WATAALAMU WA NDEGE WANAOFANYA KAZI ‘NYUMA YA PAZIA’

0
1013

Na Bestina Magutu

UNAPOZUNGUMZIA waongoza ndege yaani “air traffic controllers picha inayokuja haraka miongoni mwa watu wengi, ni ile ya wahudumu wanaotoa ishara za kumsaidia rubani aweze kuegesha ndege vizuri na salama baada ya kutua yaani “marshallers.

Hii ni kwa sababu ndio watu wanaoonekana kirahisi machoni mwa watu walio eneo la uwanja wa ndege.

Hata hivyo, kundi hili la watoa huduma katika sekta ya usafiri wa anga ni tofauti kabisa na lile la waongozaji vyombo vya usafiri angani  yaani Air Traffic Controller ambao jukumu lao ni kuhakikisha usalama  tangu ndege inapopaa hadi inapotua kwenye viwanja vya ndege vilivyokusudiwa.

 Muongoza ndege ni nani?

Kama ilivyodokezwa hapo juu, muongozaji ndege ni mtaalamu mwenye jukumu kubwa la kuhakikisha usalama wa ndege tangu inapotaka kuanza safari, inapopaa angani, inapokuwa angani hadi pale inapotua kwenye kiwanja kilichokusudiwa.

Wataalamu hawa ambao si rahisi kuwaona ufikapo uwanjani, wanafanya kazi katika ofisi maalumu zenye vifaa vinavyowawezesha kufanya  mawasiliano na marubani wakati wote wa safari za ndege, zinapokuwa angani na katika viwanja vya ndege.

Mwongoza ndege, hushirikiana kwa karibu na rubani wa ndege kupitia mawasiliano ya redio ili kuhakikisha safari ya ndege zinafanyika kwa  ufanisi na usalama wa hali ya juu na kwa muda uliopangwa.

Rubani wakati wote awapo angani, anapokea maelekezo ya safari kutoka kwa muongoza ndege aliye katika himaya ya anga husika kwa kumpa taarifa mbalilmbali ambazo rubani huzihitaji ili kufanikisha safari yake kwa usalama.

Kuna vyombo vingi vinavyosafiri angani kwa nyakati tofauti, hivyo basi ni jukumu la mwongoza ndege kuhakikisha ndege iliyo kwenye himaya yake inapaa na kutua salama katika mpangilio unaofaa. Mwongoza ndege anawajibu wa kuhakikisha ndege  anayoiongoza  inakaa angani, inapanda juu, kushuka chini na hata kupishana na ndege nyingine bila kuwapo hatari ya kugongana.

Wataalamu hawa wafanyao kazi ‘nyuma ya pazia,’ yaani bila kuonekana kirahisi machoni mwa wengi wapitao viwanja vya ndege wana jukumu kubwa na zito  kuhakikisha  usalama wa maisha ya abiria, wafanyakazi wa ndege, mizigo  na chombo chenyewe  wakati wote.

Waongozaji ndege hawa hutoa huduma zao katika ofisi zao maalumu, kama vile kwenye minara ya kuongozea ndege ‘control towers’ na ofisi zingine maalumu zilizojengwa kulingana na mahitaji ya ndege zitumiazo viwanja hivyo na anga husika.

Kazi za mwogoza ndege katika kukamilisha majukumu yake ni kutoa idhini na maelekezo kwa rubani wakati anapotaka kuanza safari na pale anapotaka kutua, afikapo kwenye kiwanja cha ndege husika.

Pili, kutoa idhini na maelekezo kwa rubani awapo angani endapo anataka kupanda juu au kushuka chini kulingana na matakwa ya ndege ili kufikia usawa wa mruko anaohitaji katika safari yake.

Tatu, kufuatilia mwenendo wa ndege ili kuhakikisha usalama na kuepusha migongano (collision) na kitu chochote au viashiria vya ajali (incident) iwapo angani na ardhini katika  uwanja wa ndege.

Nne, kufanya mwasiliano na vituo vingine vya kuongozea ndege ndani au nje ya nchi ili kutoa au kupokea taarifa mbali mbali za ndege zitokazo, ziingiazo au zipitazo katika anga hilo.

Tano, kutoa taarifa  muhimu kwa rubani awapo safarini kama vile  hali za viwanja, eneo  la mruko, pamoja na zile za hali ya hewa ili kufanikisha safari hiyo.

Saba, kutoa taarifa kwa maofisa au taasisi mbalimbali na wahusika wakuu wa mambo ya anga kuhusiana na ndege yenye dharura yoyote ili kufanikisha kazi ya  uokoaji wa haraka wa watu na mali zao na chombo husika.

 Makundi yauongozaji

Kazi za uongozaji ndege zimegawanyika katika makundi makuu matatu.

