25.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, January 19, 2022

WATAALAMU WAELEZA MBINU KUKUZA KISWAHILI

Na HARRIETH MANDARI-DAR ES SALAAM


KISWAHILI ni lugha ya Taifa la Tanzania. Ni lugha ambayo kadiri miaka inavyozidi kwenda ndivyo inavyozidi kukua na kutumiwa na nchi mbalimbali  duniani.

Tofauti na miaka ya nyuma, lugha pekee iliyokuwa ikipewa kipaumbele ni Kiingereza. Zipo lugha nyingine ambazo zimekua kwa kiasi kikubwa ikiwamo Kichina.

Profesa wa Lugha ya Kiswahili na Fasihi ya Kiafrika katika Idara ya Fasihi Mawasiliano na Uchapishaji ya Taasisi ya Taaluma ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Aldin Mutembei anasema Kiswahili kinaweza kunufaisha nchi yetu kwa njia kuu mbili za uingizaji mapato ya ndani na nje.

“Kiswahili kinaweza kutuingizia pato nchini iwapo Serikali itaweka mfumo wa aina mbili za mapato mojawapo ni kupitia mapato ya ndani. Utaratibu uwepo kwa wageni wanapokuja nchini kwa nia ya kufanya biashara au shughuli nyingine kwa zaidi ya miezi sita basi iwepo kanuni au  sera itakayomlazimu kupitia mafunzo ya Kiswahili kwenye vyuo  au hata vituo binafsi vinavyotoa mafunzo hayo,” anasema Profesa Mutembei.

Anaongeza kuwa njia hiyo imekuwa ikitumiwa na nchi  nyingine duniani kwa nia ya kukuza lugha zao.

Anataja njia nyingine kuwa ni kwa watalii ambao wanakuja kutembelea vivutio nchini kwetu kuwapo na mfumo wa kuwapatia mafunzo ya  lugha ya Kiswahili ili waweze kufurahia zaidi utalii.

Kwa upande wa pato la nje, Profesa Mutembei anasema ni vyema balozi za Tanzania katika nchi mbalimbali kuanzisha vituo vya lugha ya Kiswahili na utamamduni ili kuweza kukitangaza zaidi nchi za nje.

“Iwapo vituo hivyo vitaanzishwa Kiswahili kitakua zaidi, pia nchi itatangaza utalii na tamamduni,” anasema.

Mchambuzi mwingine wa Kiswahili, Profesa  Bashiru Ally anasema lugha hii ni tunu na rasilimali kubwa ya utajiri hata ukilinganisha na nyingine kama viwanda na migodi. Hivyo, hatuna budi kukitumia vizuri.

Anasema wakati umefika Watanzania kuachana na dhana ya kuwa wazito na waoga kwa kukitumia vizuri ili kujiinua kiuchumi, akatolea mfano wa nchi ya Uingereza ambapo ilijikita katika kukuza lugha yake hatimaye walifanikiwa kukua na hata kuanza kutawala nchi nyingi duniani na hivyo kukua kiuchumi.

“Kumbuka Kiingereza ni kama Kisukuma, Kichaga au Kinyakyusa na lugha nyingine nyingi ambacho wenzetu walikitanua na sasa wameendelea kiuchumi, ni Tanzania pekee ambako bado tunasita, hatujiamini ifike wakati tufanye uamuzi kwa kuwa na mifumo mizuri ambayo itawezesha lugha kukua kimataifa,” anasema.

Akatolea mfano wa jinsi gani nchi za nje zinathamini lugha ya Kiswahili kwa kuanzisha vituo vya redio kwa njia ya Kiswahili jambo ambalo ni chachu kwa Tanzania kukikuza zaidi kimataifa.

Anampongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kuanza kuonyesha njia ambapo amekuwa akitoa hotuba zake kwa Kiswahili na kushauri atie mkazo zaidi.

“Rais wetu amejaribu kuonyesha mfano lakini bado haitoshi, atoe tamko rasmi na litatekelezwa kama alivyofanya kwenye kuhamishia makao makuu mjini Dodoma ni jambo linalowezekana kabisa,” anasisitiza Dk. Bashiru.

Mchambuzi wa lugha ya Kiswahili nchini, Majid Mswahili ambaye ni Mchambuzi wa Lugha Fasihi na Falsafa ya Kiswahili, pia Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Kiswahili Development Ltd, anasema Kiswahili kilianzishwa kwa nia nzuri hivyo ni vema kiendelezwe na kupanuliwa zaidi.

“Sasa hivi tunachotakiwa ni kukiendeleza zaidi kwa kufanya tafsiri kwenye lugha zingine, kukalimani, kufundisha wageni wanaokuja nchini na kukifanya kuwa kama bidhaa hasa kupitia balozi zetu zilizoko nchi za nje,” anasema.

Majid anasema sera ya lugha ya Kiswahili ni lazima iundwe badala ya ilivyo sasa ambapo ipo ya utamamduni tu.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), Seleman Sewangi anasema ili lugha ya Kiswahili iweze kuingiza pato kwa serikali ni lazima nayo iunde utaratibu maalumu wa kutafuta wateja kupitia balozi za Tanzania nchi za nje.

Anashauri kuwepo kwa vyuo maalumu vya kufundishia wakalimani ili Tanzania kuwe na wakalimani wa kutosha wa lugha mbalimbali.

Wiki mbili zilizopita, kulifanyika mkutano wa wadau wa sekta ya utamamduni na lugha ya Kiswahili jijini Dar es Salaam,  aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamamduni, Sanaa na Michezo, Nape Mnauye alisema serikali imepanga kuanzisha sera ya lugha  ya Kiswahili ili kusaidia ukuaji wa lugha hiyo ndani na nje ya nchi na hivyo kukikuza zaidi.

Alizitaja baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa zikikwamisha makuzi ya lugha hii kuwa ni ufinyu wa rasilimali na utashi uliopo miongoni mwa watatu.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
175,234FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles