Na Clara Matimo, Buchosa
Wataalamu waliopewa dhamana na Serikali ya kuisimamia miradi wametakiwa kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa ikiwemo kushiriki kikamilifu katika vikao vyote vya ujenzi ili kuhakikisha inatekelezwa kwa ubora
Agizo hilo limetolewa Julai 18, 2022 na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, 2022, Sahili Geraruma, wakati akizindua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya Buchosa Mkoani Mwanza ikiwemo ya maji, elimu na afya iliyogharimu Sh milioni 735,754,300.
Amesema mwenge wa uhuru umebaini kwamba wataalamu wengi pamoja na watendaji katika halmashauri nyingi nchini wanashiriki kikamilifu kwenye miradi inayopitiwa na mwenge huo lakini ambayo haipitiwi huwaachia madiwani, walimu na watendaji wa kata wakati hawana utaalamu wa masuala ya ujenzi.
Amesema ameridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo lakini kasoro ndogo alizozibaini ambazo zinarekebishika zisingekuwepo endapo wataalamu wangeshiriki kikamilifu katika ujenzi na kutoa ushauri.
“Niwapongeza kwa usimamizi mzuri wa miradi hii ambayo mwenge wa uhuru umeipitia naomba jitihada ambazo wataalamu wameweka katika miradi yote iliyopitiwa na mwenge waziweke pia kwenye miradi mingine ambayo haipitiwi na mwenge ili iwe na ubora iweze kuwanufaisha wananchi kwa muda mrefu, Tanzania ni yetu inabidi ipendeze,”amesisitiza Geraruma.
Akitoa taarifa ya mradi wa maji uliojengwa katika kijiji cha Magulukenda kabla haujazinduliwa na Geraruma, Kaimu Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Sengerema, Mhandisi Venslaus Blaise amesema hadi umekalimika umegharimu Sh milioni 150 kutoka Serikali kuu.
“Mradi huu ulianza kutekelezwa Mei, 2020 lengo ni kutoa huduma ya maji safi kwa wakazi 5151 katika maeneo ya kijiji hiki cha Magulukenda, kukamilika kwa mradi huu kumeleta manufaa mengi kwa jamii ikiwemo kuimarisha uchumi kwa wananchi kwa kuondo muda wa kutafuta maji.
“Faida zingine ni kuchochea ukuaji wa miji hasa baada ya kuwepo huduma ya maji, kuwepo kwa shughuli za kimaendeleo mfano umwagiliaji wa mashamba, kuchochea na kuimarisha hali ya usalama katika kijiji,”ameeleza Mhandisi Blaise.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Buchosa, Erick Shigongo, ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupeleka fedha katika jimbo hilo kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo ya Afya,maji na miundombinu ya barabara.
“Nimesimama hapa kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Buchosa kukuomba kiongozi utupelekee shukurani zetu wana Buchosa kwa Mheshimiwa Rais Samia kwa fedha alizotuletea na anazoendelea kutuletea wananchi wa Buchosa kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo,” amesema Shigongo.
Awali, akipokea Mwenge wa Uhuru eneo la Iseni Halmashauri ya Buchosa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga, amebainisha kwamba mwenge wa Uhuru utakimbizwa jumla ya kilomita 94.7 ambapo utapitia miradi mitano yenye thamani ya Sh 735,754,300, kati ya hiyo mitatu itazinduliwa, mmoja utawekewa jiwe la msingi na mmoja ni kukabidhi vifaa kwa kikundi cha vijana.