Na Iman Nathaniel, Mtanzania Digital
Katika kesi inayowakabili wanandoa Bharat Nathwan na Sangita Bharat, upande wa utetezi umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuahairisha kesi kutokana na wakili wao kuwa na udhuru.
Hatua hiyo imekuja kutokana na Wakili wa upande wa utetezi Edward Chuwa kuwa na kesi nyingine Mahakama Kuu ya Tanzania.
Akijibu maombi hayo Hakimu Mkazi Mkuu Aaron Lyamuya amesema kuwa kesi lazima iishe na kwenda mbali zaidi kwa kusema analipwa na mawakili wanalipwa anatakiwa afanye kazi.
Lyamuya aliwataka washtakiwa wamueleze wakili wao kilichoendelea mahakamani na wamwambie aje mahakamani shauri lisikilizwe ili maisha mengine yaendelee.
Hakimu Lyamuya amelipangia shauri hilo tarehe nyingine ya Oktoba 7, 2024 kwa ajili ya kusikilizwa, ambapo shahidi alionywa afike tarehe hiyo bila kukosa.
Hakimu Lyamuya aliwauliza washtakiwa kama wamesikia malalamiko ya wakili wa serikali kuhusu wakili wao Chuwa kutokufika mahakamani ambapo waliiambia mahakama wamesikia.
Akijibu hoja za Wakili wa Serikali, Faraja Ngukah kuwa Sangita hakuwa mgonjwa, lakini Bharat Nathwan ameiambia mahakama kuwa,mkewe ni mgonjwa wala hakuwa anadanganya hivyo bado anaendelea na matibabu.
Licha ya Sangita kuwa mgonjwa bado amekuwa akihudhuria mahakamani bila kukosa hali ilimfanya wakili wa Serikali kusema Sangita sio mgonjwa lakini si kweli kutokana na vielelezo vya kitaalam vya kitabibu vileoneshwa mahakamani hapo.
Awali Wakili Ngukah alidai kuwa katika vikao hivyo vitatu cha Agosti 30, 2024, Septemba 10, 2024 na kikao cha leo cha Septemba 26, 2024 vikao vyote hivyo walipata hudhuru kutoka kwa Wakili Chuwa kuwa na majukumu katika Mahakama Kuu na ugonjwa wa mteja wake Sangita.
Alidai kuwa tarehe 30 , Wakili Chuwa aliomba hudhuru kuwa yuko Mahakama Kuu kwenye usikilizwaji wa shauri na Septemba 10, 2024 Mahakama iliihairisha kesi kutokana sababu Sangita kuwa anaumwa.