Watanzania waonywa wasinunue bidhaa feki

0
781
Ofisa Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), Clara Makenya
Ofisa Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), Clara Makenya
Ofisa Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), Clara Makenya

Na ELIYA MBONEA, ARUSHA

WATANZANIA wametakiwa kuanza kujifunza kukataa kununua au kuendelea kutumia bidhaa zisizokuwa na viwango ili kuepukana na umasikini.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Rashid Taka, alipokuwa akifungua mkutano wa majadiliano kuhusu mradi wa uboreshaji wa utekelezaji wa matakwa ya viwango.

Alisema watumiaji wa bidhaa mbalimbali nchini wanatakiwa kuanza kukataa kutumia bidhaa duni na zisizo na ubora ili kujiepusha na umasikini unaosababishwa na bidhaa hizo kuharibika au kufa.

“Bidhaa zisizokuwa na ubora zimeendelea kuwaletea wananchi umasikini, niwaombe Watanzania muanze kukataa kuzitumia ikiwa ni pamoja na kuzinunua,” alisema Taka kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Alisema ipo haja ya kuwekeza nguvu kubwa kwa mlaji wa mwisho.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Egid Mabofu, aliwataka wananchi kujitambua kuwa wao ni sehemu yao.

“Watumiaji wa mwisho wa bidhaa ni sehemu ya TBS, wanapaswa kujifunza kukataa kutumia bidhaa zisizo na viwango wakifanya hivyo watasababisha wazalishaji kushindwa kuzalisha tena,” alisema Mabofu.

Aliwataka wananchi kujenga utamaduni wa kutoa taarifa za mahali ambako kuna bidhaa zisizo na ubora zinazozalishwa ili kuongeza wigo wa kukabiliana na changamoto hiyo.

Naye Ofisa Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), Clara Makenya, alisema upo uhusiano mkubwa kati ya hali ya mazingira na mnyororo mzima wa uzalishaji, utengenezaji na utumiaji wa bidhaa.

“Tuko hapa kwa kuzingatia ajenda ya mwaka 2030, lengo la 12 linaongelea kuhusu matumizi na uzalishaji wa bidhaa na linaangalia katika matumizi na uzalishaji wa bidhaa uangalie uendelevu wa mazingira,” alisema Clara na kuongeza:

“UNEP ndio maana inashirikiana na TBS ili kuona viwango au jamii na wadau wanaohusika wanafahamu nafasi zao katika kuhakikisha uendelevu wa mazingira.

“Tuna amini kwamba uelewa mkubwa ndio utakaowezesha watumiaji kuanza kukataa bidhaa zisizokuwa na viwango katika masoko.”

Alisema bidhaa zisizokuwa na ubora kwa kiwango kikubwa zimekuwa mchangiaji mkubwa wa uharibifu wa mazingira katika maeneo mengi nchini ukilinganisha na bidhaa zenye ubora.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here