WATAWALA WANAIOGOPA KATIBA MPYA – SUMAYE

0
554

NA VERONICA ROMWALD

WAZIRI Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, amesema Katiba mpya imewekwa pembeni, kwani watawala hawataki madaraka yao yadhibitiwe na Katiba.

Sumaye, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Pwani, alisema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, kwenye mahafali ya vijana wa chuo kikuu wa chama hicho (Chaso).

Alisema Katiba inayopendekezwa ni ya wananchi na ilipitishwa na Bunge, lakini inaonekana si jambo la kipaumbele na wala haitashughulikiwa tena kwa sababu itawadhibiti watawala.

“Mchakato wa Katiba mpya umeigharimu nchi fedha nyingi za walipa kodi na kuitupa ni “makanikia” nyingine, najua Rais John Magufuli  amekwishasema yeye haambiwi la kufanya, lakini sisi tutaendelea kumkumbusha yale ambayo tunadhani ni muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu.

“Si jambo la kupuuzwa. Kama ni la kupuuzwa basi awakamate wote waliohusika na uamuzi huo, maana ni ubadhirifu unaofanana na ule wa makanikia,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema chama hicho pamoja na washirika wake wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wataendelea kudai Katiba mpya hadi itakapopatikana.

Alisema licha ya watawala kueleza kwamba Tanzania ina mfumo wa vyama vingi, hata hivyo si kweli, bali ina mfumo ‘bandia’ wa siasa za vyama vingi.

“Tuna mfumo ‘bandia’ wa siasa ya vyama vingi, mfumo wa chama kimoja kilichovaa ngozi ya vyama vingi, mfumo wa vyama vingi vya siasa ni lazima ufuate utawala wa sheria na unaolinda, unaoheshimu na kuitetea Katiba ya nchi ambayo watawala wameapa nayo wakati wa kukabidhiwa madaraka.

“Ukiona katika nchi watawala hawatii sheria wala katiba ya nchi, basi hakuna utawala wa kweli wa vyama vingi vya siasa, bali kuna utawala wa imla uliovaa ngozi ya demokrasia ya vyama vingi vya siasa.

“Tanzania leo hakuna uhuru wa watu kutoa na kupokea habari kama Katiba yetu inavyotaka. Ibara ya 18 ambayo inazungumzia “Haki na Uhuru wa Mawazo,” alisema.

Alisema mfumo au demokrasia ya vyama vingi haurusu ubabe katika utawala na uongozi wa nchi.

“Kama kiongozi anatawala kwa ubabe na vitisho, lazima tukubali kuwa ama Katiba tuliyonayo siyo sahihi au mfumo uliopo siyo wa demokrasia ya vyama vingi kivitendo,” alisisitiza.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here