KAMPUNI ya masuala ya kijeshi ya Urusi, Wagner Group, itatuma wapiganaji wake nchini Mali kwa lengo la kuvisaidia vikosi vya Serikali katika mapambano yake dhidi ya waasi.
Kwa mujibu wa taarifa, kampuni hiyo itakayolipwa Dola milioni 10.8 (zaidi ya Sh bil. 25 za Tanzania) kwa mwezi, itatuma wanajeshi 1,000, ingawa vyanzo vingine vimedai kuwa idadi hiyo ni ndogo kuliko inayotarajiwa kufika Mali.
Katika mkakati huo, Wagner Group itahusika kuwalinda viongozi wa Serikali ya Mali, achilia mbali kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa nchi hiyo ya Magharibi mwa Bara la Afrika.
Aidha, zipo taarifa zingine zinazodai kuwa Ufaransa haijafurahishwa na makubaliano hayo na badala yake ilitamani ibebe jukumu la kuisaidia Mali ambayo ni koloni lake la zamani.