31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

WAONYWA KUZUIA WAGONJWA WA VVU KUTUMIA DAWA

single_pill_arv_treatment_welcomed

Na RAYMOND MINJA -IRINGA

MBUNGE wa Mufindi Kusini, Mendrad Kigola (CCM), amewaomba watumishi wa Mungu wanaowaombea watu wenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), kuacha kuwakataza kutumia dawa za kupunguza makali ya Ukimwi na badala yake wawahimize kutumia dawa hizo.

Akizungumza wakati wa kikao cha Ushauri cha Mkoa wa Iringa (RCC), wakati wa kuchangia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mapambano ya Ukimwi, Kigola alisema wapo baadhi ya wagonjwa wenye maambukizi waliofariki dunia baada ya kuacha kutumia dawa za kufubaza VVU wakitegemea kupona kwa kupitia miujiza ya watumishi wa Mungu.

“Nimeona hili na nimesikia, kuna wahubiri wengi tu siku hizi wanaotangaza kuponya watu Ukimwi, baadhi yao wamewafanya wenye ugonjwa huu kuacha kutumia dawa wakiamini watapona kwa maombi pekee, hii ni hatari sana,” alisema.

Alisema katika taarifa ya ugonjwa huo, takwimu zinaonyesha kuwapo idadi kubwa ya wagonjwa walioacha kutumia dawa hizo kwa imani ya kupona kwa njia ya maombi, lakini wanafariki dunia.

“Nawaomba watumishi wa Mungu, kazi yenu ni kubwa na nzuri, ombeeni watu wapone kwa imani wakati wakiendelea kutumia dawa hizi ili kupunguza madhara ya ugonjwa huo, ni vema maombi yakaendana na dawa,” alisema.

Akiwasilisha taarifa ya hali ya ugonjwa huo mkoani hapa, Dk. Paul Luvanda, alisema bado tatizo ni kubwa linalohitaji jitihada zaidi.

Alisema kwa mujibu wa utafiti wa viashiria vya maambukizi mapya ya VVU na malaria wa mwaka 2011/2012, takwimu zinaonesha kiwango cha maambukizi mapya ni asilimia 9.1, takwimu zinazoufanya mkoa huo uwe wa pili kwa maambukizi kitaifa, baada ya Njombe.

“Kati ya hizo asilimia 10.9 ya maambukizi, ni kwa wanawake wenye umri wa kati ya miaka 15 na 49 wakati asilimia 6.9 ni kwa wanaume wenye umri huo,” alisema.

Alisema takwimu zinaonyesha asilimia saba ya wasichana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 24 wanaishi na maambukizi mapya ya VVU mkoani Iringa, huku asilimia 1.5 ya wavulana wenye umri huo wakiwa na maambukizi pia.

Dk. Luvanda alisema hali ya maambukizi ya VVU kiwilaya inaonesha wilaya ya Mufindi ndiyo inayoongoza mkoani Iringa kwa kuwa na asilimia kubwa ya wananchi wanaoishi na maambukizi hayo.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles