26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

WAPAKISTANI KORTINI KWA KOSA LA UHUJUMU UCHUMI

Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam


SERIKALI imewafikisha mahakamani raia saba wa Pakistan na Sri-Lanka kwa makosa ya uhujumu uchumi na kuisababishia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hasara ya Sh milioni 459.

Washtakiwa hao walifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Raia  wa Pakistan ni Dilshad Ahmed (36), Rohail Yaqoob (47), Khalid Mahmood (59) na Ashfaq Ahmad (38) na raia wa Sri-Lanka ni Muhamad Aneess (48), Imtiaz Ammar na Ramesh Kandasamy.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga kwa kushirikiana na Wakili wa Serikali Mkuu Johannes Karungula kutoka TCRA, waliwasomea washtakiwa mashtaka saba yanayowakabili.

Katuga alidai washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujipatia kwa udanganyifu huduma za mawasiliano, kuendesha huduma za mawasiliano bila kuwa na leseni kutoka TCRA, kuingiza na kusimika vifaa vya mawasiliano bila ya leseni, kutumia vifaa ambavyo havijathibitishwa na mamlaka hiyo na kuisababishia hasara ya Sh milioni 459.

Inadaiwa kabla ya Novemba, 2016, jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao  walikula njama ya kutenda kosa la matumizi ya huduma za mtandao kinyume cha sheria.

Alidai katika tarehe tofauti kati ya Novemba 2016 na Februari, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, washtakiwa walijipatia huduma za mtandao kwa nia ya kukwepa gharama za malipo halali kwa kujipatia huduma hiyo kwa kutumia njia ya mawasiliano ambayo haijasajiliwa.

Katuga alidai katika kipindi hicho, mkoani humo waliendesha huduma za simu za kimataifa bila ya kuwa na leseni inayotolewa na TCRA.

Katika shtaka la nne, washtakiwa hao wanadaiwa  Novemba 20, 2016, jijini Dar es Salaam, kinyume cha sheria, waliingiza nchini vifaa vya mawasiliano ambavyo ni Sim Box  bila ya kuwa na leseni inayotolewa na mamlaka hiyo.

Wanadaiwa  tarehe isiyofahamika Novemba, 2016, Dar es Salaam, walisimika na kutumia vifaa vya mawasiliano ambavyo ni Sim Box yenye namba 115200.8.n.t.n na kompyuta mpakato mbili aina ya Dell bila ya kuwa na leseni kutoka TCRA.

Pia wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Novemba 2016 na Februari, mwaka huu, Dar es Salaam, kwa njia ya udanganyifu walitumia vifaa hivyo vya mawasiliano kwa kuunganisha katika huduma ya mawasiliano kwa lengo la kupata  mawimbi  ya mtandao bila ya kuthibitishwa na TCRA.

Katika kipindi hicho washtakiwa wanadaiwa kuwa kwa kutumia vifaa vya mawasiliano visivyosajiliwa, waliisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh milioni 459.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, kwa kuwa shauri lao linasikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Makosa ya Uhujumu Uchumi na Rushwa.

Hakimu Mashauri aliwataarifu washtakiwa hao kwamba mahakama hiyo haina uwezo wa kutoa dhamana, hivyo watatakiwa kuomba katika mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Kesi iliahirishwa hadi Machi 29, mwaka huu na washtakiwa hao walirudishwa rumande hadi tarehe hiyo shauri hilo litakapopelekwa kwa kutajwa kutokana na upelelezi kutokamilika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles