28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wapinzani walia na matangazo ya ‘Live’  

Japhary Michael..Na Elizabeth Hombo, Dodoma

KAMBI ya Upinzani bungeni, imesema kitendo cha Serikali kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge, kinazua maswali mengi, pengine ina mpango wa siri wa kufuja fedha za umma katika matumizi yasiyo ya lazima.

Kauli hiyo, ilitolewa na Waziri Kivuli  wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Japhary Michael wakati akiwasilisha Hotuba ya Kambi ya Upinzani kuhusu makadirio ya mapato na matumizi Ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha 2016/17.

“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali kufuta mara moja katazo la kurusha matangazo ya Bunge moja kwa moja kupitia television ya Taifa na vyombo vingine vya habari vilivyokuwa vikirusha matangazo hayo awali, ili wananchi ambao ndio msingi wa mamlaka ya serikali wapate haki yao ya msingi ya kufuatilia mwenendo wa mgawanyo wa fedha zao katika bajeti ya serikali kutoka moja kwa moja bungeni.

“Wananchi wana haki kujua serikali yao inafanya nini na serikali inawajibika kuwapatia wananchi taarifa juu ya utendaji wake wa kazi.

“Katika hali ambayo haijaeleweka bado serikali ya awamu ya tano imeamua kwa makusudi kutumia mabavu kukataza urushwaji wa moja kwa moja wa vipindi vya majadiliano ya Bunge ili wananchi wasijue kinachoendelea bungeni.

“Ni muhimu wabunge wakafahamu, bajeti ya Tamisemi inayoombwa kuidhinishwa na Bunge kwa mwaka wa fedha 2016/17, ni Sh trilioni 6.8 sawa na asilimia 23 ya bajeti yote ya serikali.

“Fedha hizi ni za walipa kodi, kujadili na kupitisha matumizi ya fedha za umma nyingi namna hii bila wananchi kuwa na fursa ya kuona jinsi Bunge lao linavyofanya kazi ya kuwawakilisha katika kazi hiyo, si tu kuwakosesha haki, bali pia kunazua maswali mengi, pengine Serikali na mpango wa siri wa kufuja fedha za umma katika matumizi yasiyo ya lazima ndio maana haitaki wananchi wajue kinachoendelea bungeni,”alisema.

Alisema adhabu inayowafaa wabunge wa CCM ya kushabikia ufisadi, huku wakipuuza maoni ya upinzani, ni kufutwa katika uwakilishi wa wananchi.

Alisema tamthilia inayofanyika hivi sasa ya waliokuwa watetezi wakubwa wa ufisadi ya kutumbua majipu ni sawa na mchawi kutaka kurudisha msukule wake ambao yeye mwenyewe ndiye aliyeuroga hadi jamii ikaamini kuwa umekufa.

Japhary ambaye pia ni Mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), alisema kambi hiyo inaitaka Serikali kuleta muswada wa marekebisho ya sheria za serikali za mitaa, ili sheria itamke kuwapa mameya na wenyeviti wa halmashauri nguvu ya kiutendaji tofauti na sasa ambapo wanatambulika kiitifaki.

“Pia tunapendekeza nafasi za kazi za wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, miji na majiji zitangazwe na waombaji wafanyiwe usaili kama ilivyo kwa watumishi wengine wa umma na si kwa uteuzi wa kisiasa kama ilivyo sasa,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles