23.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

WASIPOSHTUKA SINGELI WATAJIUA WENYEWE

Na RAMADHANI MASENGA

BADO unasikia watu wakitaka kushindanisha muziki wa Singeli na Bongo Fleva? Bado unahisi Singeli una msisimko kwa watu wa kariba zote kama ilivyotaka kutokea miezi michache iliyopita?

Muziki wa Singeli umedumaa. Wasanii wake wameshindwa kuwaza kiubunifu na matokeo yake bado wanaufanya kuwa muziki wa tabaka lilelile. Tabaka la wahuni na masela wa kitaa.

Ili muziki uweze kuwa na mafanikio makubwa ni lazima uwe na taswira njema kwa jamii. Unaiona Bongo Fleva ya leo? Miaka karibu ishirini iliyopita ulikuwa muziki wa watu fulani.

Wahuni fulani na masela fulani. Ulikuwa na mafanikio? Hapana. Japo ulishabikiwa na vijana kwa nguvu ila haukuwa na mafanikio. Kina Sugu, Juma Nature na wenzao walikuwa na majina makubwa ila yasiyo na heshima wala mafanikio ya maana.

Baada ya miaka kadhaa, wakabadili namna ya kuandika mashairi yao. Sasa watu wakaanza kuvutiwa. Ukatoka kuwa muziki wa masela na vijana  wa vijiweni, mpaka kuingia katika majumba ya kishua na vyuoni.

Sasa hata wasomi wakaanza kuona Bongo Fleva ni muziki wa maana. Wale wazazi waliokuwa wakidhani muziki huu ni uhuni wakatoa mawazo yao na kusapoti vijana wao kujiingiza katika muziki huo.

Sasa haishangazi kuona msanii wa muziki huu akiitwa Ikulu na mkuu wa nchi. Tumeshuhudia wanamuziki wa muziki huu wakiwa wabunge na mabozi wa taasisi na kampuni kadhaa.

Kuna sehemu muziki wa Singeli upo. Wanamuziki na wadau wake wakiacha kuwa makini muziki huu utakufa ungali bado mchanga. Mpaka sasa muziki wa Singeli upo kiburudani na mambo mengine ya hovyo.

Angalia wanamuziki wakali wa Singeli na nyimbo zao. Yupo Man Fongo. Wimbo wake uliotamba sana ni Hainaga Ushemeji.

Ni wimbo mzuri kuusikiliza lakini hauna maadili. Kuna Sholo Mwamba. Naye yuko katika mfumo huohuo. Na sasa Msaga Sumu katoa wimbo mwingine ‘Mwanaume Mashine’.

Ukisikiliza huo wimbo toka mwanzo mpaka mwisho ni lazima ugeuke nyuma kuangalia unasikiliza na wangapi. Siyo wimbo wa kusikiliza na wazazi au yeyote unayemuheshimu. Lakini wadau wake wanasema ni mzuri.

Hatari ya mambo kama haya ni kudumaza muziki wenyewe.  Kama muziki huwezi kudhaniwa kusikilizwa na jamii staarabu, unategemea vipi wazazi kuwaruhusu vijana wao kuushiriki muziki huo?

Katika hali kama hiyo, unategemea vipi wadau makini, zikiwemo kampuni kuendelea kuweka hela katika muziki huo?

Kama kuna ndoto ya kubadilisha muziki huo na kuwa wa  kibiashara zaidi, wadau hawana budi kubadlika. Badala ya kuimba ilimradi tu watu wacheze bila kujali aina ya maneno ama maudhui ya wimbo husika, sasa ni zamu ya watu kuanza kufikiri kwa kina na kutoa nyimbo makini za kufaa watu kusikiliza na kujifunza kitu.

Bongo Fleva leo inatamba kimataifa kwa sababu ndani ya nchi huu muziki una heshima yake. Kina Proffesa Jay, Sugu na Ferooz wameimba nyimbo za kuelimisha na kuburudisha jamii.

Leo hata waziri akisikia mwanaye anataka kujiingiza katika muziki wa Bongo Fleva hawezi kushtuka.  Atashutuka vipi wakati ndani kuna kina Ferooz, Afande Sele, Maalim Nash na Diamond?

Ndani kuna waelimishaji na wafanyabiashara wakubwa. Katika Singeli kuna nini? Bado kuna Mwanaume Mashine, Mwaga Maji Tucheze Kama Kambale na Hakunaga Ushemeji. Aibu hii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles