25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

WATANO WAFA MGODINI, SITA WAJERUHIWA

machimbo

NA LUCAS RAPHAEL- NZEGA

WATU watano wamefariki dunia na sita kujeruhiwa baada ya kudondokewa na mwamba wa mawe katika mgodi wa zamani wa Resolute uliopo Nzega, Tabora.

Akizungumzia tukio hilo jana, Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Godfrey Ngupulla, alisema limetokea juzi saa saba mchana baada ya kundi la wachimbaji wadogo wa Mgodi wa Umoja kuvamia eneo hilo lililopigwa marufuku na Serikali.

Ngupulla alisema eneo hilo limeshapigwa marufuku kuchimbwa kutokana na hatari iliyopo lakini baadhi ya wachimbaji wamekuwa wakiingia kwa kificho kuchimba hali iliyosababisha kuleta maafa.

Aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Joseph Mpenda ambaye ni mkazi wa Shinyanga, Mohamed Mohamed, mkazi wa Singida, Manona Nyombi, mkazi wa Bariadi, Modesta Leonard, mkazi wa Nzega na mwingine bado hajatambulika.

Aliwataja majeruhi kuwa ni Kangwa Mayenga (22) ambaye ni mkazi wa Bariadi, Agness Antony (40), mkazi wa Chato, Deus Alphonce (45), mkazi wa Igunga na Mathias Mapunda, mkazi wa Chato.

Alisema majeruhi wote kwa pamoja wanaendelea kupata matibabu na wawili ambao majina yao hayakupatikana kutokana na kuwa mahututi.

Pia alisema Serikali haitamfumbia macho mtu yeyote atakayekamatwa katika eneo hilo na kufunga mgodi uliopo jirani wa namba saba.

Aliwataka kuwa na nidhamu ya kusikia kilichosemwa na viongozi wakati hatua za kutafuta vitalu vingine zikiendelea.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wachimbaji waliokuwa wakiokoa miili ya marehemu walisema sababu ya kuingia katika eneo hilo la Serikali ni kutokana na kukosa maeneo ya kuchimbia.

“Endapo Serikali ingetoa maeneo kwa wachimbaji wadogo, maafa hayo yasingetokea,” alisema David Juma ambaye ni mchimbaji mdogo.

Alisema kwa sasa eneo walilopewa ni dogo ndiyo maana wanahama na kuingia katika maeneo hatarishi.

“Tunaiomba Serikali itusaidie tusiendelee kupoteza maisha yetu, sisi hatuna fedha na maisha yetu yote ni uchimbaji hivyo viongozi watusikilize ili tusipoteze maisha,” alisema David.

Kwa upande wake, Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe, akiwa katika maeneo hayo alisema tayari hatua za awali zimeanza kuchukuliwa na Wizara ya Nishati ya Madini za kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata eneo la kufanyia shughuli zao ili kuepusha maafa.

Pia aliwataka kuacha kuvamia maeneo ya Serikali hasa yale ya hatari ili kuepusha vifo visivyokuwa vya lazima kwa wakati huo.

Bashe alisema endapo wachimbaji hao wataendelea kuvamia maeneo ya Serikali hatasita kuishawishi kuwafungia leseni walizopewa ili maeneo hayo yabaki wazi kama hawataelewa.

Naye Ofisa Madini wa Tabora, Clement Mayala, alisema Serikali ilishapiga marufuku kuingia maeneo hayo na mchakato wa kutoa vitalu vingine unaendelea kwa wachimbaji wadogo.

Katika hatua nyingine, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, aliwataka wachimbaji kuchukua tahadhari hasa katika kipindi hiki cha masika kwa kuwa ardhi imelowa maji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles