25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

‘WATANZANIA CHANGAMKIE FURSA YA HIJA ISRAEL’

Mkurugenzi Mtendaji Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Devota Mdachi

Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam

WATANZANIA wameshauriwa kuchangamkia fursa ya kutembelea  maeneo matakatifu Israel kwa gharama nafuu inayokadiriwa kuwa kati ya Dola za Marekani 1700 na 1800.

Hayo yalisemwa   Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mtendaji Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Devota Mdachi.

Alisema  wadau wa utalii   Israel wangependa kuona Watanzania wanatembelea  nchi hiyo.

Katika ziara ya TTB nchini humo, Mdachi aliongozana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Aloyce Nzuki ambaye alikuwa kiongozi wa msafara.

Walitembelea Israel kwa siku tatu na walikutana na wadau wa sekta ya utalii na kuwaeleza  vivutio vilivyopo nchini.

“Tumetembelea maeneo mengi ya kiroho ikiwamo miji ya Nazareth na Jerusalem.

“Wenyeji wetu wamenipa ujumbe kuwa wanahitaji Watanzania waende wakahiji katika maeneo hayo kwa bei nafuu inayokadiriwa kuwa kati ya Dola za Marekani 1700 na 1800.

“Fursa hii ni nzuri tafadhali tusiiache kwa sababu mbali ya hija lakini kuna mambo mengi mengine.  Watakaokwenda watakutana na raia wa mataifa mengine watawauliza kuhusiana na Tanzania,  maana yake mtageuka mabalozi wetu na kuvutia watalii wengi zaidi,” alisema Mdachi.

Alisema kiasi hicho cha Dola 1700 au 1800 kinahusisha nauli ya kwenda na kurudi, malazi   na ziara ya maeneo matakatifu ndani ya miji husika.

“Kampuni ya Another World imeahidi ifikapo Agosti mwaka huu italeta watalii kutoka Israel watakaotembelea maeneo ya Hifadhi ya Katavi, Mahale, Ngorongoro na Zanzibar,” alisema.

Mmiliki wa Kampuni ya Another World, Shlomo Carmel aliahidi kuleta watalii zaidi ya 2000 kati ya Agosti na Disemba mwaka huu.

Balozi wa Tanzania nchini humo,   Job Massima, alisema mbali ya ugeni wake katika nchi ya Israel,  amebaini kuna kuna fursa nyingi za  utalii zinazoweza kunufaisha pande zote.

Utalii ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vya mapato nchini  ambako mwaka jana sekta ya utalii iliingiza kiasi cha Dola za Marekani bilioni mbili  ikiwa ni sawa na Sh trilioni 4, mwaka 2015 iliingiza Dola bilioni 1.9.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles