25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Washauri maombi kufanyika nchi nzima kudhibiti corona mpya

Na Allan Vicent, Tabora

Waumini wa madhehebu mbalimbali ya dini hapa nchini wameshauri kufanyika maombi ya nchi nzima ili kukabiliana na maambukizi hatarishi ya ugonjwa mpya wa covid-19 ambao huathiri kwa kiasi kikubwa mfumo wa upumuaji.

Ushauri huo umetolewa Februari 17, kwa nyakati tofauti na waumini mbalimbali walioongea na gazeti hili ambapo walishauri viongozi wa dini kuitisha maombi ya siku tatu katika nyumba zao za ibada ili kumwomba Mungu atuepushie mbali ugonjwa huo wa pili.

Mwinjilisti Hanga Hangaya mkazi wa Tabora akinukuu maandiko ya kitabu cha Luka 1:37 alisema kuwa hakuna jambo lolote lililogumu la kumshinda Mungu, kinachotakiwa sasa ni kufunga na kuomba ili ugonjwa huo uondoke.

Alisema kuwa viongozi wa dini wanapaswa kuwa na macho ya rohoni na kuisaidia serikali kwa njia ya maombi ili kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo ambayo yanaendelea kusambaa kwa kasi na kupoteza roho za watu,

‘Rais wetu Dk. John Magufuli, ana imani kubwa ndiyo maana ugonjwa wa kwanza ulipoingia aliitisha maombi ya nchini nzima na Mungu akaliponya taifa, sasa umekuja kwa namna nyingine, viongozi wa dini chukueni hatua,’ alisema.

Alfa Kabombo mkazi wa Temeke jijini Dar es salaam akiongea na gazeti hili kwa njia ya simu alisema kuwa ugonjwa huu ni adui mwingine wa maendeleo, na unaathiri nguvu kazi ya taifa, hivyo viongozi wa dini hawapaswi kukaa kimya.

Alisisitiza kuwa kama alivyofanya Rais Magufuli mara ya kwanza kwa kutangaza maombi ya siku tatu ya nchi nzima kwa ugonjwa wa kwanza na Mungu akasikia kilio chetu, hata sasa tukimwomba atasikia na kutuondolea ugonjwa huu.

Mkazi wa wilaya ya Urambo mkoani Tabora, Asha Maulid, alishauri Mashekhe, Maaskofu, Mapadre na Wachungaji kuitisha dua na sala katika nyumba zao za ibada ili kumwomba Mungu, inshallah atatuepusha na balaa hili.   

Kwa upande wake, Magdalena Yusufu, mkazi wa Nzega Mkoani hapa aliwataka waumini wa kanisa Katoliki hapa nchini ambao wameanza kipindi cha mfungo wa kwaresima kutumia nafasi hiyo kumwomba Mungu ili atuondolee ugonjwa huo.

Alishauri viongozi wa madhehebu yote kwa kushirikiana na viongozi wa serikali kuitisha maombi kwa waumini wao ili kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo ambao huathiri mfumo wa upumuaji kwa kiasi kikubwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles