27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Watanzania milioni sita tu ndio waliopata vitambulisho vya taifa

 RAMADHAN HASSAN -DODOMA 

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amesema hadi sasa Watanzania waliopata vitambulisho vya taifa ni milioni sita kati ya 21 waliojiandikisha. 

Akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema Serikali imenunua mtambo mpya wa kisasa ambao utakuwa na uwezo wa kuzalisha vitambulisho 9,000 kwa saa, hivyo ndani ya miaka miwili wote waliojiandikisha watapata vitambulisho. 

Alisema hadi sasa tayari Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) imefanikiwa kutambua wananchi milioni 21. 8, kati ya milioni 27. 7 waliotarajiwa kusajiliwa. 

Simbachawene alisema namba za kipekee za milioni 17. 8 zimezalishwa na zinaweza kutumika katika utambuzi wa watu. 

Alisema kwenye utoaji vitambulisho bado Nida haijafanya vizuri. 

“Ni kweli kwamba tumechelewa (kutoa vitambulisho), wakati mwingine ni vyema kukiri. Watanzania walijitokeza, lakini kasi (ya kutoa vitambulisho) imekuwa ni ndogo. 

“Mitambo ya zamani imetuchelewesha, matarajio yetu kama tutaweza kuzalisha vitambulisho 9,000 kwa saa, lengo la kuwapa Watanzania milioni 27 vitambulisho tutahitaji miaka miwili wote wapate,” alisema Simbachawene. 

Alipoulizwa gharama za mtambo huo, Simbachawene alisema umenunuliwa kwa Sh bilioni 8.5. 

Alisema Nida imeendelea na ukamilishaji wa ufungaji mtambo huo na uzalishaji vitambulisho utaanza mwishoni mwa Aprili. 

“Na ule wa zamani tunataka uendelee kufanya kazi na vitambulisho vilikuwa vina kiwango cha chini kwa sababu ya mtambo kuwa wa zamani. 

“Mtambo wa zamani ulikuwa unazalisha vitambulisho 500 kwa saa,” alisema Simbachawene. 

Katika hatua nyingine, Simbachawene aliwaomba radhi Watanzania ambao wamekuwa hawakaribishwi vizuri katika vituo vya kujiandikishia kwa kutolewa kauli ambazo si nzuri na uchelewaji wa vitambulisho hivyo. 

“Nataka watambue (watumishi wa Nida) hawapaswi kufanya kazi kama wanajitegemea, agizo langu la kwanza wafahamu kwanza zipo Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo wanapaswa kushirikiana nazo na kushirikisha mfumo wa uongozi na Serikai za Mitaa. 

“Mkurugenzi anahusika kusimamia zoezi hili, kwahiyo Mamlaka ya Serikali za Mitaa hazipaswi kukaa 

 mbali, wakuu wa wilaya na mikoa ninawasihi kusimamia watumishi wa Nida waliopo katika maeneo yao. 

“Nitawaomba makatibu tawala kusimamia watumishi wa Serikali, hawa maofisa wa Nida hawapaswi kuwa na uhuru ambao wanao kuwajibu vibaya watu, wajue kwamba kuna watu wapo juu yao na wanapaswa kupata taarifa za kila siku. 

“Malalamiko ni makubwa, unawakuta kwenye vituo wanasema wewe ni Mtanzania ama sio Mtanzania, na wangeshirikisha Serikali za Mitaa ingekuwa ni jambo la uhakika zaidi,” alisema Simbachawene. 

Alisema watendaji wa Nida nao wamekuwa ni changamoto kubwa na ameahidi kwamba ataanza kuwashughulikia kwa kuziachia kazi mamlaka za ajira. 

“Ndani ya Nida kumekuwa na changamoto, ucheleweshaji huu umeleta msongamao mkubwa wakati mwingine hata usajili wa namba za simu umesababishwa na kukosa namba. 

“Nikiri tu kwamba ipo changamoto ndani ya Nida na inahitaji kushughulikiwa na tutafanya mabadiliko makubwa kuanzia leo, kesho na keshokutwa mtasikia mamlaka za ajira zitasema kitu. 

“Nichukue nafasi hii kukiri mbele ya Watanzania zoezi letu limesuasua, lakini mpaka mwisho wa mwezi wa nne tutakuwa tumekamilisha kufunga mtambo,” alisema Simbachawene. 

 MAENEO YA MIPAKANI 

Vilevile aliwataka watendaji wa Nida kushirikiana na Serikali za Mitaa na Vijiji kutambua raia wa Tanzania katika maeneo ya mipakani kwani wamekuwa wakizua taharuki. 

“Maeneo ya mipakani kuna changamoto ya utatuzi nani raia ama sio raia. Mamlaka za Serikali za Mitaa ndio zinatakiwa kutoa majibu. 

“Mnawapa watu hofu kwani unapojua kwamba wewe ni Mtanzania halafu mtu anakwambia sio Mtanzania lazima utakuwa na hofu,” alisema Simbachawene. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles