26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Wanywaji pombe kali hatarini kupata saratani ya koo

VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAMKOO ndiyo njia pekee ambayo chakula chochote ambacho binadamu hukila, humeza au kinywaji anachokunywa hupita kuelekea tumboni mwake, hewa anayovuta nayo huingia ndani ya mwili kupitia njia hiyo ya koo.

Kiungo hicho nacho huweza kuathiriwa na ugonjwa wa saratani, kimsingi saratani ni jina ambalo limetungwa na wataalamu likiwa na mkusanyiko wa kundi la magonjwa mengi yanayofanana kwenye njia kuu mbili.

Kwanza ni kule kukosekana kwa udhibiti wa uzalianaji wa seli au chembechembe hai za mwili, pili ni kutodhibitiwa kwa zile chembechembe hai zinazozaliana kwa wingi.

Chembechembe hizo huweza kusafiri kutoka sehemu zilipozaliwa kwenda sehemu mbalimbali za mwili, huendelea kuota na kusambaa zaidi katika sehemu zingine za mwili, hukosa udhibiti.

Mabingwa wa magonjwa ya saratani wanaeleza saratani hupewa majina kulingana na mahala ambapo imetokea katika mwili wa binadamu na kwamba kuna zaidi ya aina 200 za saratani.

Aina hizo hutokana na majina ambayo hupewa kulingana na mahala (sehemu ya mwilini) ambapo saratani imejitokeza, hivyo ikijitokeza kooni huitwa saratani ya koo.

Takwimu za ORCI

Takwimu za Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), zinaonesha kuna ongezeko la wagonjwa wa saratani ya koo 511 ndani ya kipindi cha miaka 12, kuanzia 2005 hadi 2016.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani wa ORCI, Jerry Ndumbalo anasema dalili kuu ya kwanza ambayo mtu mwenye saratani ya koo huanza kupata ni kushindwa kumeza vema hasa anapokuwa akila chakula.

Anasema takwimu zinaonesha saratani ya koo inashika namba nne kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa ikitanguliwa na saratani ya shingo ya kizazi, matiti na ngozi (kaposisis sarcoma) ambayo huwapata zaidi watu wenye ulemavu wa ngozi.

“Inasumbua watu wengi, bahati mbaya wagonjwa tunaowapokea huja wakati ugonjwa ukiwa umefika hatua za juu (tatu au nne) ambazo kwa kawaida huwa ni vigumu kupona,” anasema.

Anasema takwimu zinaonesha idadi ya watu wanaopokewa wakikabiliwa na saratani hiyo inaonekana kuongezeka mwaka hadi mwaka.

“Katika kipindi cha mwaka 2005 hadi 2016 tumehudumia jumla ya wagonjwa 5,262 sawa na asilimia 10, idadi inaonekana kuongezeka kwa mfano katika mwaka 2005 tuliona wagonjwa 196 kufikia 2016 tumeona wagonjwa 707,”anasema.

 

Visababishi

Dk. Ndumbalo anasema vipo visababishi mbalimbali ambavyo huchangia mtu kuishia kupata saratani hiyo ikiwamo unywaji wa pombe kali, uvutaji sigara na ulaji usiofaa hasa kutokula mbogamboga na matunda.

“Unywaji pombe kali humuweka mtu kwenye hatari ya kupata saratani ya koo siku zijazo maisha mwake, kwa mfano gongo utaona mtu akinywa anakuwa hadi anakunja sura kutokana na ule ukali.

“Kimsingi, pombe kali inapopita kooni huwa kuna uwezekano mkubwa wa kukwanguka kwa sehemu hiyo, hali hiyo inaweza kusababisha saratani ya koo hapo baadaye katika maisha ya mhusika,”anabainisha.

 

Mbogamboga/matunda

Dk. Ndumbalo anasema ulaji wa matunda na mbogamboga ni kinga madhubuti dhidi ya saratani hiyo.

“Kimsingi, ulaji wa mbogamboga na matunda ni muhimu kwani vyakula hivyo vina nyuzi nyuzi ambazo husaidia kulinda koo lisichubuke.

