25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Watanzania kunufaika na ajira Qatar- Pinda

Mizengo-Pinda

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Na Mwandishi Maalumu, Qatar
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema Watanzania watanufaika na kipato na maarifa ya teknolojia ya kisasa kutokana na ajira ambazo watapata katika nchi ya Qatar baada ya mkataba kusainiwa hivi karibuni.
Hayo aliyasema jana jijini Doha, Qatar wakati akizumgumza na waandishi wa habari ili kuwapa taarifa fupi juu ya mambo yaliyojiri katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Abdulla Nasser Al Thani.
Katika mazungumzo hayo ambayo yalifanyika ofisini kwa Sheikh Abdulla, Waziri Mkuu Pinda alisema wamekubaliana kutoa ajira kwa Watanzania kwa sababu nchi hii inahitaji wafanyakazi wengi kwenye sekta mbalimbali na raia wake ni wachache.
“Hivi sasa wapo Watanzania wanaofanya kazi hapa lakini ni wachache mno. Mazungumzo yalishaanza siku za nyuma. Tukisaini mkataba katika muda mfupi ujao, tutajua ni idadi gani wanahitajika na wanaweza kuja kila baada ya muda gani.
“Hapa Qatar kuna uwekezaji mkubwa umefanyika, kwa hiyo wanahitaji watu wa kufanya kazi… kwenye mahoteli, viwandani, na kikubwa hapa ninachokiona watu wetu watapata kipato lakini pia watapata ujuzi kwa maana ya maarifa yanayoendana teknolojia ya kisasa,” alisema Pinda.
Akieleza mambo mengine ambayo wamekubalina kushirkiana kama nchi rafiki, Waziri Mkuu alisema kuna mambo makuu manne likiwemo hilo la ajira.
“La kwanza ni Kilimo. Hapa Qatar ni jangwa kila mahali. Wamekubali kuja kuwekeza kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi kwa sababu sisi tuko karibu nao zaidi kuliko Marekani au Brazil.
“Wanaweza kupata mchele, matunda, nyama kwa maana ya machinjio na viwanda vya kusindika nyama lakini pia katika uvuvi wa samaki. Tunayo bahari ila mitaji yetu ni midogo. Kwa hiyo wamekubali kuangalia eneo hilo pia,” alisema.
Alisema eneo la pili ni la gesi na mafuta “Wamekubali kutusaidia utaalmu ili tushirikiane nao katika namna kutumia gesi kwenye ngazi ya chini hasa viwanda kwa sababu wenzetu wana uzoefu wa muda mrefu. Hata kwenye mafuta wameonyesha kuwa wako tayari,” alisema.
Katika ziara hiyo Pinda, aliongozana na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kimani, Waziri wa Kilimo na Maliasili wa Zanzibar, Dk. Sira Ubwa Mamboya, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Maalim, Naibu Waziri wa Nishati, Charles Kitwanga, Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi.
Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, wabunge wawili ambao ni Amina Makilagi, Aeshy Hilali na wakuu wa taasisi za TPSF na TPDC.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles