30.9 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Washindi Kili Marathon waacha neno Tanzania

kilimanjaro marathon*Watanzania wang’ara Nusu Marathon, waangushwa vibaya mbio ndefu

*Nape asema watashinda mwakani, kutumbua majipu kwenye riadha

NA MWANI NYANGASSA, MOSHI

WASHINDI wa mbio ndefu za kilomita 42 kwa wanawake na wanaume, Kiprotich Kirui  na Alice Kibor, wameeleza kuwa kushindwa kwa Watanzania katika mbio za Kilimanjaro Lager Marathon kunasababishwa na wanariadha kutokuwa makini katika mazoezi, hali inayowapa Wakenya nafasi ya kutawala mbio hizo.

Kirui aliyetokea Kericho, Kenya amefanikiwa kutetea nafasi hiyo baada ya mwaka jana kuwa mshindi katika mbio hizo za kilomita 42, wakati Alice ameshiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza na kushinda ambapo kila mmoja  aliondoka na zawadi ya Sh milioni 4.

Akizungumza na MTANZANIA baada ya kumaliza mbio, Kirui alisema hakuna miujiza kwa Wakenya bali siri ya ushindi kwao ni umakini walionao katika mazoezi kipindi wanapokua wanajiandaa.

“Hakuna miujiza ni mazoezi tu, nawashauri Watanzania wafanye sana mazoezi ili washinde mbio ndefu, nimefanya mazoezi sana ndio maana nina furaha kupata ushindi huu,” alisema Kirui.

Kwa upande wake Alice alisema siri ya ushindi kwa Wakenya ni kufanya mazoezi kwa muda mrefu huku wakiwa na nia ya kushinda hasa kwenye mbio ndefu za kilomita 42.

“Nilijiandaa kwa muda mrefu, nikijua nakuja kushinda Tanzania, niliweka juhudi katika mazoezi na kila siku nilikua nakimbia umbali mrefu kujiweka sawa katika njia zenye milima na tambarare, hatimaye nimeshinda ushindi ambao umenifanya niweke rekodi yangu kwa kuwa najituma,” alisema Alice.

Akizungumza wakati wa kutoa hotuba katika mbio hizo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alitoa rai kwa wanariadha wa Tanzania kutowaangusha wadhamini  na Watanzania kwa ujumla kwa kushindwa kila siku.

“Riadha sasa hivi ni kama lulu kwani tumeona watu kutoka nchi mbalimbali wakitajirika na kujizolea umaarufu mkubwa kutokana na riadha, mfano mzuri ni jirani zetu Kenya.

“Sisi pia tuna uwezo mkubwa hata kuwashinda tukiweka bidii zaidi na kulazimika kutumbua baadhi ya majipu na kuvunja safari za nje mwakani, nitaongoza hili mwenyewe kuhakikisha tunaingiza fitna zozote kuona Watanzania tunashinda hakuna namna, nitaingia mwenyewe si kwa bao la mkono bali kwa kwa gharama yoyote,” alisema Nape.

Naye Rais wa Chama cha Riadha Tanzania (RT), Antony Mtaka, alisema suala la matokeo mabaya kwa Watanzania ni changamoto kubwa sana kwao na kwa waandaaji.

“Watanzania hawajafanya vizuri kama wenzetu kutoka Kenya, hii ni changamoto kwetu kuhakikisha tunafanya vizuri.

“Tunaomba kwa kuanzia, Serikali itembelee kambi ya riadha iliyowekwa West Kilimanjaro, kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya Olimpiki yatakayofanyika Rio De Janeiro, nchini Brazil Agosti mwaka huu,” alieleza.

Kwa upande wake Mkurugenzi Masoko Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Kushilla Thomas, alisema wataendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine kuendeleza riadha nchini.

“Kilimanjaro inajivunia kuwa mdhamini mkuu wa mbio hizo kwa sababu ya umaarufu wake, kwani ndizo mbio kubwa Tanzania, tunaahidi kusaidia mchezo wa riadha nchini ili upige hatua kama zamani,” alisema Thomas.

Hata hivyo, katika mbio hizo zilizofanyika jana Moshi, Kilimanjaro, Wakenya waliendelea kutawala baada ya kushinda karibu nafasi zote za mbio ndefu za kilomita 42 na nafasi za mwanzo katika Nusu Marathon Kilomita 21.

Katika mbio za kilomita 42 wanaume ambazo Kirui alishinda, Mtanzania mmoja tu Sigiarid Ngolly aliyeshika nafasi ya sita ndiye aliingia kwenye nafasi kumi za mwanzo, huku Wakenya wakichukua nafasi zote.

Mbali na ushindi wa Kirui aliyetumia muda wa saa 2:16:42, washindi wengine kwenye kumi bora ni Kenneth Ronoh, Bernard Kimaiyo, Kemboi Mathew, Kipkorir David, Ngollym Alex Bartilol, Timoth Pius, Phillip Ngetich na Kiprono Kirui.

Katika mbio za kilomita 42 wanawake, Mkenya Alice, alishinda akitumia muda wa saa 2:38:03, akifuatiwa na Elizabeth Chamweno, Alice Serser, Euliter Tanvi, Eveline Atancha, Eunice Muchiri, Techlah Chebet, Angel Joseph (Mtanzania), Monica Mengich na Stella Kabui.

Mshindi katika mbio za kilomita 21 wanaume ni Mkenya Benard Mathekha aliyetumia muda wa saa 1:03:23, akifuatiwa na Daniel Muteti (Kenya), Ismail Gallet (Mtanzania), Fabian Naasi (Mtanzania), Geay Gabriela (Mtanzania), Kiptoo Nicholaus (Kenya), Benard Korir (Kenya), Reginald Lucian (Tanzania), Elly Sang (Kenya) na Augustino Sulle (Tanzania).

Kilomita 21 wanawake mshindi alikuwa Mkenya Grace Kimanzi, aliyetumia muda wa saa 1:14, akifuatiwa na Vicoty Chepkemoi (Kenya), Failuna Matanga (Mtanzania), Angelina Tsere (Mtanzania), Catherine Yuku (Mtanzania), Jane Mula (Kenya), Amina Ngoo (Mtanzania), Adelina Asimwe (Mtanzania), Neema Kusuda (Mtanzania) na Eumice Musa (Mtanzania).

Wadhamini wengine wa Kilimanjaro Marathon ni Grand Malt – Kilomita 5 na wale wenye meza za maji ni Kilimanjaro Water, RwandAir, CMC Automobiles, KK Security, Kibo Palace, TPC Limited, FNB na Keys Hotel.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles