30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 30, 2023

Contact us: [email protected]

Watanzania 20,000 wamepata chanjo ya Sinopharm-Wizara

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imesema mpaka kufika Oktoba 23, mwaka huu jumla ya watu 20,000 wamechanja chanjo aina ya Sinopharm ambapo imedai lengo ni kila siku watu 100,000 waweze kuchanja huku akitanabaisha kwamba zaidi ya watu 1,000,000 wameweza kupata chanjo ya Johnson and Johnson ambayo ililetwa awali kutoka nchini Marekani.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Oktoba 25, 2021 jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Abel Makubi wakati akifungua mkutano ambao uzikutanisha Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) na Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali (NG’Os) ambao ni wadau wa sekta ya afya kwa lengo la kushirikisha katika kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO-19.

Katibu Mkuu huyo amesema wamekutana na wadau hao kufuatia hivi karibuni NGÓs kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan na kudai kwamba wapo tayari kushirikiana na Serikali kutoa elimu na kuhamasisha watu kuchanja ili kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO 19.

Prof. Makubi amesema mpaka kufika Oktoba 23, mwaka huu jumla ya watu 20,000 wamechanja chanjo ya Sinopharm na kuongeza kuwa lengo ni kila siku watu 100,000 waweze kuchanja huku akitanabaisha kwamba zaidi ya watu milioni moja wameweza kupata chanjo ya J J ambayo ililetwa awali kutoka Marekani.

“Sasa wamechanja zaidi ya watu milioni moja kwenye zile zingine zimeisha na hizi za sasa hivi Sinopharm mpaka tarehe 23 tulikuwa tumechanja watu 20,000 sasa lengo letu  kuchanja watu 100,000 kila siku tunataka kuongeza ushirikiano na wadau,”amesema.

Amesema maeneo ambayo wanahitaji kushirkiana zaidi ni katika kuongeza suala la uchanjaji uweze kuwa juu zaidi ambapo  sasa hivi wamefikia  kiwango cha kuchanja wananchi  50,000 kwa siku kabla J J haijaisha.

“Tumeona Serikali peke yetu hatuwezi hivyo ni lazima tuwashirikishe hawa wadau watatusaidia katika hili tunataka tuendelee kuongeza kuwapa elimu zaidi kuhusiana na kuchanja,”amesema.

Aidha, Katibu Mkuu huyo amesema Serikali kupitia Wizara yake itaendelea kuzisimamia NG’Os zote ambazo zimekuwa zikipata fedha kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo kwa kutaka ziende kwenye lengo lilokusudiwa.

“Tuna wajibu wa kufuatilia tumekuwa tukifanya hivyo ndio maana tumewaita, kama umepewa fedha mfadhili yoyote lazima tujue zinaenda kulenga kukabiliana na COVID 19  kinyume na hapo lazima tuwekeane mipaka kwamba hapo sio tuende njia hii tufuate muongozo wetu,”amesema.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (TAMISEMI) anaeshughulikia afya, Dk. Grace Maghembe amesema wamefanikiwa katika chanjo awamu ya kwanza kwa kutoa elimu kwa makundi mbalimbali jinsi ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Amesema wamejipanga kuendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ili jamii iendelee kupata chanjo huku akiwaomba Waandishi wa Habari kuendelea kupaza sauti juu ya umuhimu wa watu kuchanja.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali (NACoNGO), Lilian Badi amesema wao kama wadau wapo  kwenye jamii hivyo wapo tayari kutoa elimu hivyo wanaomba wapewe nafasi ili waweze kuelimisha jamii kuhamaisha chanjo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles