WASIOKUWA NA MIKATABA WAZUIWA KUNUNUA PAMBA

0
501

Na Raphael Okello-BundaMKUU wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Lydia Bupilipili, amezitaka  kampuni ambazo hazikuingia  mkataba  na wakulima wa pamba  wa wilaya  hiyo  kutonunua  zao hilo  katika msimu  wa ununuzi unaotarajiwa kufunguliwa rasmi  Juni 5, mwaka huu.


Akizungumza na waandishi  wa habari  ofisini  kwake jana, Bupilipili alisema  kampuni  zenye  mkataba  na wakulima  wilayani Bunda ni OLAM  Company Ltd na S & C  Company Ltd  na ndizo pekee zitakazonunua pamba  kwa wakulima, huku akiagiza kuwa mwisho  wa kusafirisha  zao hilo ni saa 12 jioni.


 “Nitoe angalizo  kwa kampuni ambazo  hazina  mkataba  hapa  wilayani kuacha mara moja  mchakato  wa  kutaka  kununua pamba kutoka Bunda, Serikali  haitawavumilia  itachukua hatua mara moja dhidi yao, kwa sababu  huwezi kuvuna  usipopanda,” alisema Bupilipili.


Alisema  bei elekezi ya Serikali  ya kununulia ni kuanzia Sh 1,100  kwa kilo moja ya pamba, hivyo amemtaka  kila mkulima  kuelekeza  mazao yake  kwa kampuni aliyoingia nayo mkataba  wa pembejeo na si vinginevyo.


Bupilipili aliwatahadharisha  wakulima  na  mawakala  wa kampuni kutojihusisha na  udanganyifu wowote  wakati  wa ununuzi, ikiwa ni pamoja na kuchakachua mizani, kuongeza  maji, michanga au taka  katika pamba kwa lengo la kuongeza uzito kwamba hatua zitachukuliwa dhidi yao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here