33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Watano wapitishwa urais CCM Z’bar

Na Waandishi Wetu  ZANZIBAR/DAR/DOM)

HATIMAYE Kikao cha Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichojifungia jana  kimetoka na mapendekezo ya majina ya wanachama watano kati ya 32 waliochukua fomu  kuwania nafasi ya urais kupitia chama hicho visiwani Zanzibar. 

Pamoja na kwamba safari hii CCM imesema kuwa imeamua kufanya siri juu ya majina hayo, kwa kile ilichodai kuwa inakwepa kutengeneza makundi lakini MTANZANIA Jumapili limefanikiwa kupata majina hayo kupitia vyanzo vyake vya ndani.

Kwa mujibu wa taarifa hizo waliopendekezwa na kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi,  Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Khamis Mussa Omar. 

Yumo pia Dk. Khalid Salum Mohammed ambaye alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar kabla ya kuondolewa katika nafasi hiyo kwa tuhuma za kuanza mbio za urais mapema.

Wengine ni aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof. Makame Mbarawa. 

Ratiba inaonyesha majina hayo sasa yatapelekwa Dododma ambapo Julai 9 Kamati Kuu ya Halmashauri ya Taifa itapendekeza majina matatu.

Julai 10, Halmshauri Kuu ya Taifa ya CCM  itachagua jina moja la mgombea.

Julai 11 – 12, Mkutano Mkuu wa CCM utathibitisha jina la mwanachama atakayesimama katika uchaguzi wa urais Tanzania na  upande wa Zanzibar.

Wakati vikao vya juu vya kuchuja majina ya wagombea nafasi ya urais CCM vikianza kesho jijini Dodoma, Kwa upande wa Zanzibar tayari vikao vya juu vya kujadili wagombea urais vilikwishaanza tangu Julai 1- 2 kwa  Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar kuketi kuchuja majina.

Julai 3 kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili Zanzibar kiliketi kwa ajili hiyo hiyo.

TAARIFA YA CCM ZANZIBAR

Akizungumza na waandishi wa habari jana jioni, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi alisema wameamua kufanya siri juu ya majina hayo matano ili kulinda umoja ndani ya chama hicho.

Alisema kamati hiyo iliyopendekeza majina hayo matano ni sehemu muhimu ya maandalizi na uchujaji wa majina ya wagombea watano wanaotakiwa kuwasilishwa katika Kamati Kuu kwa ajili ya kujadiliwa tena na kumtafuta mgombea mzuri mwenye sifa 12 zikiwemo hekima, kuaminika, kuthamini muungano na Mapinduzi ya Zanzibar.

Dk. Mabodi alisema baada ya Kamati kuu kujadili kwa kina majina hayo matano itapendekeza majina matatu na kuyapeleka Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambayo itachagua jina la mtu mmoja ambaye atapeperusha bendera ya CCM kwa nafasi ya urais wa Zanzibar.

Alisema baada ya hatua hiyo mgombea huyo atapelekwa katika Mkutano Mkuu wa CCM kwa ajili ya kuthibitishwa na kupata baraka za wajumbe wote wa Kamati Kuu ya chama hicho na kuendelea na michakato mingine.

Dk.Mabodi, alisema baada ya kukamilika kwa mchakato huo itaendelea awamu ya pili ya uchukuaji wa fomu kwa nafasi za ubunge, uwakilishi na Udiwani na kufuata utaratibu wa miongozo ya CCM.

Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo, amewasifu viongozi kwa ukomavu wao wa kisiasa kwa kufuata Katiba, miongozo na kanuni za CCM kwa kutobeba wagombea mifukoni.

DK. MABODI: UKITOA SIRI MAJINA HUNA SIFA 

Alisema kuwa kikao hicho kimesisitiza usiri kwa wagombea hao kwani ndani ya CCM ikibainika miongoni mwao kuna mtu kakiuka utaratibu anaweza kuondolewa na kuchaguliwa mtu mwingine.

“Lazima tuenzi siri za vikao hivyo ni muhimu sana watu wote kuheshimu maamuzi ya vikao na kufuata utaratibu uliowekwa ndani ya CCM,” alisema Dk.Mabodi.

Mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu ulianza Juni 15 hadi 30, mwaka huu ambapo jumla ya makada 32 walijitokeza kuchukua fomu hiyo ambao ni Mbwana Bakari Juma, Ali Abeid Karume, Mbwana Yahya Mwinyi, Omar Sheha Mussa, Hussein Ali Mwinyi, Shamsi Vuai Nahodha, Mohamed Jafar Jumanne Mohamed Hijja Mohamed, Issa Suleiman Nassor.

Wengine ni Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, Mwatum Mussa Sultan, Haji Rashid Pandu, Abdulhalim Mohamed Ali, Jecha Salum Jecha, Dk.Khalid Salum Mohamed, Rashid Ali Juma, Khamis Mussa Omar, Mmanga Mjengo Mjawiri, Hamad Yussuf Masauni Mohamed Aboud Mohamed, Bakari Rashid Bakar, Mgeni Hassan Juma, Ayoub Mohamed Mahmoud, Hashim Salum Hashim, Fatma Kombo Masoud, Hasna Attai Masoud, Maalim Hamad Idd Hamad Idd, Pereira Ame Silima, Shaame Mcha, Mussa Aboud Jumbe na Moudline Cyrus Castico.

DODOMA KUMEKUCHA

Dodoma ambako vikao vya juu ya maamuzi vya CCM vinatarajiwa kuanza kuketi kuanzia kesho vimelifanya jiji hilo kuchangamka kutokana na kuonekana wageni wengi.

Mwandishi wa MTANZANIA, Ramadhani Hassan anasema; “Ukiwa Jijini hapa utaona tofauti na siku za nyuma kutokana na idadi ya watu kuongezeka huku wafanyabishara wakionekana kuchangamkia fursa hiyo”.

Vikao hivyo ambavyo vinatarajiwa kuanza Dodoma kesho Julai 6 na 7 ni cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ambacho kitaanza kuchuja majina na kitaketi katika ukumbi ya Jakaya Kikwete uliopo njia ya kwenda Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) Jijini hapa.

Julai 8 kitafuatia kikao cha  Kamati ya Usalama na Maadili CCM na  Julai 9- Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, ambayo itatoa mapendekezo ya majina matano NEC

Julai 10, NEC itapendekeza majina matatu kwenye Mkutano Mkuu.

Julai 11 -12, Mkutano Mkuu wa CCM utachagua jina moja la mgombea wa urais wa Tanzania.

Kutokana na uwepo wa vikao hivyo pembezoni mwa   ofisi za makao makuu ya chama hicho (White House) wafanyabiashara wameonekana kuchangamkia fursa ya kuuza vitu mbalimbali ambavyo wanachama na wasio wanachama wananunua.

MTANZANIA lilifika katika eneo hilo na kujionea jinsi ambavyo biashara imechangamka ikiwemo ile ya  mashati,magauni yenye nembo ya CCM,matunda na chakula.

Juma Matokeo ambaye ni mfanyabishara alisema kipindi hiki, hali ya biashara kwa upande wake imekuwa nzuri kwani wengi wamekuwa wakifika katika eneo hilo na kununua mashati, magauni na urembo mbalimbali ambao una rangi ya CCM.

“Mimi hapa nauza mashati na vitu mbalimbali vyenye nembo ya CCM mfano bangili, shanga, biashara imekuwa nzuri kila mmoja anayekuja hapa ananunua kitu,”alisema.

Naye, Mwajuma Mwashamba alisema mara baada ya Rais kurejesha fomu ya kugombea urais biashara imechangamka katika eneo hilo.

“Mimi nauza mashati tu, biashara imekuwa nzuri nilikuwa na mzigo wa muda mrefu lakini sasa hivi nakaribia kuumaliza,”alisema.

Naye,Ramadhan Juma ambaye ni wakala wa kutoa fedha jirani na Ofisi za CCM alisema biashara imekuwa nzuri kwani wanaotoa na kuingiza fedha ni wengi.

“Wengi wanatoka kwenye hilo geti la CCM wanakuja hapa kutoa na kuweka fedha nadhani kutakuwa kuna kitu lakini nilisikia ku kulikuwa kuna vikao vya Wenyeviti wa Mikoa wa CCM,”alisema.

Pia, katika maeneo mengine hali ya biashara imechangamka kuanzia katika migahawa ya chakula.

Nyumba za wageni nyingi zimeonekana kuwa na wageni ambapo Mfanyakazi wa Hoteli ya Kidia ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini  alisema kwamba idadi ya watu imeongezeka tangu wiki iliyopita.

“Watu ni wengi wengine wamekuja tu kuangalia jinsi ambavyo vikao vya CCM vitafanyika ila wiki iliyopita pia kulikuwa kuna watu wengi kutokana na Wenyeviti wa CCM kuwepo hapa,”alisema.

Naye,mfanyakazi wa Bustani ya Nyerere Square iliyopo katikati ya Jiji la Dodoma,Mwapwani Yahaya alisema watu wengi wamekuwa wakikaa katika bustani hiyo kwa ajili ya kupanga mambo mbalimbali lakini kwa sasa ni kama wameongezela.

“Wameongezeka ila wengi wamevaa rangi za kijani na njano labda kwa sababu hapa ni jirani na ofisi za Chama cha Mapinduzi,”alisema.

Fundi Cherehani,Raju Jumaa alisema watu wengi wamekuwa wakifika ofisini kwake kwa ajili ya kushona mashati yenye rangi za CCM.

“Biashara imekuwa nzuri mimi nashona mashati tangu wiki iliyopita nina oda wateja wameongezeka,wengine wanatoka mikoani wanakuja kushonea hapa kwetu jirani na White House,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles