WAPIGA DILI WAMZUIA JPM KWENDA NJE

0
541

Na ELIZABETH HOMBO, DAR ES SALAAM NA BENJAMIN MASESE, MWANZA

WAKATI utawala wa Rais Dk. John Magufuli ukikaribia mwaka wa pili, huku akiwa amesafiri nje ya nchi mara chache ikilinganishwa na watangulizi wake, amevunja ukimya akisema kwamba anataka kwanza kumaliza wapiga dili ambao akiondoka wataweza kufanya mambo ya ajabu.

Amesema tangu aingie madarakani amepata mialiko zaidi ya 60 kwenda nje ya nchi, lakini ameikataa kwa sababu anataka kuishughulikia Tanzania kwanza.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana wakati akizindua mradi wa uboreshaji maji wa Sengerema akiwa katika ziara yake mkoani Mwanza.

“Ndiyo maana mimi sitembei sana, nikienda huko watafanya ya ajabu, ngoja nidili nao kwanza, lazima nihakikishe nasafisha kwanza.

“Leo (jana) nilitakiwa niwe Ethiopia kwenye mkutano wa AU, nimeona nimtume makamu wangu (Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan), ameniwakilisha na anafanya kazi vizuri, mimi ngoja nidili na ya watu kwa sababu nilichaguliwa kwa ajili ya Watanzania, safari nitaenda nikishastaafu.

“Ngoja nizifanyizie safari humu humu ndani kwani ningejuaje kama kuna Sh bilioni mbili za maji zimeibwa na kama wapo walioziiba waanze kuzirudisha.

“Kabla sijaondoka vyombo vyangu vitaanza kufuatilia kwa sababu nina Serikali iko hapa. Lazima mali za watu masikini ziende kuwanufaisha watu, ndio wajibu wangu na ndio haki yao,” alisema.

Tangu kuingia madarakani, nje ya Afrika Mashariki, Rais Magufuli ameenda Addis Ababa, Ethiopia kuhudhuria Mkutano wa 28 wa Baraza Kuu la Umoja wa Afrika (AU).

Mbali na hiyo, ametembelea nchi za Rwanda, Uganda na Kenya kwa ziara za kikazi.

Katika mikutano ya kimataifa, amekuwa akiwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustine Mahiga, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Samia amewahi kumwakilisha Rais Magufuli katika mikutano iliyofanyika nchi za Rwanda, Ethiopia, Papua New Guinea, Swaziland, Zambia na Afrika Kusini, huku Majaliwa akimwakilisha katika mikutano iliyofanyika Botswana, Uingereza na Kenya.

 

MIMBA SHULENI

Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli pia alipigilia msumari msimamo wake wa kutoruhusu wanafunzi waliopata mimba kutoendelea na masomo katika utawala wake.

Juni 22, mwaka huu, akiwa katika ziara yake ya siku tatu mkoani Pwani, Rais Magufuli alisema katika utawala wake hakuna mwanafunzi atakayepata mimba na kuruhusiwa kurudi shule.

Akizungumza jana, Rais Magufuli alisema mwalimu mkuu atakayeruhusu mwanafunzi aliyejifungua kurudi shule na kuendelea na masomo katika shule za Serikali, atafukuzwa kazi.

“Ni kweli pia kuwa wanafunzi waliopata mimba hawatarudishwa shuleni, lakini kuna ujanja ujanja wa walimu, wanaandika cheti kuwa alilazwa.

“Nikimuona mwalimu mkuu amerudisha mwanafunzi aliyepata mimba kwenye shule za Serikali, ataondoka yeye.

“Niwaombe wazazi wawachunge watoto, hizi mimba zinatokana na wazazi wetu, ni lazima wazazi tujifunze kulea, tumechagua kueleza ukweli, tuambiane ukweli,” alisema.

Pia alizitaka asasi za kiraia (NGO’s) kufungua shule kwa wanafunzi wanaopata mimba shuleni kama kweli zinawapenda.

“Si kwamba nawachukia wenye mimba, hata kwa bahati mbaya akapata mimba, kama hizo NGO’s zinawatetea sana, zifungue shule za wenye mimba kwa sababu zinawapenda wenye mimba, wafungue shule zao,” alisema.

Pamoja na hilo, pia aliwataka wale wanaofanya makongamano ya kuhamasisha watu wapate mimba wafungue shule zao kwa wanafunzi wao.

“Haiwezekani fedha za walipakodi Sh bilioni 17 kila mwaka za kusomesha watoto wetu, kwenda kusomesha wakinamama, wazunguke, waimbe, waseme nini, lakini mimi ndiyo rais, huo ndio ukweli.

“Watapiga kelele, waimbe, wazunguke wee, lakini mimi ndiyo rais,” alisema Rais Magufuli.

Alisema tatizo si wanaopata mimba, kwani wapo waliopata matatizo, kama kuugua kwa muda mrefu wakashindwa kwenda shule, lakini ulianzishwa mpango maalumu wa kuwasomesha katika mfumo usio rasmi.

HATI YA DHARURA MISWADA

Akizungumzia kuhusu miswada mitatu iliyowasilishwa bungeni kwa hati ya dharura, alisema aliamua kufanya hivyo kwa sababu nchi iliibiwa sana kwa upande wa madini.

Miswada iliyowasilishwa bungeni kwa hati ya dharura ni pamoja na wa madini ambao umejadiliwa katika kamati za Bunge.

Mwingine ni muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali zenye upungufu uliojitokeza wa mwaka 2017 ambao nao umefanyiwa kazi na Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria.

“Nimeamua kupeleka muswada huu kwa dharura, kwangu mimi wizi tuliokuwa tunatendewa tulikuwa watumwa sisi Watanzania wote, kila kitu kinasombwa, nikaona hakihitaji kusubiri hadi mwaka, hiki kwangu nilikiona ni dharura kwa sababu ndiko uchumi wa Tanzania ulikolala.

“Lakini dhamira yangu huwa inaumiza, watu wengine wanapokwenda kupinga hadharani hata kwa kuchezewa na baada ya kupeleka muswada huu kwa dharura hao hao wanasema hapakuhitajika dharura, tungesubiri Bunge la Novemba, waendelee kuiba hapa.

“Lakini wao wakitaka hata wagombea wao wanafanya dharura, walipotaka rais wao kwani walichelewa, walisubiri hata mwaka, ilikuwa dharura bila kufuata utaratibu wa kawaida. Tunaibiwa kila siku tunasombwa. Je, sio la haraka hili?

“Tunalipa mabilioni ya ajabu, mtu alikuwa yuko radhi kuuza maisha ya Watanzania kwa pickup, tumefanya mikataba ya ovyo, tumebinafsisha viwanda vyetu tukavigawa. Sitaki kuwalaumu kwa kufanya hivyo, lakini sizuiliwi kuzungumza ukweli,” alisema Rais Magufuli.

Aidha, mkuu huyo wa nchi pia alimsifia Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo, akisema ni mchapakazi na kwamba pamoja na kwamba ni mwanachama wa ACT-Wazalendo, lakini anaipenda CCM.

“Profesa Kitila yeye alikuwa ACT-Wazalendo, lakini ni mchapakazi na ameahidi kutekeleza ilani ya CCM. Maendeleo hayana chama na anavyoonekana usoni ni ACT, lakini yeye moyo wake ni CCM,” alisema.

PEMBEJEO

Rais Magufuli alisema mchakato wa uchunguzi wa pembejeo utaanza nchi nzima ili kubaini mchezo mchafu uliokuwa ukifanywa na viongozi kwa kuandikisha majina hewa ya wakulima.

“Wakati tulipoanzisha juu ya watumishi hewa, tuliwagundua 19,000, vyeti feki vilikutwa zaidi ya 10,000, katika mradi wa kuwezesha kaya masikini vijijini (Tasaf) tulibaini kaya 56,000 na wanafunzi 65,000 tulikuta wanapokea mikopo hewa, hii ndiyo Tanzania ilipokuwa imefikia.

“Sasa natangaza rasmi kuanzisha uchunguzi wa ugawaji wa pembejeo, kuna watumishi waliandikishwa kuwa wamepewa mbolea kumbe hakuna na hata hawapo duniani, ninachotaka Tanzania inyooke, nikitoka anayekuja aongoze kwa raha,” alisema.

Pia alizungumzia uvuvi haramu na kuagiza vyombo vya dola kusimamia hilo kikamilifu, huku akionya baadhi ya viongozi kuhusika kwa kupokea rushwa.

Pia alisema Serikali imeongeza bajeti ya afya kutoka Sh bilioni 30 ya mwaka 2016/17 hadi Sh bilioni 250 katika bajeti ya mwaka huu ya 2017/18 ikiwa lengo ni kununua dawa, vitanda.

Rais Magufuli alisema kuwa katika sekta ya nishati, Tanzania ya viwanda inakwenda sambamba na uhakika wa umeme, hivyo Serikali yake imekusudia kuendeleza miradi mikubwa ambayo itazalisha umeme mkubwa.

Alisema tayari amezungumza na benki mbalimbali za nje ya nchi kuwezesha miradi mikubwa ya maji.

Katika ziara yake, wananchi walisimamisha msafara wake mara kwa mara na kumwelezea shida ya maji, huku Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, akilazimika kumwomba radhi kwa kitendo hicho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here