31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Wataka Serikali iwatafutie soko la shayiri

Na JANETH MUSHI-MONDULI

WAKULIMA wadogo wa shayiri kutoka vijiji vinne vilivyopo Kata za Monduli Juu na Emairete wilayani hapa, wameiomba Serikali kuwatafutia masoko ya zao hilo kama ilivyofanya kwa zao la korosho mkoani Mtwara.

Walitoa ombi hilo jana katika Kijiji cha Emairete wakati wa mkutano wa wakulima uliohudhuriwa na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli.

Mmoja wa wakulima hao, Loretu Meyan, alisema kwa zaidi ya miaka 20 Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) chini ya Kampuni ya Kimataifa ya ABInBev, ilikuwa ikiwakopesha mbegu na dawa kisha hununua shayiri hiyo, ila kuanzia mwaka huu hawajaingia nao mkataba tena.

Meyan alisema katika kata hizo mbili wamekuwa wakitegemea kilimo cha shayiri kujiongezea kipato na kusomesha watoto, hivyo kuanzia sasa hawajui kilimo cha kuendelea nacho kwani msimu wa kupanda mazao mengine umeshapita.

“Serikali ituangalie kwa jicho la huruma kwani zaidi ya hekari 3,000 hazijapandwa, tulikuwa tunasubiri mbegu za mkopo mwaka huu ili tupande shayiri, tulikuwa tunasomesha watoto kupitia zao hili ambalo limekuwa na faida kwetu kwa kiasi kikubwa.

 “Tunaiomba Serikali itutafutie masoko ili tukipanda zao hili tujue pa kuuzia au ifanye kununua shayiri kutoka kwetu kama ambavyo ilifanya kule Mtwara kununua korosho,” alisema Meyan.

Naye Mboyo Kayai alisema nia ya Serikali ya kuelekea uchumi wa kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025 itatekelezeka zaidi iwapo itaangalia wakulima wadogo.

“Falsafa ya Serikali ya ‘hapa kazi tu’ na ‘kuelekea uchumi wa kati wa viwanda’ itatekelezeka vipi kama tunarudisha majembe nyuma? Kilimo hiki kina msaada mkubwa kwetu kwani sasa hivi husikii Masai kaiba ng’ombe, tumejikita katika kilimo,” alisema Kayai.

Naye Katibu wa Chama cha wakulima Monduli Juu, Moloimet Sane, alisema Serikali iangalie namna ya kuwasaidia wakulima na kwamba Januari 13 ndipo walipopewa taarifa za kutokuendelea na mkataba wa awali.

Kwa upande wake, ofisa ushirika kutoka halmashauri hiyo, Ester Tarimo, aliwaeleza wakulima hao kuwa watafuatilia na kupeleka suala hilo ngazi za juu kutafutiwa ufumbuzi.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Monduli, Salim Omary, alisema licha ya wananchi hao kukosa mbegu hizo, halmashauri hiyo pia itapoteza mapato waliyokuwa wakitegemea.

“Tutafuatilia suala hili kwani hata zao la mtama mnaloambiwa mlime linahitaji utaalamu siyo la kubahatisha, tukiwa kama Serikali tutafuatilia na kupeleka suala hili ngazi husika,” alisema Omary.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles