Safina Sarwatt, Kilimanjaro
Watanzania wametakiwa kumpongeza na kumuenzi Rais wa zamani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dk. John Magufuli kwa uzalendo na upendo wake wa kuanzisha kiwanda cha Kimataifa cha ngozi Kilimanjaro kilichopo Mjini Moshi.
Afisa Habari na Masoko wa kiwanda cha ngozi Kilimanjaro, Fredrick Njoka, ameyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari waliotembelea kiwanda hicho na kutoa wito kwa wananchi kupenda kununua na kutumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
Amesema utekelezaji wa ujenzi wa kiwanda hicho ni ndoto za zilizoanzishwa na hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere tangu mwaka 1977 alipoanzisha kiwanda cha kutengeneza viatu vya jeshi.
Njoka amesema katika kukuza uchumi wa Tanzania ya Viwanda, Hayati Dk. Magufuli alitilia mkazo kuhakikisha uzalishaji unaongezeka na kiwanda hicho kimekuwa kikipanuka zaidi ili liweze kukithi mahitaji ya soko Kitaifa na Kimataifa.
Amesema Tanzania ni Nchi ya pili barani Afrika ikitanguliwa na Ethiopia kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo na kwamba lengo la kuanzishwa kwa kiwanda hicho hapa nchini ni kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa kwa ngozi.
Njoka amesema kiwanda hicho tayari kimefungua milango kwa wafugaji kuuza ngozi kiwanda cha Kilimanjaro ili liweze kuongeza thamani ya mnyororo kwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini kwa kutumia ngozi.
Amesema uwekezaji uliofanyika katika kiwanda hicho ni mkubwa na umegawanyika katika sehemu nne ikiwemo kiwanda cha kuchakata ngozi ambapo pia kitahusika na kuzalisha malighafi za kulisha viwanda vingine.
Sehemu nyingine ni kiwanda cha kutengeneza soli na sehemu ya kuhifadhi mali ghafi ndani ya kiwanda na kwamba asilimia 60 ya bidhaa zinazozalishwa zitauzwa hapa nchini na asilimia 40 itauzwa kimataifa.
“Kukamilika kwa kiwanda hicho ni faraja kubwa kwa wafugaji na Watanzani kwa ujumla kwani kiwanda hicho kitanunua ngozi za wafugaji hapa nchini kutoa ajira zaidi ya watu 3,000 na kuchangia pato la taifa.
“Nitoe wito kwa wananchi kupenda kununua na kutumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini kwa lengo la kuchochea ukuzaji wa pato la Taifa,” amesema Njoka.