26.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Wasaka urais CCM wapigana vikumbo mikoani

LOWASSAAANa Waandishi Wetu
HEKA HEKA za kusaka wadhamini mikoani kwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaowania kugombea urais zimeendelea kushika kasi mikoani.
Wakati hayo yakiendelea, Mwenyekiti Mstaafu na kada mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kagera, Pius Ngeze ametangaza rasmi kumuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika harakati zake za kutafuta kuwa mgombea urais kupitia chama hicho.
Ngeze aliyekuwa miongozi mwa viongozi wa chama hicho mkoani humo waliojumuika katika mapokezi ya Lowassa aliyewasili mjini Bukoba saa 6.00 mchana akitokea Sumbawanga, alisema kama alivyomuunga mkono Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005 na akashinda, pia anamuunga mkono Lowassa.
“Leo ndiyo leo. Kila siku mnaniuliza, Mzee Ngeze uko wapi… Sasa leo nawatangazia rasmi mbele yenu. Kama nilivyomuunga mkono Rais Kikwete mwaka 2005 na akashinda, natangaza Kagera na dunia nzima, namuunga mkono Lowassa… hata kwenye fomu ya udhamini nimekuwa mtu wa kwanza,” alisema Ngeze huku akishangiliwa na umati wa wanachama na wapenzi wa CCM katika ofisi ya chama hicho mkoa.
Akitaja sababu ya kumuunga mkono Lowassa, Ngeze alisema haoni mgombea mwingine wa kumshinda na kwamba ana uamuzi mgumu.
“Ukiangalia wagombea wote walio nyuma yake, yeye ndiye kiongozi pekee anayeweza kuingia Ikulu na kudumisha yale yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete.
“Anajulikana kwa uamuzi mgumu na nchi yetu inahitaji watu wenye uamuzi kama huo. Lowassa hajawahi kuajiriwa na Serikali, tangu alipomaliza chuo kikuu alichukuliwa pamoja na Rais Kikwete na wengine wawili kukitumikia Chama cha Mapinduzi,” alibainisha Ngeze.
Aliendelea kumwagia sifa Lowassa akisema ndiye aliyejenga shule za sekondari za kata na kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria kwenda mikoa ya Shinyanga na Tabora.
Lowassa akiwashukuru wana CCM waliomdhamini kuwania kuteuliwa kugombea urais kupitia CCM, alisema kupata wadhamini wengi ni kufunga bao la urais.
“Nawashukuru sana kwa mapokezi makubwa mliyonipa. Wadhamini wanaotakiwa kila mkoa ni 30 tu, lakini nikipata 2000, 4000 au 7000 nashukuru kwani inaonyesha imani na upendo wenu kwangu. Imani hujenga imani… Niliwaambia Shinyanga kuwa ukiona watu wengi ujue umefunga bao na ninyi ndiyo mtaniwezesha kufunga,” alisema Lowassa.
Akizungumzia sababu ya kugombea urais, Lowassa alisisitiza kuwa anachukia umasikini hivyo anataka kupambana nao kwa mwendo wa mchakamchaka.
“Nakerwa sana na umasikini. wapo baadhi ya viongozi wanaovaa nguo mbaya wanadhani ni sifa. Ni aibu kuwa masikini, ni aibu kuishi chini ya dola moja kwa siku, nikishinda nitapambana na umasikini kwa mwendo wa mchakamchaka,” alisema Lowasssa.
Alisema ili kufikia maendeleo ya kweli ni lazima kubadilishwa mtazamo wa kazi na watu wafanye kazi kwa bidii.
“Ukifanya kazi unapewa pole, ya nini? Kana kwamba kazi ni hisani, unatakiwa upewe hongera. Mungu ametupa akili na nguvu ni lazima tufanye kazi kwa bidii kuondoa umasikini. Kwa nini Uganda watushinde? Kwa nini Kenya na Wanyarwanda watushinde?” alihoji Lowassa.
Aliwahimiza pia wana CCM hao kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura waweze kupiga kura wakati wa uchaguzi.
Naye Mbunge wa zamani wa Bukoba Vijijini, Nazir Karamagi alisema wana CCM waliomdhamini Lowassa wamefikia 6500.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma, Dk. Walid Kaborou, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa, Hypolitus Matete, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja na Mwenyekiti mstaafu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita.
Profesa Mwandosya
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais(Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, amesema wananchi wengi wanaojitokeza kuwadhamini wana CCM wanaowania kuteuliwa na chama chao kupeperusha bendera katika Uchaguzi Mkuu ujao, wahamasishwe pia kujiandikisha katika Daftari la Wapiga Kura.
Profesa Mwandosya ambaye ni mmoja wa wana CCM zaidi ya 30 waliochukua fomu ya kuwania nafasi hiyo, alisema hayo jana mjini Moshi alipokuwa akizungumza na wanaCCM wenzake waliojitokeza kumdhamini katika mbio hizo.
Katika siku ya jana wengi wa waliojitokeza kumdhanini Profesa Mwandosya walikuwa ni wasomi wa Chuo Kikuu cha Ushirika lakini pia walikuwapo mabalozi wa nyumba 10 na viongozi wa kata.
Profesa Mwandosya alionesha kufurahishwa baada ya kusikia kati ya wadhamini wake kwa siku ya jana walikuwa ni wasomi na kusisitiza wamemkumbuka alipokuwa Chuo Kikuu akifundisha lakini kinachokosekana wakati ule alitumia chaki lakini sasa wanatumia mitandao.
Pinda atua Katavi
Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameanza safari ya kusaka wadhamini kwa kuzuru Mkoa wa Katavi.
Pinda ambaye aliwasili Mpanda jana, alipokelewa na maelfu ya wakazi wa mji huo ambao walimsindikiza kutoka Uwanja wa ndege hadi nyumbani kwake, Makanyagio.
Akiwa mkoani Katavi ambapo pia ndiyo nyumbani kwake Pinda, alipata wadhamini 4,243 katika vituo viwili tu vya Inyonga na Mpanda Mjini. Ratiba yake inaonyesha atazuru vituo vitatu katika Mkoa wa Katavi.
Pinda bado anaendelea na safari ya kuelekea kijijini kwake Kibaoni, kata ya Mpimbwe, wilayani Mlele ambako ni upande wa bondeni wa Wilaya ya Mlele ambako pia kuna wadhamini wanamsubiri.
Dk. Migiro ajitosa rasmi
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha Rose Migiro jana amekuwa mwanamke wa nne kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kuwa mgombea wa urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Dk. Migiro alichukua fomu hiyo mjini Dodoma jana akiwa amefuatana na mume wake na Mwanasiasa Mkongwe na Mbunge wa Viti Maalum, Mama Anna Abdallah.
Akijibu maswali kuhusu vipaumbele vyake endapo atafanikiwa kuteuliwa kuwa mgombea wa kiti hicho na hatimaye kuwa Rais wa Tanzania, alisema atasimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM ambayo bado inaandaliwa.
“Katika historia ya nchi yetu, viongozi wote huongozwa na Ilani ya chama , ilani ya sasa imeainisha maeneo ya vipaumbele, nina imani ilani inayoandaliwa itazingatia utekelezaji wa ilani ya sasa,” alisema.
Aliyataja baadhi ya masuala yaliyozingatiwa katika Ilani ya sasa kuwa ni uwezeshaji wa wananchi, kuwa na uchumi wa kisasa na mazingatio kuhusu kuulinda muungano
“Mambo mengi mazuri yamefanyika katika awamu hii ya uongozi na ilani ya inayokuja itayaendeleza hivyo nyenzo yangu kubwa ya kazi itakuwa ni hiyo,” alisema.
Alisema akipata fursa ya kuongoza nchi nyenzo yake kuu itakuwa ni kukuza uchumi na kuhakikisha mafanikio yanakuwa endelevu na yanawanufaisha wananchi.
“Lakini pia vipaumbele vyangu vitategemea kadri ya maendeleo na mahitaji yanayojitokeza,” alisema.
Akijibu swali kuhusu nafasi ya Unaibu Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Kimataifa kama alipewa kwa upendeleo, alisema siyo kweli kwa kuwa viongozi wa umoja huo huteuliwa baada ya kufanyiwa uchunguzi kwa muda mrefu.
“Unapochaguliwa kuwa kiongozi UN unapitia mchujo mkali, hakuna nafasi ya rafiki, kwa maadili ya UN ni kosa kupewa kazi kwa kujuana, ushawishi au ujamaa.
“Kabla ya Tanzania nafasi yangu ilikuwa inashikiliwa na mtu wa kutoka Uingereza lakini alipokuja Ban Ki-moon akaamua kwamba nafasi hii itoke Bara ya Afrika na kwa mara ya kwanza, nikabahatika kuipata mimi hata hivyo nafasi ilikuwa ni ya Tanzania,” alisema.
HABARI HII IMEANDALIWA NA ELIAS MSUYA (BUKOBA), SARAH MOSSI (KILIMANJARO) NA DEBORA SANJA (DODOMA)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles