Faraja Masinde, Dar es Salaam
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Tanzania (NHIF), umesema kuwa ni Watanzania milioni 4.6 tu wenye bima ya Afya sawa na asilimia nane.
Akizungumza Dar es Salaam leo Jumatano Novemba 27, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga, amesema kiwango hicho ni sawa na watu nane kati ya 100 kiwango ambacho ni cha chini mno.
“Hali hiyo inatokana na Watanzania wengi kutokuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu bima na lengo letu ni kuhakikisha kuwa hadi kufikia Juni 2020 tunawafikia Watanzania asilimia 50,” amesema.
NHIF imezindua vifurushi nafuu vipya vya huduma ya bima ya afya vya Najali Afya, Wekeza Afya na Timiza Afya ambavyo vitatambulishwa rasmi kesho Alhamisi katika Viwanja vya Mnazi Mmmoja jijini Dar es Salaam.