30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

WATANZANIA 35,000 WAJITOKEZA KUHAKIKI TIN DAR ES SALAAM

NA KOKU DAVID,

ZOEZI la uhakiki wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kwa Mkoa wa Dar es Salaam, limekamilika na kwamba hivi sasa linaelekezwa mikoani.

Zoezi hilo ambalo lilizinduliwa Agosti 16, mwaka jana, limehitimishwa Januari 31 na watu zaidi ya elfu 35 walijitokeza kuhakiki taarifa zao.

Lengo la zoezi hilo ni kuhuisha ikiwa ni pamoja na kuiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuweza kupata taarifa sahihi za walipakodi wake.

Hata hivyo, kutokana na sababu mbalimbali, baadhi ya wananchi walishindwa kushiriki katika zoezi hilo kwa muda uliopangwa, hivyo TRA imewataka kufika katika ofisi za mamlaka hiyo katika mikoa yao ya kodi ili waweze kupata maelekezo ya uhakiki.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, anasema wale wote ambao watakuwa hawajahakiki TIN zao kwa muda uliokuwa umepangwa, wanatakiwa kuzifanyia uhakiki kabla ya kupata huduma za kulipia ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazotoka na kuingia nchini, kuhuisha leseni za udereva, kulipia ada ya mwaka ya gari, kulipa kodi nyinginezo zinazosimamiwa na mamlaka, ikiwa ni pamoja na kupata cheti cha uhalali wa ulipaji wa kodi.

Anasema kwa upande wa wananchi wanaoishi nje ya nchi, watatakiwa kuhakiki TIN zao pindi watakapokuwa wamerejea nchini na kwamba watatakiwa kuonyesha vielelezo vya kuthibitisha kuwa hawakuwepo nchini.

Kwa upande wa wale watakaobainika kuwa na TIN zaidi ya moja, utaratibu uliopo ni wa kuhuisha taarifa ya TIN mojawapo kati ya hizo na kwamba zitakazobaki zitafungiwa.

Iwapo mtu atakuwa na madeni ya kodi katika mojawapo ya TIN hizo au zaidi, ataendelea kudaiwa kama kawaida kwa mujibu wa sheria.

Pia kwa mtu anayedaiwa kodi, hata kama alikuwa na TIN zaidi ya moja na kati ya hizo mojawapo inadaiwa au zaidi, mamlaka haitamzuia kuhakiki TIN yake na kwamba atahakiki kama kawaida na deni litabaki pale pale na atatakiwa kulilipa.

Baada ya zoezi hili kumalizika katika awamu ya kwanza ya uhakiki kwa Mkoa wa Dar es Salaam, linatarajiwa kuanza rasmi Februari 15, mwaka huu katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Morogoro, Tanga na Pwani.

Baada ya kumalizika katika mikoa hiyo, tarehe ya kuanza kuhakiki katika mikoa mingine iliyobaki itatangazwa baadaye.

TRA ambayo imepewa jukumu na Serikali la kuhakikisha inakusanya kodi kutoka kwa kila mtu anayestahili kulipa kodi kwa mujibu wa sheria ili iweze kufanya mambo mbalimbali ya maendeleo kwa jamii, imewataka wananchi kuwa wazalendo kwa kuendelea kujitokeza kwa wingi ili kuirahisishia Serikali kufanya kazi kwa urahisi.

Pia kwa wanachi wote wa mikoa ambayo zoezi hili linatarajiwa kuanza, wanatakiwa kushirikiana kwa karibu na maofisa wa mamlaka watakaoendesha zoezi hilo ili kuweza kulikamilisha kwa wakati uliopangwa.

Pamoja na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza katika Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa zoezi hilo, TRA imejipanga kuhakikisha hazijitokezi tena ili kuweza kumaliza haraka na kulihamishia katika mikoa mingine ambayo itaangazwa baadaye.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles