

Kwa upande wake,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo,Siwema Hamoud Jumaa amesema suala la mapato ni jambo ambalo linawaumiza sana ambapo amedai wapo katika mchakato wa kuhakikisha wizi na udanganyifu katika mapato unamalizika kwa kuchora mstari upya.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,Abdi Msuri   ambaye ni Diwani wa Jangalo amesema hali kimapato katika Halmashauri hiyo ni mbaya hivyo wataanza utaratibu wa kukusanya mapato kupitia Mawakala.

“Zamani tulikuwa tukitumia Mawakala mfano katika mnada wa Soya tulikuwa tukikusanya shilingi milioni 7 mpaka nane baada ya kuwaondoa wale sasa tunakusanya shilingi milioni 3 mpaka 4 sasa hali ni mbaya turudi tu kwa Mawakala kwani tutakuwa tukiwasimamia,”amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles