25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

WATANZANIA 500 WAFUKUZWA KENYA

Na Mary Mwita-Namanga

UHUSIANO  kati ya Tanzania na Kenya umeanza kuingia dosari baada ya uongozi wa Kaunti ya Kajiado kuwamuru Watanzania zaidi ya 500 wanaoishi kwenye mpaka wa Namanga  kuondoka katika eneo hilo.

Hatua hiyo ya Kaunti ya Kajado  kuwafukuza Watanzania hao imetokana na Serikali ya Tanzania kupitia Idara ya Uhamiaji kudhibiti raia wa Kenya waliokuwa wakiingia nchini holela kupitia mpaka wa Namanga wilayani Longido Mkoa wa Arusha.

Uamuzi huo wa Kenya unatajwa kuathiri uhusiano wa  jamii za   pande mbili za nchi hizo uliojengewa kwa zaidi ya miaka 60 ambako wananchi wamekuwa wakipita kwenda kila upande  kununua bidhaa bila kuzuiwa.

Baadhi ya Watanzania waliofukuzwa   Kenya  walisema  uamuzi huo wa Kaunti ya Kajiado, umewasababishia hasara kutokana na uwekezaji waliofanya nchini humo.

Shedrack Tlway  ambaye   amefukuzwa Kenya na kuacha mali zake, alisema kwa sasa amepoteza mwelekeo kwa kuwa shughuli zake za biashara alikuwa akizifanya Namanga upande wa Kenya.

Naye John Bakari alidai hatua ya kufukuzwa   Kenya imemfanya aishi kama ndege asiyekuwa na makazi ya kueleweka kwa sababu  kwa sasa amezuiwa kuishi   pande mbili za Kenya na Tanzania.

“Hata  Rais Moi (Daniel Arap) wakati anamaliza muda wa uongozi wake alipita barabara hii ya Namanga na kusimama na kutoa salamu kwa wananchi wote wa mpaka huu.

“Alitoa zawadi ya ng’ombe 10 upande wa Namanga Tanzania na Kenya kama ishara ya kudumisha uhusiano baina ya pande zote mbili.

“Kwa hali hii ninaziomba Serikali zote mbili zitafakari uamuzi huu kama njia ya kudumisha umoja.

“Kwa kweli mimi sijui niende wapi, sikujua kama nitakosa makazi kwa kufukuzwa… wanangu ambao ni wakenya wamenikataa, Tanzania pia nimekataliwa na kunyang’anywa vibali vyote, Mwenyezi Mungu nisaidie,” alisema Bakari.

Akizungumzia hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Daniel Chongolo, alisema akiwa kiongozi na mwakilishi wa Rais Dk. John Magufuli anatekeleza sheria za nchi.

Aliwataka wananchi wanaotaka kuishi nchi yoyote   wafuate sheria za nchi husika na si vinginevyo.

“Ikiwa wazazi wanataka watoto wao wasome   Kenya wafuate sheria za Kenya na Wakenya wakitaka kuingia Tanzania wafuate sheria za Tanzania. Huu ndiyo utaratibu na si vinginevyo,” alisema DC Chongolo.

Nao raia wa Kenya ambao walizungumza na mwandishi wa habari   kwa nyakati tofauti, walisema hatua ya kufukuzwa kwa Watanzania nchini humo imetokana na Serikali ya Tanzania  kuwafukuza wananchi wa nchi hiyo Machi mwaka huu.

Wahome Wafula, alisema   anashangazwa na viongozi wa Tanzania kuondoa uhusiano ambao umejengwa na waasisi wa mataifa hayo kwa miaka zaidi ya 60 kabla na baada ya Uhuru wa nchi hizo.

“Mimi naona   hatua ya viongozi wa Kenya  kuwafukuza Watanzania ni sahihi kabisa na ikiwezekana  uhusiano ufe kwa kuwa viongozi wao ndiyo wametaka iwe  hivyo,” alisema wafula.

Gazeti hili lilimtafuta Gavana wa Kaunti ya Kajiado, David Nkedianye  kupata ufafanuzi wa uamuzi huo lakini simu yake iliita bila kupokewa hadi tunakwenda mitamboni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles