24.8 C
Dar es Salaam
Saturday, May 28, 2022

WAT-Human Settlements Trust faraja kwa watu kipato cha chini

housesNa FARAJA MASINDE

KILA siku gharama za ujenzi zinazidi kuongezeka licha ya serikali kujitahidi kuweka mazingira rafiki kwenye sekta ya ujenzi.

Ingawa kumekuwa na ongezeko kubwa la mashirika yanayojihusisha na ujenzi wa makazi ya binadamu huku pia yakiwa na nia moja ya kujenga makazi bora na kutoa huduma ya viwanja kwaajili ya Watanzania lakini bado siyo suluhisho kwa wale wenye vipato vya chini na vya kati.

Hivi basi licha ya mashirika hayo kutayarisha nyumba na viwanja kwaajili ya kukopesha Watanzania kwa lengo la kuwaepusha na adha za ujenzi sanjari na gharama kubwa za kupanga, bado wale wenye kipato cha chini hawawezi kumudu nyumba hizo.

Hii inatokana na kuwa na masharti magumu ikiwamo kiwango cha juu cha tozo na mlolongo mrefu wa mikopo ambao umekuwa ukiwekwa na taasisi nyingi za fedha ambazo nyingi zimeshikamana na mashirika ya ujenzi wa nyumba kwaajili ya kuwasaidia Watanzania.

Hali hiyo kwa namna moja imefanya kuendelea kuwapo kwa matabaka kati ya wenye kipato cha juu ambao wamekuwa wakipewa kipaumbele zaidi cha kumiliki nyumba ikilinganishwa na wasio na kipato rasmi wakiwamo wajasiriamali na hivyo kuwafanya wengi kusalia kuwa wapangaji kwenye nyumba za wale wenye vipato vya juu.

Ili kuhakikisha kuwa fursa inakuwepo kwa kila Mtanzania mwenye akili timamu na mwenye chanzo halali cha kipato anamiliki kiwanja au nyumba yake kwa masharti nafuu na yaliyo rafiki, Shirika lisilokuwa la kiserikali la WAT-Human Settlements Trust (WAT-HST) limeamua kuwa kiungo katika kuwasaidia Watanzania wenye vipato vya kawaida kuhakikisha kuwa wanamiliki makazi bora kupitia vipato vyao.

WAT –HST lilianzishwa Oktoba 1989 likifahamika kama Women Advancement Trust (WAT) kabla yakubadilishwa mwaka 2005 na kuwa WAT- Human Settlements Trust (WAT-HST) lengo likiwa ni kuendana na shughuli zake kihalisia.

Kwa mujibu wa Mkurungenzi Mtendaji Mkuu wa WAT-HST, Bi Judith Sando, lengo la kufanyika kwa mabadiliko hayo ilikuwa ni katika kuhakikisha kuwa kila mtu hasa wanawake wanapata fursa ya kuingia kwenye shirika hilo.

“Kwakutambua kuwa kuna watu wa kipato cha chini na cha kati wakiwamo madereva, waendesha bodaboda, walimu, wanawake wajasiriamali, watumishi wa kada mbalimbali wa Serikali na wengine mbao wako mjini na wanahitaji makazi bora ya kuishi, shirika linawahudumia kwani ndio dhamira na mtazamo wa Shirika kuhakikisha kuwa inawasaidia wale wote waliosahauliwa na mfumo rasmi’’

“Hivyo kwa kuwa na uhakika wa kipato unakuwa na uwezo wa kumiliki nyumba yako au kiwanja kutoka WAT-HST tukiwa na maana kuwa badala ya kumlipa kodi mwenye nyumba utakuwa unalipa kodi hiyo kama sehemu ya marejesho ya mkopo wako wa nyumba au kiwanja.

“Kwani tayari nyumba na viwanja vipo ambapo mtu wa kipato cha chini anaweza kumudu huku viwanja vikiwa vimepimwa sanjari na kuwa na huduma zote muhimu,”anasema Judith.

Kuhusu marejesho ya mikopo ya viwanja, Judith, anasema kuwa mteja anapewa muda wa kulipia mkopo wake mpaka miezi 24 huku ile ya nyumba ikiwa miezi 60 jambo ambalo ni nadra kulikuta kwenye mashirika mengine yanayotoa mikopo ya nyumba na viwanja.

Kwanini ukope WAT-HST

Judith, anasema kuwa faida ya kukopa kutoka kwao kutokana na mikopo kupatikana kwa urahisi na ndani ya muda mfupi, huku ikiwa ni mikopo ya kipekee ya viwanja, uboreshaji na ujenzi wa nyumba inayotolewa kwa watu wenye kipato cha chini na cha kati.

“Mikopo yetu ni ya riba nafuu, hivyo itakupa fursa ya kufaidika na huduma za kiufundi na ushauri pia inakinga ya bima hivyo mkopaji akifariki familia yake haitawajibika kulipa mkopo’’

“Jambo jingine tunalojivunia ni kuwa tunamjali mteja kwa kumpa elimu na kumfanyia tathimini ya kipato chake ili kumjengea uwezo wa kurejesha mkopo bila tatizo kulingana na kipato chake,”anasema Judith.

Anasema hii ni fursa ya kipekee kwa watu wote kuhakikisha kuwa wanaitumia kujikwamua, kupata makazi bora kwani nyumba zipo za kutosha sanjari na viwanja kwenye miradi yao iliyoko kwenye maeneo mbalimbali.

“Miradi yetu imesambaa kwa kiasi kikubwa ambapo ipo kwenye maeneo ya Kigamboni, Mabwepande na Mbezi ambako huko ni kwaajili ya miradi ya nyumba, huku miradi ya Kiluvya na Kerege ikiwa ni kwa ajili ya viwanja ambavyo ukubwa wake unaanzia mita za mraba 350 mpaka 800.

“Chakufurahisha zaidi ni kuwa maeneo yote ya mradi yanafikika kirahisi. Lakini pia tunasaidia katika kurasimisha makazi yasiyopimwa, uhamasishaji wa jamii na mafunzo kuhusu nyumba na masuala muhimu ya kijamii,” anasema Judith.

Anasema jukumu jingine la WAT-HST ni juu ya uboreshaji wa nyumba na makazi ikiwamo kuunganisha huduma zote muhimu za kijamii na uwezeshaji wa fursa ya kumiliki ardhi salama pamoja na ujenzi wa nyumba mpya kwa awamu.

 

Taratibu za kupata mkopo wa nyumba

Bi. Judith, anabainisha kuwa jambo la kwanza kwa mtu anayehitaji kumiliki kiwanja au nyumba za WAT-HST ni lazima asajiliwe kama mteja au hata kuwa kwenye kikundi kisichopungua watu watano na umri usiopungua miaka 18.

“Ni lazima awe ni mtu mwenye akili timamu, awe na chanzo halali cha kipato, na awe raia wa Tanzania bila kusahau kuhudhuria mafunzo ya awali juu ya huduma zetu yanayoratibiwa na WAT-HST,” anasema Judith.

Anaendelea kubainisha kuwa ili mtu aweze kusajiliwa na WAT-HST ni lazima awe na barua ya utambulisho kutoka serikali ya mtaa, picha mbili ndogo pamoja na nakala ya kitambulisho chake

“Kuna njia rahisi za kufanya malipo ya awali na marejesho ambapo mteja anawajibika kurejesha deni lake kila mwezi, ambapo anaweza kufanya hivyo kupitia benki au mtandao wa simu.” anasema.

Anafafanua kuwa mkakati wa WAT-HST ni kuhakikisha kuwa wanakamilisha ujenzi wa nyumba 300 kila mwaka kwa kipindi hiki cha miaka minne mpaka 2020.

“Tunamkakati wa kuhakikisha kuwa tunasambaa ili kuwafikia Watanzania wengi kwani tunaamini kuwa wapo wengi ambao wanahitaji kumiliki makazi yao hasa wanawake ambao wamekuwa wakikosa haki.

“Huu ni wakati muafaka kwa makundi yaliyosahaulika ikiwamo wanawake kumiliki makazi bora na tunashukuru kuona kuwa Watanzania wengi tunawahudumia kutokana na kutoa nyumba za gharama nafuu,”anasema Judith.

Watanzania wengi ambao walikuwa na vipato vya kati na vidogo walionufaika na mpango huo wa mikopo ya kumiliki makazi kwa gharama nafuu na hivi ndivyo wasemavyo.

“Ki ukweli ilikuwa ni ndoto yangu ya muda mrefu kumiliki nyumba lakini nilikuwa sijui nitafanikisha vipi ukilinganisha kuwa mimi ni mjasiriamali mdogo na mashirika mengi yanayojenga nyumba yamekuwa yakitoza kiwango kikubwa.’’

“Ndipo nikaarifiwa juu ya uwepo wa WAT-HST na kuwa wanakopesha viwanja na nyumba kwa bei nafuu kulingana na vipato halisi vya Watanzania, kiukweli imekuwa ni faraja kubwa sana kwangu kwani leo niko kwangu na najivunia kwa hili, kwani badala ya mtu kuendelea kumlipa mwenye nyumba unakuwa unatumia kiasi hicho kurejesha mkopo wako ukiwa kwako.’’

“Napenda kuwashauri Watanzania wenzangu ambao wanajua kuwa hawawezi kumudu kuchukua mikopo ya nyumba kwenye mashirika yanayotoza riba kubwa waje wajiunge na WAT-HST, Kwani wanataratibu ambazo yeyote anaweza kuzimudu.”

WAT–Human Settlements Trust wanapatikana Kinondoni B, barabara ya Kawawa, kitalu namba 37 ambapo pia unaweza kuwasiliana nao kwa barua pepe ambayo ni, [email protected]  au hata kutembelea kwenye tovuti yao ambayo ni www.wat.or.tz .

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,577FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles