WAPIGAKURA wanne wa Jimbo la Bunda Mjini mkoani Mara, wamekamilisha taratibu za kimahakama na kuwasilisha upya maombi ya kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania kutokana na maombi yao ya awali kutupiliwa mbali Februari 24, mwaka huu.
Maombi hayo yamewasilishwa na wapigakura Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Ascetic Malagila dhidi ya Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya, kuiomba mahakama hiyo kuwapa kibali cha kukata rufaa katika mahakama hiyo.
Wapigakura hao ambao wamekuwa wakimpigania aliyekuwa Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika na mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Bunda Mjini, Stephen Wasira, waliwasilisha maombi ya kufungua shauri katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ili itoe ufafanuzi kuhusu haki ya mpigakura ya kuhoji matokeo pamoja na vigezo vinavyotakiwa ili aweze kuhoji matokeo ya uchaguzi.
Maombi yao ya awali yalitupiliwa mbali na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Sirilius Matupa kutokana na kuwasilishwa sura 141 ya sheria ya rufaa na kueleza kuwa yalikuwa yamewasilishwa chini ya kifungu cha 15 (a) (b) badala ya kifungu 15 (c) ambacho ndiyo sahihi kwa ajili ya maombi hayo na kuwaeleza wanaweza kurekebisha na kuyawasilisha upya.
Januari 25, mwaka huu Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Mohamed Gwae, aliitupilia mbali kesi namba moja ya kupinga matokeo ya Uchaguzi Jimbo la Bunda Mjini iliyofunguliwa na wapigakura hao dhidi ya Bulaya.
Wakati huo huo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Sumbawanga, Kakusulo Sambo anayesikiliza kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi Jimbo la Nyamagana, amekutana na mawakili wa pande zote na kuweka mikakati ya namna ya kuiendesha.
Jaji Sambo amekutana jana na mleta maombi (Ezekiel Wenje), mjibu maombi wa kwanza (Stanslaus Mabula) pamoja na mawakili wanaowawakilisha kuweka mikakati ya uendeshwaji wa kesi hiyo ikiwa ni pamoja na kubainisha sehemu zinazobishaniwa.
Akizungumzia hatua hiyo, Wakili Deya Outa anayemwakilisha Wenje, alisema katika kikao hicho wamebainisha sehemu zinazobishaniwa na pande zote katika kesi hiyo pamoja na mashahidi watakaotakiwa kufika mahakamani kutoa ushahidi.