|Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Serikali ya China imetoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 20 kwenda kusoma masuala ya gesi na mafuta nchini humo.
Akizungumza katika hafla ya kuwaaga wanafunzi hao, Katibu wa Wizara ya Nishati, Hamis Mwinyimvua amesema lengo la ufadhili huo ni kuhakikisha Watanzania wanajengewa uwezo wa kushiriki katika uendelezaji wa rasilimali ya mafuta na gesi ipasavyo.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, iliingia makubaliano na Serikali ya China kutoa ufadhili wa fani ya mafuta na gesi kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili na Uzamivu ambapo kwa mwaka huu wameongeza hadi wale wa shahada ya kwanza ambapo tangu programu hii ianzishwe wanafunzi 100 wamefadhiliwa.
“Niwapongeze Watanzania wenzetu waliopata ufadhili kwa mwaka huu, haikuwa kazi rahisi na maombi yalikuwa mengi ila wao wamechaguliwa katika nafasi hizo na mjue mnaenda kuwakilisha nchi hatimaye mlete ujuzi nchini.
“Tunaishukuru serikali ya China tumekuwa tukisaidiana katika mambo mengi hasa hili la ufadhili wa masomo ya elimu ya juu, ufadhili huu ni mhimili muhimu katika nchi yetu kuwa na wataalamu wa kutosha katika sekta ya nishati ambayo ni injini ya kufikia katika Tanzania ya Viwanda,” amesema.
Kwa upande wake muwakilishi wa Balozi wa China, XU Chen amesema serikali yake iliamua kutoa ufadhili huo kwa Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano ili kusaidia kupata wataalamu katika sekta ya nishati jambo ambalo litaimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili.
“Tanzania ni nchi yenye utajiri wa mafuta na gesi ila hawana watu wenye taaluma ya kutosha jinsi ya kuvumbua rasilimali hizo na hii ndiyo sababu imetufanya tutoe ufadhili huu na tunafuraha kuona ushirikiano wa nchi hizi mbili unakua,” amesema Chen.