Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
MAHAKAMA ya Rufaa imebatilisha uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza ya kutupilia mbali kesi ya kupinga matokeo ya ubunge Bunda Mjini iliyofunguliwa na wapiga kura dhidi ya mshindi wa kiti hicho, Esther Bulaya (Chadema).
Akisoma uamuzi huo Dar es Salaam jana, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Jaji Elizabeth Mkwizu, alisema mahakama hiyo imepitia hoja zilizowasilishwa na upande wa walalamikaji na kujiridhisha na maombi yao.
Alisema baada ya kupitia kifungu hadi kifungu, imejiridhisha kuwa hoja zilizowasilishwa na upande wa walalamikaji ni za msingi kwa kuwa sheria inawapa haki wafuasi hao kufungua kesi ya kuhoji na kupinga matokeo hayo.
Kutokana na sababu hizo mahakama imeelekeza kuwa kesi hiyo irudi katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza   ianze kusikilizwa upya na jaji mwingine tofauti na aliyeisikiliza awali.
Awali, wapiga kura hao, Â Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Escietik Malagila walifungua kesi ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi Bulaya katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Wafuasi hao ambao wanawakilishwa na Wakili Yasin Memba walitaka uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza utamkwe kwamba ni batili kwa mujibu wa sheria.
Walalamikiwa katika kesi hiyo ni   Msimamizi wa uchaguzi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na mbunge wa jimbo hilo.
Katika kesi hiyo, Jaji Mohamed Gwae wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza alitupilia mbali kesi hiyo kwa madai kuwa wafuasi hao hawakuwa na haki ya heria kufungua kesi hiyo.
Walalamikaji hao walikata rufaa Mahakama ya Rufani  kupinga uamuzi huo.