25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wataalamu watoa tahadhari ya chanjo kwa wajawazito, wagonjwa

Na Faraja Masinde, Dar es Salaam

WATANZANIA wanaendelea kuhimizwa juu ya kuchangamkia kupata chanjo ya kujikinga na virusi vya corona ambayo tayari imeendelea kutolewa kwenye maeneo mbalimbali nchini, hata hivyo kuna makundi ambayo watalaamu wa afya wameshauri yasipatiwe chanjo hiyo kwa sasa. Makundi hayo ni watoto chini ya miaka 18 na mtu anayeumwa.

Wataalamu wa Afya wanaofanyakazi na Ubalozi wa Marekani nchini, kutoka kushoto ni Dk. Eva Matiko ambaye ni Bingwa wa Afya ya Jamii, akifuatiwa na Dk. Arkan Ibwe(katikati) na Dk. Emmanuel Tluway anayefanyakazi na Shirika la misaada la Marekani Usaid.

Ushauri huo umetolewa na wataalamu wa afya wanaofanya kazi na Ubalozi wa Marekani nchini kwenye mkutano wa maswali na majibu kwa waandishi wa habari juu ya chanjo ya corona.

Wameeleza sababu ya kutotolewa chanjo hiyo kwa watoto kuwa ni pamoja na kutohusishwa wakati wa utafiti wa chanjo za corona.

“Tunasema watoto chini ya miaka 18 wasipatiwe chanjoya corona sababu wakati utafiti wa chanjo hizi unafanyika haukuhusisha watoto ndiyo maana haishauriwi sana kwao kupatiwa chanjo hiyo, lakini pia kama mtu anaumwa basi ni busara akasubiri apone ndipo aweze kupata chanjo hii,” ameshauri Dk. Arkan Ibwe, anayetoa huduma za matibabu kwa raia wa Marekani walioko kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, amefafanua zaidi kuwa kuna baadhi ya watu ambao chanjo hizo zimekuwa zikiwaletea changamoto na hivyo hawapaswi kuchanja bila kupata ushauri wa daktari.

“Kuna watu wenye mzio ambao hawa mara nyingine miili yao inakuwa na shida na sampuli zilizotumika kutayarisha chanjo husika, hawa wanashauriwa wasichanje bila kushauriana na daktari ili kuona kama anaweza kupata madhara kulingana na vitu vilivyoko kwenye chanjo hiyo.

“Hivyo ndio maana utasikia mtu amepata madhara haya na yale ni kutokana na tu kwamba mwili wake una mzio (allergy) na alichanja bila kujua iwapo vitu vilivyotumika kweneye chanjo hizo vinamadhara kwake,” amesema Dk. Ibwe.

Kuhusu kundi la wajawazito, Dk. Ibwe amesema kuwa wanapswa kwanza kupata ushauri wa daktari kabla ya kupata chanjo hiyo kwani ni kundi muhimu.

“Hawa ni miongoni mwa watu wa mstari wa mbele kwenye kupata chanjo kutokana na kuwa kwenye hatari kubwa ya kupata kmaambukizi kwa urahisi.

“Hivyo ni seme tu kwamba hakuna kinachomzuia mjamzito kupatiwa chanjo kwa sababu ya mabadiliko ya mwili wake, kwani yuko kweye kundi lenye uwezekano wa kupata corona kali, hivyo anatakiwa kupata kinga, hivyo jambo la muhimu hapa ni yeye kushauriana na daktari wake,” amesema Dk. Ibwe.

Kuhusu upatikanaji wa chanjo, Dk. Eva Matiko ambaye ni bingwa wa afya ya jamii amesema kuwa  chanjo inayostahili ni ile inayopaktikana kwa haraka katika eneo husika ikiwa salama kwa matumizi, ili kuokoa watu na janga husika.

“Kwa kawaida kila Taifa huchagua chanjo au bidhaa kwa kuangalia hali ya hewa ya nchi yake ikiwamo uwezo wa uhifadhi, kutoa na kusambaza.

“Mfano wakati wa janga, Shirika la Afya Duniani (WHO) hutoa idhini ya dharura ya matumizi ya dawa na vifaa tiba, jambo la muhimu huwa ni ubora na usalama,” amesema Dk. Matiko ambaye ana uzoefu wa miaka 20.

Akizungumzia kuhusu chanjo hiyo kupatikana mapema, Dk. Emmanuel Tluway anayefanyakazi na Shirika la misaada la Marekani Usaid, amesema kwa sasa dunia imepiga hatua kubwa kwenye sayansi na teknolojia huku kujitoa kwa matajiri na mataifa makubwa kukichangia uharaka wa upatikanaji.

“Chanjo hii imepatikana mapema kutokana kwanza na kuimarika kwa teknolojia tofauti na miaka ya nyuma, lakini pia ugonjwa wa corona ulionekana haubagui  kwa maana mtu yeyote anaweza kupata awe tajiri au mtu wa kawaida, ndiyo sababu suluhisho la upatikanaji wa chanjo likaungwa mkono kwa haraka na matajiri pamoja na mataifa yenye fedha.

“Hivyo, hakukuwa na uzito kwenye kutoa fedha ilikufanikisha upatikanaji wa chanjo hizi za Covid-19, pia kujitoa kwa watu waliofanyiwa majaribio ya chanjo mbalimbali kulirahisisha sana upatikaji wake kuwa mwepesi,” amesema Dk. Tluway.

Awali, Balozi wa Marekani nchini, Donald Wright, alisema kuwa virusi vya corona vimesababisha vifo vya zaidi ya watu milioni nne duniani kote toka lilipoanza kusambaa kutoka China zaidi ya mwaka mmoja na nusu uliopita.

“Gharama haihesabiki. Leo hii, shukurani kwa jitihada za kishujaa za wanasayansi wanaofanya kazi pamoja duniani kote, tuna nyenzo ya kulitokomeza janga hili. Nyenzo hiyo ni chanjo dhidi ya virusi vya korona. 

“Ikiwa mchangiaji mkubwa zaidi wa chanjo dhidi ya virusi vya korona, Marekani imedhamiria kwa dhati kuongoza mapambano ya dunia dhidi ya janga la UVIKO-19 na kuongeza kasi ya usambazaji wa chanjo duniani,” amesema Balozi Wright.

Balozi huyo amesisitiza kuwa hakuna aliyesalama hadi pale wote tutakapokuwa salam.

“Ni kwa sababu hiyo utawala wa Rais Joe Biden unakusudia kutoa dozi milioni 500 za chanjo kupitia mpango uitwao Gavi kwa ajili ya kusambazwa katika nchi 92 zenye uchumi wa chini na ule wa chini kati kupitia mpango wa COVAX na Umoja wa Afrika, ili kuongezea nguvu mapambano ya kimataifa dhidi ya janga hili. 

“Haya ni manunuzi makubwa zaidi ya chanjo kuwahi kufanywa na nchi moja duniani na hatimaye kutolewa kama msaada. Hiki ni kielelezo cha kujitoa kwa watu wa Marekani katika kusaidia kuwalinda watu duniani kote dhidi ya UVIKO-19. 

Kama sehemu ya jitihada hizo, Julai 24, Marekani ilitoa msaada wa zaidi ya dozi milioni moja za chanjo dhidi ya UVIKO-19 za aina ya Johnson & Johnson kwa Tanzania.

“Msaada huu ulitolewa baada ya kupokea ombi kutoka kwa Serikali ya Tanzania. Aidha, msaada huu ni ishara ya uimara wa ushirikiano wetu wa miaka 60 na Tanzania na dhamira yetu ya dhati ya kusaidia afya ya watu wa Tanzania,” amesema Balozi Wright ambayekitaaluma ni Daktari wa binadamu. 

Aidha, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hasan kwa ujasiri wake wa kuzindua mpan wa utoaji chanjo JUlai 28.

“Ninampongeza Rais Samia kwa uongozi wake katika suala hili na kufanya maamuzi thabiti ya kulinda afya za wananchi. 

“Chanjo zimekuwa sehemu muhimu za nyenzo za kulinda afya ya jamii kwa zaidi ya miaka 200 sasa. Karibu kila nchi duniani hutoa chanjo za mara kwa mara kwa wananchi wake ili kuwakinga na maradhi mbalimbali.

Akitolea mfano nchini Marekani Balozi huyo amesema kuwa asilimia 99 ya vifo vipya vinavyotokana na corona nchini humo ni vya watu ambao hawajachanja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles