29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Watalii zaidi ya 2000 watua na meli kubwa bandarini Dar


Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Bandari ya Dar es Salaam imepokea meli kubwa Norwegian Cruise Line Dawn yenye urefu wa mita 294 iliyobeba watalii zaidi ya 2000 na wafanyakazi 1000.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 16, 2024 jijini Dar es Salaam baada ya kuwasili kwa meli hiyo, Mkurugenzi wa bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho amesema ujio wa meli hiyo umedhihirisha maboresho makubwa yaliyofanywa hasa katika uchimbaji wa kina kirefu na upanuzi wa lango la kuingilia.

“Kwa bandari ya Dar es Salaam hii ndio meli ndefu ya kwanza kwa ukubwa wake kuweza kuingia nchini tangu uhuru, hii imetokana na maboresho yaliyofanyika katika kuchimba kina kirefu chenye mita 14 kwenda chini na upanuzi wa lango la kuingilia meli. Pia upanuzi huu tunajivunia sana na kuishukuru serikali ya awamu ya sita,”amesema Mrisho.

Amesema meli hiyo umechukua nafasi ya meli tatu ambazo wanazihudumia kila siku yaani gati namba 2 na 3.

Ameongeza kuwa matarajio ya bandari hiyo ni kuhudumia meli zenye urefu wa mita 305.

Kwa upande wake Nahodha Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Nchini(TPA), Abdula Mwingamno amesema meli yenye ukubwa huo haijawahi kuingia kwenye bandari yeyote za TPA.

Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho akizungumza na waandishi wa habari baada ya Meli Norwegian cruise line Dawn kuwasili yenye urefu mita 294 yenye watalii zaidi ya 2,000 na Wafanyakazi 1,000.

Amesema kuboresha mlango wa kuingilia meli utasaidia kuingiza bandari ya Dar es salaam,Tanga na Mtwara kwenye ushindani wa kibiashara.

Aidha ametoa rai kwa wafanyabiashara kuendelea kuingiza meli zenye ukubwa wa hadi mita 305 muda wowote na si kama ilivyokuwa awali ambapo meli zenye ukubwa huo zilikua zikiingia mchana lakini sasa mda wowote zinaingia kutokana na maboresho hayo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii (TTB), Damus Mfugale amesema zao la utalii limeendelea kukua katika sekta hiyo kutokana na ongezeko la watalii linaloendelea.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Nchini (TTB), Damas Mfugale.

Amesema watalii hao ambao ni watalii wa meli ni mkakati wa Serikali kuendeleza na kukuza utalii huo kwani utasaidia kuongeza pato la taifa na ongezeko la fedha za kigeni nchini.

Amesema baadhi ya watalii hao waliowasili watatembelea vivutio mbalimbali ikiwemo mbuga ya Selous na maeneo ya historia Bagamoyo na wengine kwenye vivutio mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Nahodha Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA), Abdula Mwingamno

“Ujio wa meli hii kubwa ni mkakati wa kukuza sekta ya utalii lakini pia muendelezo wa utalii wa meli ambao ni moja ya mkakati wa serikali kuhakikisha utalii huo unakua kwa kasi hapa nchini,”amesema Mfugale.

Amesema ujio wa meli hiyo ni mwanzo wa kuingia meli nyingine za utalii ambapo Februari,2024 kupokea meli nyingine kubwa ya watalii nchini ikiwa ni muendelezo wa kuhakikisha zao la utalii wa meli linakua.

Meli hiyo iliyotia nanga leo ikitokea Mombasa ikiwa inaendelea na safari zake za utalii Duniani itaondoka nchini jioni ya leo januari 16,2024.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles