25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wasindikizaji/wasambazaji maziwa mbadala na vyakula vya watoto zingatieni sheria

Na Catherine Sungura, Ikungi

Sekta binafsi, wasindikaji, wasambazaji na wauzaji wa maziwa mbadala na vyakula vya watoto wameagizwa kuepuka matangazo ya bidhaa zao ili kuzingatia sheria na kanuni ya kudhibiti uuzaji na usambazaji wa maziwa na vyakula vya watoto wachanga na wadogo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Khamis wakati akiongea na wananchi wa Halmashauri ya Ikungi, Mkoani Singida katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama kwa watoto duniani.

“Mnapaswa kuzingatia Sheria na Kanuni ya Kudhibiti Uuzaji na Usambazaji wa Maziwa na Vyakula vya Watoto wachanga na wadogo kwa kuepuka utoaji wa matangazo, ushawishi na kufanya promosheni ya maziwa mbadala na vyakula vya watoto wachanga kwenye vyombo vya habari au katika maeneo yoyote,” amesema Mwanaidi.

Aidha, alisema Viongozi wa kijamii wakiwemo Viongozi wa Dini na Siasa, watu maarufu wenye ushawishi katika jamii, wasanii na wanamichezo wana wajibu wa kuhamasisha jamii kuhusu unyonyeshaji wa maziwa ya mama.

Naibu Waziri huyo amewataka wasambazaji na wasindikizaji wa maziwa mbadala na vyakula vya watoto kutafuta na kusambaza taarifa sahihi zinazohusu unyonyeshaji na lishe na kuepukua kusambaza taarifa au imani potofu zinazoathiri unyonyeshaji.

Hata hivyo ametoa rai kwa sekta ya viwango na udhibiti ubora wa vyakula, wanataaluma na taasisi zinazosimamia sheria zinazohusu vyakula vya watoto kuendelea kufanya tafiti na ufuatiliaji wa kina wa taratibu za uuzaji na usambazaji wa maziwa na vyakula vya watoto wachanga na wadogo ili kusaidia kuwalinda watoto hao dhidi ya athari wanazoweza kuzipata kutokana na kutumia bidhaa zisizokuwa na ubora na pia kulinda na kuendeleza unyonyeshaji watoto maziwa ya mama.

“Ujumbe wa wiki ya unyonyeshaji mwaka huu inayosema “Chukua hatua endeleza unyonyeshaji, Elimisha na toa msaada” unatukumbusha sote tuna wajibu wa kuwawezesha wanawake waweze kunyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo baada ya kujifungua,” amesema.

Wakati huohuo Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida ambaye ni Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk. Victoriana Ludovick amesema asilimia 93.4 ya akina mama na walezi katika Mkoa huo wamepatiwa elimu ya unyonyeshaji pia moja ya mikakati ya Mkoa ni suala la lishe kupewa kipaumbele na shughuli za lishe zinajumuishwa kwenye mpango kabambe wa Halmashauri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles