Na SHOMARI BINDA
MBUNGE wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, amewataka wananchi wa jimbo lake kuhakikisha wanawasomesha watoto wasiweze kuteteleka katika maisha yao.
Kauli hiyo aliitoa ikiwa ni mara ya kwanza kuzungumza na wananchi wa jimbo lake ikiwa ni miezi minne tangu alipojiuzulu uwaziri wa Nishati na Madini kwa kushindwa kusimamia suala la mchanga wa dhahabu unaosafirishwa nje kwenye makontena.
Alikuwa akizungumza baada ya kufunguliwa nyumba za watumishi wa afya, tanuru la kuchomea taka na vyoo kwa ajili ya wagonjwa kwenye Kituo cha Afya Murangi.
Mradi huo umefadhiliwa na ubalozi wa Japan.
Prof. Muhongo alisema elimu ndiyo mkombozi jamii kwa sababu pia wanaweza kupatikana wataalamu wa afya.
Alisema wananchi wanapaswa kuzingatia elimu kwa watoto kuweza kuwapata wataalamu wa kada mbalimbali hasa wanasayansi ambao ni vigumu kuteteleka kutokana na taaluma zao.
“Mtu aliyesoma hawezi kuteteleka hata ije dhoruba ya aina gani…nawaomba wananchi mlitilie mkazo suala la elimu tuweze kuwapata wataalamu wengi ambao katika siku za usoni waweze kutoa huduma kwenye vituo vyetu na kuyatumia majengo haya,”alisema.
Prof. Muhongo aliwataka wananchi kuacha kuitegemea serikali na wafadhili katika kufanikisha mambo yao ikiwamo ujenzi wa majengo ya zahanati na nyumba za wauguzi.
Aliwashauri wajitoe katika kuchangia wenyewe kabla ya kuletewa misaada.
Alisema wananchi wanapaswa kujitoa na kuchangia kwa mali na nguvu zao katika ujenzi wa miradi mbambali yakiwamo majengo ya madarasa na maabara kuweza kuzalisha wasomi wengi watakaoweza kusaidia taifa na jamii kwa ujumla.
Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida, alimshukuru Profesa Muhongo kwa kupendekeza mradi huo na kusaidia wakati wa utekelezaji wa mradi huo ambao umekamilika kwa viwango.
Alisema ubalozi wa Japan ulitoa Sh milioni 150 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya wafanyakazi, choo cha wagonjwa, tanuru la kuchomea taka hospitalini ambavyo vyote vimekamilika kwa viwango.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Musoma, Flora Yongolo, alisema mradi huo umetekelezwa kwa ubora wa viwango vya serikali ya Tanzania.
Alisema mradi umelenga kupunguza adha ya makazi kwa watumishi wa Kituo cha Afya Murangi na uboreshaji utoaji na upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.