30.3 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

WARAKA WA PRU KIMITI KWA WATANZANIA

KIFO hakizoeleki ingawa kipo na tunaishi nacho, kila uchwao kimekuwa kikichukua wazazi wetu, watoto wetu, dada, kaka, jamaa, rafiki na hata jirani zetu.

Kama kifo kingeweza kuonekana, naamini hakuna mtu angekubali kukutana nacho. Hata walemavu wa miguu wangekikimbia.

Kifo ni fumbo la imani ambalo halijapata wa kulifumbua kwa miaka dahari sasa.

Ugumu wa kukiona kifo umekuwa mtihani hata kwa majemedari na mashujaa wa kijeshi. Ushujaa wao unakuwa ni udhaifu mbele ya kifo.

Ubaya wa kifo ni kutokuchagua, kifo kinachukua wema na wabaya, wakubwa na hata wadogo.

Kifo sasa kinailiza dunia, kifo kimemchukua shujaa wa Tanzania, mpambanaji na jemedari wa kweli Dk. John Pombe Magufuli.

Dk. Magufuli sasa ni hayati, mwili wake umo ndani ya jeneza, amelala, amelala milele na hawezi kupumua tena.

Kwa sasa kaburi ndio makazi yake, hawezi kusimama tena na kuwakemea mafisadi na wadhalimu waliokuwa wakipoka haki za wanyonge.

Mwangwi wa vilio vya Watanzania, Waafrika na dunia kwa ujumla, unaelekea Chato yalipo makazi yake ya milele.

Watu wanalia, wanamkumbuka, hakuna aliyeamini kama mwamba imara umeanguka.

Kifo kimetuondolea mpigania haki, kifo kimetupokonya jasiri wa karne ya 21, hakika Dk. Magufuli anastahili kuliliwa milele.

Mimi Prudencia Paul Kimiti ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Uhalifu wa Ushuru wa Forodha ndani ya Mamlaka ya Mapato na Kodi nchini Uingereza (HMRC), sitaacha kumlilia.

Na ili kutimiza ahadi yangu hiyo nimeiona haja ya kuandika Waraka wangu kwa Watanzania wenzangu.

Imani yangu ni kuwa Waraka wangu huu utasalia kwa miaka mingi kuwa kumbukumbu ya maombolezo yangu kwa Hayati Dk. Magufuli na Tanzania kwa ujumla.

POLE

Nianze kwa kuwashukuru Watanzania kwa mapenzi makubwa waliyoyaonesha kwa nchi na kwa Hayati Dk Magufuli.

Wamemuenzi kishujaa na kuionesha dunia kuwa walikuwa na mapenzi ya kweli na Dk. Magufuli ambaye alipachikwa majina mengi ya kishujaa kama vile Bulldozer, jembe na jiwe.

Pili nachukua nafasi hii adimu na adhimu kumpa pole Rais mama Samia Suluhu Hassan.

Wote tunakubali kuwa kwa sasa tumo ndani ya kipindi kigumu kilichojaa majonzi na maombolezo makubwa.

Aidha nampa pole Mama Janeth Magufuli na familia yote ya hayati Dk. Magufuli, ndugu, jamaa, marafiki na kwa Watanzania wote popote walipo ndani na nje ya nchi.

Kifo cha Dk. Magufuli kimetuumiza wote, na tunapaswa kumwomba Mwenyezi Mungu azidishe Upendo kwa Watanzania na hasa kwa mama yetu Rais Samia.

Tunamwomba awe jasiri na shupavu katika kuendelea kuwapigania raia wake hasa wanyonge, kulinda uhuru wetu, maslahi, haki na heshima yetu kama Taifa.

Tuna imani kubwa kwamba chini ya uongozi wake imara na shupavu hatuwezi kuwa wapweke wala wakiwa.

Imani hiyo hiyo inatupa matumaini kuwa ataendelea kutimiza majukumu ya kuliongoza na kulivusha taifa letu kwenye mambo yote yanayolikabili sasa na siku zijazo – kwenye raha na karaha.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu amlinde, na ampe nguvu ya kuendelea kulinda maslahi ya Watanzania ambayo hayati Dk. Magufuli aliwapigania usiku na mchana.

Sisi tulio ughaibuni, mioyo yetu inaungana nanyi nyumbani katika maombi, machumgu, maumivu na huzuni.

Mola atupe faraja, subira na utulivu.

RAI YANGU

Rai yangu kwa viongozi, nawasihi kamwe wasiache kuiga na kuyatafsiri maisha ya hayati Dk. Magufuli.

Wamuenzi kwa vitendo kwa kuendeleza yote aliyoyasimamia, kuukataa uzembe, kuikataa rushwa, kuupinga ufisadi na kuwatetea Wanyonge na kuipenda nchi yetu.

Naamini hakuna linaloshindikana, kama yeye aliweza basi na wao wanaweza, wanaweza kwa sababu walishayaweza hayo pamoja nae. Wanachotakiwa kufanya sasa ni kuyaendeleza tu.

MAMA SAMIA ANAWEZA

Mama Samia ni kati ya kina mama jasiri wanaoweza kuifikisha nchi mahali alipotarajia Hayati Magufuli.

Uzoefu wa kazi aliuonyesha akiwa Serikalini Zanzibar unatosha Sisi kuwa na imani nae.

Alipoteuliwa na Wabunge wa Bunge la Katiba kumsaidia Marehemu Samuel Sitta, ilidhihirisha wazi kuwa ni mwanamke shupavu na hodari.

Kuwa kwake Makamu wa Rais kunaakisi uwezo wake wa kuwa shujaa na sauti ya wanyonge kama ilivyokuwa kwa Hayati Dk. Magufuli ambaye walifanya Kazi kwa kipindi cha miaka mitano na miezi minne.

Muda huu ulitosha kunoa makali yake ya kiuongozi.

Naamini hata Hayati Dk. Magufuli alimwamini na ndio maana mwaka 2015 alimteua tena kuwa msaidizi wake wa karibu .

Mama huyu anafaa kuendeleza mapambano katika kipindi kingine cha pili.

Mama Samia ni mpambanaji anajua mbinu zote za kivita kwenye mapambano haya ya kiuchumi.

Ni nahodha mwenye uwezo wa kulifikisha salama jahazi hili la Tanzani.

Sisi watanzania bila kujali tupo eneo gani la nchi hii tutakuwa naye na tunamtakia kheri ili alifikishe jahazi hili salama.

Poleni Watanzania wenzangu, poleni Waafrika na pole kwa dunia.

Sote tunakiri kuwa kifo hakina huruma na ndio maana imetuchukulia shujaa wetu Dk. John Joseph Magufuli.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles