25.7 C
Dar es Salaam
Monday, November 28, 2022

Contact us: [email protected]

Watalaamu waonya ongezeko magonjwa yasiyoambukiza

Na EVALINE KITOMARY -DAR ES SALAAM

KUTOKANA na kuendelea kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza, wataalamu wa afya wamewasisitiza wananchi kuweza kuacha mtindo mbaya wa maisha badala yake wazingatie lishe inayotakiwa na ufanyaji mazoezi.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa kuhitimisha wiki ya magonjwa yasiyoambukiza ambayo ilianza Novemba 07 hadi 14, Mkuu wa Mkoa huo Abubakar Kunenge alisema magonjwa hayo yamekuwa yakigharimu pato la taifa na uchumi wa mtu mmoja mmoja.

“Takwimu za WHO zinaonesha magonjwa yasiyoambukiza yanachangia zaidi ya vifo milioni 41 ambayo  sawa na asilimia 71 ya vifo vyote milioni 57 vilivyotokea mwaka 2018, taarifa ya shirika la Maendeleo Duniani  (UNDP) zinaonesha kuwa pamoja na changamoto za kiafya magonjwa hayo yanaathiri sana nyanja zingine za maisha na jamii kwa ujumla.

“Inabashiriwa kuwa ifikapo mwaka 2033 gharama zitokanazo na huduma ya magonjwa haya yatafikia Dola za Marekani Trilioni 47,fedha ambazo zingeweza kupunguza umasikini kwa watu Bilioni 2.5 kwa miaka 50 na kwa nchi za uchumi wa kati na chini magonjwa hayo yanagharimu Dola za Marekani Trilioni saba kwenye kipindi cha 2011-2025.

“Gharama hizo zinatokana na huduma za matibabu na nguvu kazi inayopotea na makadirio yanaonesha kuwa gharama za huduma kwa wagonjwa yasiyoambukiza itafikia asilimia 75 ya mzigo wote wa bajeti ya Afya duniani huku ugonjwa wa kisukari pekee ukisababisha gharama zaidi ya dola za Marekani bilioni 465 sawa na asilimia 11 ya bajeti yote ya Afya duniani,”alibainisha Kunenge.

Akitoa mifano ya gharama za huduma za afya nchini Kungene alisema wagonjwa wa matatizo ya figo kushindwa kufanya kazi wanahitaji huduma ya kusafisha damu angalau mara tatu kwa wiki moja.

“Gharama za kusafisha kwa kiwango cha kawaida katika hospitali za serikali ni Sh 200,000 kwa siku bila ya gharama nyingine ya matibabu, usafiri na chakula kwa wiki mmoja mgonjwa atatumia Sh 600,000 na kwa mwezi Sh milioni 2.4 ambayo ni sawa na Sh milioni 28 kila mwaka.

“Gharama hii ni kubwa kwa watanzania wengi lakini gharama za kuzuia tusipate madhara yatokanayo na magonjwa haya ni nafuu sana hivyo tunawaasa wananchi kuzingatia msemo wa ‘Kinga ni Bora, Kuliko Tiba’ kwasababu tatizo hilo lipo nchini na linaongezeka kwa kasi kuna ongezeko la asilimia 24 ndani ya miaka miwili ni kubwa linahitaji mikakati kukabiliana nalo,”alifafanua.

Alisema ni vema wananchi wakaunganisha nguvu pamoja katika kuzuia vihatarishi zinavyoelezwa kama kudhibiti matumizi ya vilevi na kuhamasisha jamii kushiriki mazoezi au shughuli za nguvu.

“Kuzingatia mlo kamili na unaofaa kwa kuondoa au kupunguza chumvi, sukari na mafuta na kwa pamoja tujipange kukabiliana na madhara mengine yatokanayo na uharibifu wa mazingira na tabia ya nchi.

“Kuhusu mazoezi hapa niweke msisitizo kwa sekretarieti ya mikoa na mamlaka za serikali za Mitaa kuendeleza utaratibu wa mazoezi uliozinduliwa na makamu wa Rais mama Samia Suluhu wa kila jumamosi ya pili ya kila mwezi kufanya mazoezi pamoja”alieleza Kunenge.

Kunenge pia alikumbusha kuundwa kwa kamati ya pamoja ya uratibu wa shughuli zote za udhibiti wa magonjwa hayo iliyoagizwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ili kuweza kuwa na mwongozo wa pamoja katika kuunda na kutekeleza mipango na mikakati ya kitaifa.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Chama cha Wagonjwa wa Kisukari nchini Prof Andrew Swali alisema ugonjwa huo unaongezeka ambapo kwa miaka ya nyuma kati ya watu 100 ni mtu mmoja alipatikana na ugonjwa huo huku kwa sasa kati ya watu 100 watu tisa wanakuwa na ugonjwa huo.

“Zamani watu wazima ndio walikuwa wanapata lakini hata sasa hivi miasha yamebadilika hata vijana wanapata magonjwa haya sasa tujiulize kwanini zamani watu walikuwa hawapati wengi ni kwasababu ya mtindo mbaya wa maisha watu wanakula bila kushughulisha miili yao,”alisema Prof Swai.

Katika vipimo vilivyofanyika kwa siku mbili takribani watu  5,067 walijitokeza kupima magonjwa yasiyoambukiza ambapo zoezi hili lilifikia kikomo jana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,444FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles