30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wasafirishaji kemikali bashirifu wapewa neno

MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

WADAU wanaoagiza, kusafirisha na kutumia kemikali bashirifu nchini wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya kemikali hizo ili kuepusha kuchepushwa na kutumika kinyume na matumizi yaliyolengwa ikiwemo kutengeneza dawa za kulevya.

Akizungumza Dar es Salaam jana kwa niaba ya Mkemia Mkuu wa Serikali  katika mkutano wa pamoja kati ya mamlaka za udhibiti na wadau wa sekta binafsi katika kuzuia uchepushaji wa kemikali bashirifu, Kaimu Mkurugenzi wa Sayansi Jinai na Huduma za Vinasaba, David Elias, alisema Serikali imekuwa ikitumia njia mbalimbali ili kuongeza jitihada ikiwemo kutunga sheria kwa lengo la kupambana na kudhibiti uchepushwaji wa kemikali bashirifu ambazo zinaweza kutumika kutengeneza dawa za kulevya.

“Kama njia mojawapo ya kusimamia mwenendo wa biashara na matumizi ya kemikali bashirifu, Serikali kupitia mamlaka za udhibiti imeunda sheria na kanuni mbalimbali za kusimamia na kudhibiti uingizaji, usambazaji, usafirishaji, utumiaji, utekelezaji na usafirishaji wa kemikali nje ya nchi.

“Hivyo ni muhimu kwa wadau wa sekta binafsi wanaojishughulisha na kemikali mbalimbali ikiwa pamoja na kemikali bashirifu, kuelewa sheria na kanuni ili kuzitekeleza,” alisema.

Alisema kuwa mkutano huo utatoa ufafanuzi juu ya uchepushaji wa kemikali bashirifu na ushirikishwaji wa sekta binafsi katika udhibiti.

“Ni matumaini yetu kwamba wadau mliopo kwenye mkutano huu mtapata uelewa wa kemikali bashirifu ni nini na umuhimu wa kudhibiti, uelewa wa sheria na kanuni za udhibiti na mbinu zinazotumika katika kuchepusha kemikali hizo.

“Hivyo naomba muwe huru kujadiliana, kutoa mapendekezo ya namna bora ya kushirikiana kati ya mamlaka za udhibiti na sekta binafsi ili kufikia lengo la Serikali katika kudhibiti mianya yote inayoruhusu uchepushwaji wa kemikali bashirifu,” alisema Elias.

Kamishna wa Ukaguzi na Sayansi Jinai kutoka Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya, Bertha Mamuya,  alisema wanaamini ushirikishwaji wa wadau wa kemikali utaongeza ufanisi katika kudhibiti uchepushaji wa kemikali.

“Kama Serikali tunaamini ushirikiano na wadau wa kemikali katika kujisimamia na kushirikiana na mamlaka husika kutaongeza ufanisi katika kudhibiti uchepushwaji wa kemikali bashirifu, hivyo kufanikisha vita dhidi ya dawa za kulevya.

“Ni matumaini yangu majadiliano katika mkutano huu yatachagiza nia njema ya uanzishwaji wa ushirikiano wa hiari kati ya wadau na mamlaka za udhibiti ili kufanikisha lengo la Serikali katika upatikanaji wa dawa za kulevya,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles