30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

WATANZANIA KUTAKIWA KUFUATA TARATIBU UMILIKI HALALI VYOMBO VYA MOTO

Na KOKU DAVID


KILA mtu hujisikia vizuri anaponunua kitu kama gari au hata nyumba, nyaraka za umiliki zikasomeka kwa jina lake. Hii inamsaidia kuonyesha kuwa ni mmiliki halali.

Zipo taratibu za kisheria ambazo humwezesha mtu anayenunua chombo cha moto kama vile gari au pikipiki, kubadilisha umiliki kutoka kwa aliyemuuzia na kuja kwake. Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo, anafafanua taratibu zinazotakiwa kufuatwa ili kubadilisha umiliki.

Anasema TRA ina jukumu la kusimamia usajili wa vyombo vya usafiri Tanzania Bara ambao unasimamiwa kwa kutumia sheria na. 30 ya usalama barabarani ya mwaka 1973, Sheria ya Vyombo vya usafiri (Kodi ya usajili na ubadilishaji wa umiliki) ya mwaka 1972, kanuni za usalama barabarani (magari ya kutoka nje ya nchi) ya mwaka 1973 na taratibu za usalama barabarani (usajili wa vyombo vya usafiri).

Kwa mujibu wa sheria, kila mtu anayemiliki chombo cha usafiri anatakiwa kupeleka maombi kwa kujaza fomu MV 10 kwa ajili ya usajili wa chombo husika kama gari, pikipiki za magurudumu matatu na mawili maarufu kama bodaboda.

Kayombo anasema kuna taasisi ambazo haziombi usajili ambazo ni vyombo vya usafiri vinavyomilikiwa na Serikali, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWT), Mashirika ya kimataifa pamoja na ofisi za kidiplomasia au balozi ndogo.

Anasema kila chombo cha moto kinatakiwa kulipiwa ada ya leseni kwa mwaka na kwamba hutozwa wakati wa usajili wa kwanza wa chombo na kila mwaka baada ya hapo.

Pia ada hiyo ya mwaka hutegemea ukubwa wa injini, lakini matrekta, pikipiki na pikipiki za magurudumu matatu zimeondolewa malipo ya ada hii isipokuwa yanatakiwa kulipiwa kiasi cha Sh 10,000 kama ada ya ukaguzi wa vifaa vya kuzimia moto.

Malipo hayo yanatakiwa kufanyika kupitia simu za viganjani, mawakala wa maxmalipo au kupitia benki zilizoidhinishwa.

Kwa upande wa wamiliki watakaotaka kuchukua stika ya leseni ya mwaka ya chombo chake cha moto, atatakiwa kutumia namba ya kumbukumbu aliyopewa kupitia ujumbe wa simu, ikiwa ni pamoja na kitambulisho ili aweze kuipata stika hiyo ambayo ataipata kupitia ofisi yoyote ya TRA na kwamba hairuhusiwi mtu yeyote kumchukulia mwingine.

Katika mabadiliko ya umiliki wa chombo cha moto, mmiliki mpya ndiye atakayetakiwa kulipia kodi ya mabadiliko ambayo malipo yake hufanyika pindi chombo cha moto kinataka kubalishwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.

Baada ya hapo, muuzaji atatakiwa kulipa ushuru wa stempu ambayo ni asilimia moja ya bei ya mauziano na kwamba malipo hayo yote hulipiwa benki.

Vitu vinavyohitajika wakati wa mabadiliko ya umiliki wa chombo cha usafiri, ni kadi halisi ya chombo husika, namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) pamoja na mkataba wa mauziano uliosainiwa na mwanasheria na kwa upande wa ada za kubadili umiliki wa gari ni Sh 50,000, pikipiki 27,000 na kadi mpya ya usajili kutokana na kubadili mmiliki ni Sh 10,000.

Kwa kadi ya usajili wa chombo cha usafiri iliyopotea, mmiliki atatakiwa kutoa taarifa kituo cha polisi ambapo polisi atakagua chombo hicho na kutoa ripoti ya upotevu na baadaye ripoti hiyo itawasilishwa TRA ambako atatakiwa kulipa malipo ya Sh 10,000, ili aweze kupewa nakala mbili za kadi ya usajili.

Kwa gari lililopata ajali na kutoweza kutumika tena, kwa mujibu wa kanuni Namba 177 ya mwaka 2001 ya Sheria ya Usalama Barabarani ya Mwaka 1973, mwenye chombo hicho cha moto atatakiwa kuomba ili kifutwe kwenye usajili wa magari.

Hata hivyo, TRA imekuwa ikikutana na changamoto kutoka kwa baadhi ya wamiliki kutobadilisha umiliki mara wauzapo au kununua vyombo vya moto, wamiliki kutotoa taarifa za vyombo vyao ambavyo havipo tena barabarani, ikiwa ni pamoja na wananchi kutotafuta taarifa TRA ya chombo husika kabla ya uamuzi wa kununua chombo hicho cha moto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles