Na SHOMARI BINDA
MKUU wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, amewaonya watu ambao wamekuwa wakikwepa kujiandikisha vitambulisho vya taifa kuwa baada ya hatua hiyo kukamilika ataagiza polisi kuwasaka waliopuuzia.
Alisema watu hao watatakiwa waeleze sababu za kutojisajili na kupata vitambulisho.
RC alikuwa akizungumza juzi baada ya kumalizika siku 90 za usajili na uandikishaji wa vitambulisho vya taifa kwa Mkoa wa Mara.
Alisema hatua hiyo imekamilika kwa kusajili wananchi 718,647 kati ya 763,142 waliostahili kusajiliwa hivyo kufanya idadi ya wananchi waliodahiliwa kufikia asilimia 94.
Alisema katika hatua hiyo pia wamesajili wageni wakazi 224 ambao wamekuwa wakiishi halali mkoani humo.
Rc aliwaonya ambao hawakujiandikisha kutumia siku za marekebisho kujisajili na kujiandikisha.
“Wale waliojiandikisha baada ya hatua hiyo kumalizika watapata vitambulisho vyao na wasiokuwa navyo tutawahesabu kuwa siyo wenzetu.
“Zipo wilaya ambazo zimefanya vizuri katika hatua hii ni Musoma na Bunda ambazo zimesajili kwa asilimia 112 zinastahili kupongezwa,” alisema.
Hata hivyo alisema licha ya kukamilika hatua hiyo itaendelea katika ofisi za wilaya hivyo kuwaomba wale ambao hawakupata fursa hiyo wafike kukamilisha kuanzia Mei hadi Juni 2018.