Mosi, ni waongozaji ndege wanaofanya kazi katika minara ya kuongozea ndege (Tower controllers), pili ni waongozaji ndege wa anga la kati kwa ndege zinazopanda na kushuka uwanjani (Approach Controllers) na tatu ni waongozaji wa Anga la juu na masafa marefu (Area Controllers)

‘Tower Controllers’

Wataalamu hawa hutoa huduma za kuongoza ndege katika minara maalumu iliyojengwa katika viwanja vya ndege.

Hapa nchini kuna vituo 14 vilivyopo, Arusha, Dar es Salaam (JNIA), Dodoma, Iringa, Kilimanjaro (KIA) na  Kigoma.

Vingine ni Mwanza, Mtwara, Pemba, Ruvuma, Songwe,Tabora,Tanga na Zanzibar (AAKIA). Wataalamu hawa huongoza ndege kwa kuziona kwa macho katika eneo la maili kumi na tano liitwalo “Aerodrome Traffic Zone” kati ya usawa wa mruko wa futi 2,500 kwa kutoa idhini na maelekezo kwa ndege zinazotarajia kuanza kupaa au safari kutoka uwanja wa ndege  na zile zinazotua na kuelekea kwenye maegesho ya ndege uwanjani.

Pia wataalamu hawa wanajukumu la kuhakikisha mpangilio mzuri na wa haraka wa ndege zinazoondoka na zile zinazotua ili kupunguza ucheleshwaji wa ndege pale zinapotaka kupaa au kutua.

 ‘Approach Controllers’

Kundi hili la waongozaji ndege, lina wajibu wa kuzitenganisha (separation) ndege zinazopanda na zinashoshuka au kupita katika anga lake (departing, approaching and transit air traffic) la kati takribani maili 100  na futi za usawa wa bahari  24,000 katika viwanja vya ndege. Kazi hii hufanywa kwa umakini mkubwa na haraka ili kuhakikisha ndege zinapaa na kutua kwa usalama katika muda uliopangwa bila kuwepo na mgongano au viashiria vya ajali.

Ili kufanikisha hilo,  ana wajibu wa kuhakikisha ndege zinaruka na kutenganishwa katika umbali  unaokubalika baina ya ndege moja hadi nyingine ziwapo angani kwa kuzingatia kanuni na viwango vilivyowekwa na Shirika la Kimataifa la Usafiri Duniani (ICAO). Hapa nchini kuna vituo vikuu vinne ambavyo ni Dar es Salaam (JNIA), Zanzibar (AAKIA), Kilimanjaro (KIA) na Mwanza.

 ‘Area Controllers’

Wataalamu wa kundi hili, wanao wajibu mkubwa wa kuongoza ndege katika anga la juu takribani futi 24,000 kwenda juu zaidi, pia kwa ndege ziendazo masafa zaidi ya maili 100 hadi kwenye mipaka ya nchi yetu kwa ndege zote zinazoondoka, zinazowasili na zile zinazopita kwenye anga letu bila kutua kueleke nchi jirani.

Kama ilivyo kwa waongozaji ndege wa kundi la pili yaani ‘Approach controllers,’ waongozaji ndege wa anga la juu na masafa marefu ‘Area Controllers’  wanatekeleza majukumu yao kwa umakini ili kuhakikisha ndege zinaruka salama na umbali unaokubalika kati yao kulingana na vigezo vilivyowekwa na ICAO. Hapa nchini kituo kinachotoa huduma hiyo ni cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kilichopo Dar es Salaam katika ofisi ya Area Control Center (ACC).

Kituo hiki pia kina ofisi nyingine (Rescue Coordination Centre) ambayo hutumika kutoa huduma za msaada wa mawasiliano yote kwa ndege ipatayo dharura ili kuratibu na kufanikisha zoezi la utafutaji na uokoaji wa watu na mali zao pale huduma hiyo itakapohitajika.

Mafunzo

Waongoza ndege hufanya kazi kwa weledi mkubwa, baada ya kupata mafunzo maalumu kutoka vyuo vinavyotambulika kimataifa katika taaluma hiyo, Aviation Training Centers. Hapa nchini chuo cha Civil Aviation Training Center (CATC), kinachomilikiwa na TCAA, kinatoa mafunzo hayo  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wa Zamani (JNIA Terminal I),  Dar es Salaam.

 Vifaa

Vifaa mbalimbali vya tehama hutumika hutumika  kutekeleza jukumu la uongozaji ndege katika sekta kuu tatu nazo ni, mfumo wa mawasiliano (Communication System),ikiwa ni pamoja na redio, simu, mikrofoni, mfumo wa uendeshaji ndege (Air Navigation System), mfano vifaa vya kupima muelekeo na umbali (VOR, DME) na ufuatiliaji wa ndege au vyombo angani (Surveillance System) , ikihusisha mitambo ya rada na ile ya A-DSB.

Mwandishi wa makala haya, Bestina Magutu, ni Ofisa Habari Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here