26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Watanzania zaidi watakiwa kuanzisha viwanda vya kuzalisha mbolea

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

KATIBU Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya, amesema wakati Serikali ya awamu ya tano ikiendelea kuhakikisha wakulima wanaongeza uzalishaji wa mazao ya biashara na chakula wawekezaji wanahamasishwa kuanzisha viwanda vya mbolea ili nchi ijitosheleze.

Kusaya aliwataka Watanzania kuanzisha viwanda vya mbolea ambayo inahitajika kwa wingi zaidi wakati huu kilimo kikiwa ni biashara na kinaajiRi asilimia 58 wananchi na kuchangia malighafi za viwandani kwa asilimia 65.

Kusaya alitoa kauli hiyo wakati alipotembelea kiwanda cha mbolea za asili na zilizoongezewa virutubishi (Organic Fertilizer) cha Guavay kilichopo Gongolamboto jijini Dar es Salaam ikiwa ni ziara yake ya kuhamashisha viwanda vya ndani vinaongeza uzalishaji wa mbolea.

Alisema mahitaji ya mbolea za viwandani yameongezeka nchini kutokana na hamasa kubwa na wakulima kujitokeza kulima zaidi ikiwa ni mafanikio yaliyopatikana na Wizara ya Kilimo kwa ushirikiano na sekta binafsi.

Alisema  mahitaji ya mbolea kwa mwaka ni tani 664,000 wakati uzalishaji kwenye viwanda umefika tani 30,000 ya mbolea hivyo kuwa na uhitaji mkubwa.

“ Nawahamasisha Watanzania zaidi kujitokeza kuwekeza kwenye viwanda vya kuzalisha mbolea ili wakulima wapate mbolea kwa gharama nafuu na karibu na wakulima,” alisema Kusaya.

Alisema hivi karibuni alifanya ziara mkoani Kagera na kupokea malalamiko ya wakulima kuuziwa mbolea aina ya UREA mfuko wa kilo 50 kwa bei kati ya Sh 80,000 na 90,000 hali inayowakwamisha kuongeza tija na uzalishaji.

Wakati huo huo, Kusaya amewashauri wakulima kote nchini kuwa na utaratibu wa kupata ushauri toka kwa maofisa ugani wa aina ya mbolea kwa mazao wanayolima kabla ya kwenda kununua ili wapate mbolea bora na yenye kuongeza tija ya uzalishaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dk. Stephano Ngailo, alisema uwepo wa malalamiko ya bei kubwa ya mbolea nchini unatokana na mbolea nyingi kuagizwa toka nje ya nchi.

Alisema kuna viwanda 12 pekee nchini vinavyozalisha mbolea na kuwa uzalishaji ni chini ya tani 30,000 ambazo ni sawa na asilimia 6 ya mahitaji yote ya mbolea kwa mwaka.

“ Kazi ya TFRA ni kuhakikisha upatikanaji wa mbolea bora na yenye gharama nafuu kwa wakulima, ndiyo maana tunahamasisha wawekezaji kujitokeza kujenga viwanda vya mbolea kama ilivyo kwa kampuni ya Guavay” alisisitiza Dk. Ngailo.

Meneja ubora wa kiwanda hicho cha Guavay, Latifa Mafumbi, alimweleza Kusaya kuwa kiwanda hicho kinazalisha mbolea aina ya Hakika zinazorutubisha udongo.

Latifa alisema uwezo wa kiwanda cha Guavay kwa sasa ni kuzalisha tani 2,000 za mbolea kwa mwaka na kuwa soko lao lipo kwenye mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Arusha na Kilimanjaro.

“ Mbolea yetu ya Hakika inafanya vizuri zaidi kwenye mazao ya parachichi, mpunga na vitunguu kutokana na utafiti tuliofanya” alisema Latifa.

Alitaja changamoto ya mtaji kukuza uzalishaji wa mbolea ya asili umepelekea kampuni hiyo ya Guavay iliyoanzishwa mwaka 2014 na vijana wa kitanzania kushindwa kufikia mahitaji ya soko la mbolea ya Organic ya tani 20,000 kwa mwaka nchini.

Kusaya ameanza ziara ya kukagua na kutembelea viwanda vya mbolea vilivyopo Dar es Salaam, Tanga, Arusha na Manyara kukagua uzalishaji mbolea nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles