Na Raphael Okello-Bunda
MKUU wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Lydia Bupilipili, amezitaka kampuni ambazo hazikuingia mkataba na wakulima wa pamba wa wilaya hiyo kutonunua zao hilo katika msimu wa ununuzi unaotarajiwa kufunguliwa rasmi Juni 5, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Bupilipili alisema kampuni zenye mkataba na wakulima wilayani Bunda ni OLAM Company Ltd na S & C Company Ltd na ndizo pekee zitakazonunua pamba kwa wakulima, huku akiagiza kuwa mwisho wa kusafirisha zao hilo ni saa 12 jioni.
“Nitoe angalizo kwa kampuni ambazo hazina mkataba hapa wilayani kuacha mara moja mchakato wa kutaka kununua pamba kutoka Bunda, Serikali haitawavumilia itachukua hatua mara moja dhidi yao, kwa sababu huwezi kuvuna usipopanda,” alisema Bupilipili.
Alisema bei elekezi ya Serikali ya kununulia ni kuanzia Sh 1,100 kwa kilo moja ya pamba, hivyo amemtaka kila mkulima kuelekeza mazao yake kwa kampuni aliyoingia nayo mkataba wa pembejeo na si vinginevyo.
Bupilipili aliwatahadharisha wakulima na mawakala wa kampuni kutojihusisha na udanganyifu wowote wakati wa ununuzi, ikiwa ni pamoja na kuchakachua mizani, kuongeza maji, michanga au taka katika pamba kwa lengo la kuongeza uzito kwamba hatua zitachukuliwa dhidi yao.