23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Watahiniwa 900,000 kufanya mtihani darasa la saba leo

Waandishi wetu – Dar es salaam/Dodoma

JUMLA ya watahiniwa 947,221 wanatarajiwa kuanza mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE) 2019 leo, huku Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) likiwaonya wasimamizi, wamiliki wa shule na walimu kutojihusisha na udanganyifu.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa yeyote atakayefanya udanganyifu, baraza halitasita kuchukua hatua kama ilivyovifutia matokeo baadhi ya shule katika mitihani ya mwaka jana.

Katika matokeo ya mwaka jana, shule zilizofanya udanganyifu na kufutiwa matokeo na baadaye kurudia mitihani katika vituo vipya ni pamoja na shule zote za Halmashauri ya Chemba, New Hazina (Kinondoni), Aniny Nnduni na Fountain of Joy (Ubungo), Alliance na Kisiwani (Mwanza) na Kondoa Integrity (Kondoa).

Alipoulizwa endapo shule hizo kama zimeruhusiwa kuwa vituo vya mitihani mwaka huu, Dk. Msonde alisema bado vimefungwa hadi pale baraza litakapojiridhisha ndipo vitaruhusiwa tena.

Katika hilo, alisema watahiniwa wa shule hizo watafanyia mitihani kwenye vituo ambavyo vimepangwa na baraza.

Alisema kati ya watahiniwa 947,221 waliosalijiwa kufanya mitihani mwaka huu, 902,262 watafanya kwa lugha ya Kiswahili na 44,959 watafanya kwa lugha ya Kiingereza ambayo wamekuwa wakiitumia katika kujifunzia.

Dk. Msonde alisema watahiniwa wenye mahitaji maalumu wapo 2,678 kati yao 81 ni wasioona, 780 wenye uoni hafifu, 628 wenye ulemavu wa kusikia, 325 ulemavu wa akili na 864 ulemavu wa viungo vya mwilini.

“Baraza linatoa wito kwa wasimamizi wote walioteuliwa kufanya kazi yao ya usimamizi kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu, wasimamizi wanaelekezwa kufanya kazi yao kwa weledi na kwa kuzingatia kanuni za mitihani na miongozi waliyopewa,” alisema Dk. Msonde.

Aliwataka wasimamizi kuhakikisha wanalinda haki ya watahiniwa wenye mahitaji maalumu ikiwa ni pamoja na kuongezewa muda wa dakika 20 kwa kila saa kwa somo la Hisabati na dakika 10 kwa kila saa kwa masomo mengine.

Dk. Msonde alisema wamiliki wa shule zote wanatakiwa kutambua kuwa shule zao ni vituo maalumu vya mitihani, hivyo hawatakiwi kuingilia majukumu ya wasimamizi katika kipindi chote cha ufanyikaji wa mtihani huo.

“Baraza halitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayebainika kujihusisha au kusababisha udanganyifu wa mitihani kufanyika kwa mujibu wa sheria za nchi yetu na kanuni za utumishi wa umma,” alisema. 

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Seif Deus, ametoa angalizo kwa walimu watakaosimamia mitihani hiyo kwa kuwataka kutojihusisha  na vitendo vya udanganyifu na wizi wa mitihani.

Akizungumza jana jijini Dodoma na waandishi wa habari, Deus alisema CWT inawataka walimu nchini kusimamia mitihani hiyo kwa uadilifu na uaminifu na kutojihusisha na vitendo vya kutoa majibu kwa wanafunzi.

“Kwanza niwatakie kila heri wanafunzi, wanahitimisha miaka yao saba, wanajumuisha yale yote waliyofundishwa, ila pia niwatakie kila la heri walimu wangu ambao wanaenda kusimamia mitihani hiyo.

“Moja ya kazi zetu ni utetezi, sasa walimu wangu naomba niwaambie kazi ya kufundisha wamemaliza wiki iliyopita tuwaache watoto wafanye mitihani. Natamani siku moja uaminifu wa zamani urudi tena, zamani kulikuwa hakuna mgambo, hakuna askari.

“Lakini sasa hivi kutokana na uaminifu kupungua, imekuwa sasa mgambo walinde uaminifu wetu, tumeona haitoshi tumepewa Jeshi la Polisi walinde wakiwa na SMG ili kuutafuta uaminifu.

“Uaminifu ukizidi kupungua kuna siku tutapewa vifaru waje walinde hiyo mitihani, kwahiyo niwaombe walimu wangu wawe waaminifu kwenye zoezi la mitihani, wawaache watoto wafanye mitihani, kazi ya kufundisha waliishamaliza,” alisema Deus.

Alipoulizwa kuhusu hatua watakazochukua iwapo itabainika kuna walimu wamehusika na njama ya kutoa majibu ya mitihani, alisema kuna mamlaka ambazo zinahusika na mambo hayo wao hawawezi kusema jambo lolote.

“Kwanza sisi sio mamlaka ya nidhamu, sisi sio dola, ikitokea hivyo tunaacha vyombo vyenye mamlaka kufanya kazi yao, lakini kwanini nimewaasa walimu wangu, moja ya msingi wa kuanzisha kwa chama cha walimu ni utetezi, kwahiyo ndiyo maana tunawaasa kutojiingiza katika mambo hayo,” alisema Deus.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles