29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, October 21, 2021

WAOMBA NGUVU YA JWTZ KUKOMESHA UVUVI HARAMU

Na SAMWEL MWANGA-BUSEGA


SERIKALI mkoani Simiyu imeomba kuwapo kwa kikundi cha ulinzi cha kijeshi katika Wilaya ya Busega, ili kusaidia mapambano dhidi ya vitendo vya uhalifu ikiwemo uvuvi haramu.

Ombi hilo lilitolewa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, wakati wa hafla ya kumpongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo iliyoandaliwa na familia kijijini kwao  Yitimwila ‘A’  Kata ya Kiloleri wilayani hapa.

Alisema wamekuwa wakipata changamoto nyingi katika Ziwa Victoria ikiwamo vitendo vya uvuvi haramu sambamba na vitendo vya kihalifu, ambapo katika vikao vya mkoa waliona ni vizuri kikawepo kikundi cha kijeshi kwa ajili ya kuimarisha ulinzi katika maeneo hayo.

“Tumepata changamoto nyingi sana kwenye Ziwa Victoria matukio mengi ya kihalifu ikiwemo uvuvi haramu sisi kama mkoa tulikuja na wazo kwamba tungehitaji tupate ‘detouch’ moja eneo la Ziwa ili ukanda huu baada ya kufanya kazi kubwa ya kuchoma makokoro ya wananchi ili tuwapeleke kwenye uvuvi wa kisasa,” alisema.

Alisema pamoja na kufanya ufugaji wa samaki  katika ziwa hilo mkoa huo umefanya makubaliano na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuwawezesha wananchi wa Wilaya ya Busega kufanya kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia maji ya Ziwa Victoria ambayo ni ya uhakika.

“Tumeongea na NSSF kwa ajili ya kuanzisha mradi ambao hautazidi Sh bilioni moja tutaleta mbegu za nyanya na pilipili zinazotakiwa ili wananchi wa Busega wazalishe kwa wingi kwani hatutakuwa tayari kuona wananchi wanalima  nyanya na kuuza ndoo moja Sh 500,”alisema.

Aidha wataalam wa wilaya na mkoa wa kilimo kwa kushirikiana na wataalam wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji na Kituo cha Utafiti wa Kilimo Ukiriguru wanafanya upembuzi yakinifu kuona namna miundombinu ya umwagiliaji itakavyojengwa ili kuwawezesha wananchi wa wilaya hiyo kulima muda wote kupitia kilimo cha umwagiliaji badala ya kutegemea mvua.

Alisema mkoa huo umedhamiria kuhakikisha katika kipindi cha miaka mitatu ijayo hauingizi bidhaa kutoka mikoa mingine na badala yake wananchi wake watazalisha na kutumia bidhaa zao wenyewe.

Hivyo ameomba Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuona namna ya kuweka vituo vya kuuza zana za kilimo katika maeneo ya Kanda ya Ziwa, ili wananchi wapate zana bora za kisasa zitakazowasaidia kulima kisasa.

Kwa upande wake Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi hapa nchini, Jenerali Venance Mabeyo amewataka wananchi wa Busega kubadili mtazamo wao na kutumia maji ya Ziwa Victoria kwa manufaa yao kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili wasikumbwe na tatizo la upungufu wa chakula kunapotokea ukame.

Kuhusu suala la ulinzi katika Ziwa Victoria alisema ombi hilo amelipokea na viongozi watalitafakari kuona namna ya kulishughulikia na kueleza kuwa tayari Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeweka kikundi kidogo cha ulinzi kutoka Jeshi la Wanamaji, lakini kutokana na ukubwa wa ziwa hilo kikundi hicho hakiwezi kuhimili kufanya doria maeneo yote.

Pia Jenerali Mabeyo amewaasa vijana wa wilaya hiyo na mkoa huo kwa ujumla kujiunga katika vikundi ili Serikali iwasaidie kutafuta mitaji ya kujishughulisha na kilimo, uvuvi na ufugaji badala ya kukimbilia JKT.

“Vijana msikimbilie kwenda kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)undeni vikundi vya kuzalisha mali na serikali itawasaidia kutafuta mitaji na mjishughulishe na kilimo, uvuvi na ufugaji na si wengi kukimbilia JKT huko nako kunaweza kuwasaidia kupata stadi mbalimbali za maisha kwa wale ambao watabahatika kuchaguliwa,”alisema.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,682FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles