WATU watatu wamefariki dunia baada ya kukosa hewa ndani ya shimo lenye urefu wa zaidi ya mita 30 walipokuwa wakichota maji ya kusafishia dhahabu katika Kijiji cha Itumba wilayani Chunya, mkoani Mbeya.
Akithibitisha kutokea tukio hilo jana, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Rehema Madusa, alisema watu hao walikuwa wakichota maji ndani ya shimo ambalo awali lilikuwa likifanyika shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu.
Aliwataja waliofariki ni Zawadi Soda (28), Wilson Soda (24) na Jamal Omary (20) wote wakazi wa Kata ya Chalangwa.
Alisema wachimbaji hao walikumbwa na mauti Septemba 17, mwaka huu.
Alisema baada ya uchunguzi wa vipimo kutoka kwa daktari, Moris Mdoe, aliyefanyakazi ya kupima ilibainika watu hao walipoteza uhai kutokana na kukosa hewa.
Alisema mashimo hayo awali yalikuwa yanamilikiwa na Keneth Mwakyusa ambaye baada ya kuona dhahabu zimepungua aliamua kuacha kuchimba.
Alisema chanzo cha vifo hivyo kwa mujibu wa mganga ni kukosa hewa baada ya vijana hao kutumia mashine ya kuvuta maji ambayo waliingiza kwenye shimo na kuiwasha wakiwa ndani ya hilo shimo, baada ya kompresa kutofika sehemu yenye maji.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Bosco Mwanginde, alipotembelea eneo la tukio alisema wachimbaji wadogo wadogo wengi katika wilaya hiyo wamekuwa wakitumia njia zisizo rasmi za kuchimbia madini hayo.
Alisema kitendo cha vijana hao kuchukua uamuzi wa kuweka injini ya jenereta shimoni na kuvuta maji ambayo yalikuwa umbali mrefu na wao wakiwamo ndani, ni hatari kwani hewa inakosekana.
Alisema vijana wanatakiwa kuachana na tabia ya kutumia vifaa duni kwa ajili ya uchimbaji wa madini, hususani injini za jenereta ambazo zimekuwa zikizalisha moshi mwingi.
“Shimo hili ukiliangalia lina zaidi ya urefu wa mita 30, kwa kawaida maji yalikuwa chini, hawa wachimbaji waliamua kuchukua mashine yao na kuifunga ndani huku na wao wakiwa ndani ya shimo hilo,” alisema Mwanginde.