“Mtu anapokula chakula kigumu peke yake (kisicho na nyuzi nyuzi), koo lake huchubuka, kule kuchubuka mara kwa mara kwa koo baadaye huweza kusababisha kupata saratani ya koo,”anasema.

 

Kinachotokea

Anasema saratani inapoota katika eneo hilo hukua na kufanya njia ile kuwa ndogo na hatimaye kuziba kabisa ikiwa mtu hatapatiwa matibabu sahihi kwa haraka dhidi ya ugonjwa huo.

“Kutokana na kuanza kupungua kwa njia hiyo, mtu huanza kupata tabu wakati wa kumeza chakula na kwa sababu anakuwa hali vizuri anaanza kupungua uzito, pakiziba kabisa hushindwa kula kitu chochote,”anasema Dk. Ndumbalo.

 

Matibabu

Dk. Ndumbalo anasema tangu Oktoba 30, mwaka huu Ocean Road imeanza kuwatibu wagonjwa wa saratani ya koo kwa njia ya kisasa zaidi.

Anasema wanawapatia matibabu wagonjwa hao kwa kutumia mionzi ya ndani, ambapo kitaalamu huduma hiyo inaitwa Oesophageal Brachyltherapy.

“Aina hii ya tiba awali hapa ORCI tulikuwa tunaitoa kwa wagonjwa wa saratani ya kizazi pekee, lakini kuanzia Oktoba 30, mwaka huu tumeanza rasmi kutoa tiba hii pia kwa wagonjwa wa saratani ya koo,”anasema.

Dk. Ndumbalo anasema tiba hiyo ya mionzi ya ndani ni nzuri zaidi kuliko ile ya nje pekee ambayo wamekuwa wakiitoa kwa wagonjwa wa saratani ya koo.

Anasema kwa kutumia tiba ya mionzi ya ndani kwa kutumia kifaa maalumu cha Oesophageal Applicators inawawezesha wataalamu kutibu ugonjwa moja kwa moja katika eneo lililoathiriwa na ugonjwa.

Mtaalamu

Mtaalamu Mbobezi wa Fizikia Tiba wa Taasisi ya Eckert & Ziegler ya nchini Ujerumani, Antonius Spiller anasema aina hiyo ya tiba imekuwa ikitolewa nchini humo kwa miaka mingi sasa.

“Ingawa tunayo kule Ujerumani, sisi hatuna idadi kubwa ya wagonjwa wanaohitaji kama ilivyo kwa Tanzania,”anasema.

Anasema ndiyo maana ORCI walipoamua kuanzisha huduma hii niliona vema kuja kushirikiana nao kuwaelekeza madaktari jinsi ya kuitumia katika kutibu wagonjwa.

“Mionzi ya ndani ni tiba nzuri zaidi kuliko ile ya nje, kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki hakuna taasisi inayotoa matibabu ya aina hii.

“Hivyo, kwa hatua hii maana yake Tanzania inakuwa nchi pekee ukanda wa Afrika Mashariki kuanzisha tiba ya aina hii, ni wazi wananchi wengi zaidi watanufaika,”anasema.

Inavyotolewa

Mfizikia Tiba wa Idara ya Tiba ya Mionzi ORCI, Shaid Yusuph anasema kwa kawaida ili mgonjwa apatiwe tiba ya mionzi ni lazima alazwe kwanza katika kitanda.

“Akishalazwa, sisi tunachofanya ni kuchukua ‘image’ yake hapo daktari anakuwa ameshatupatia kiwango cha tiba anachopaswa mgonjwa kupatiwa, tukiwa tumeingiza kifaa hiki kupitia kinywa chake, tunampatia tiba kulingana na maelekezo ya daktari,”anabainisha.

Dk. Ndumbalo anasema “Kifaa hicho kinaelekea moja kwa moja kwenye sehemu yenye ugonjwa na wanaweza kupima kuangalia kimefika eneo husika ama la!

“Kwa hiyo, sasa tuna uwezo wa kutibu ugonjwa kwa haraka zaidi na majibu huwa ya haraka zaidi.

“Tunamshukuru Spiller kwa kuja nchini kutusaidia ujuzi zaidi, awali tulijifunza utaalamu huu vyuoni lakini changamoto ilikuwa kwamba vifaa hivi hapa hospitalini havikuwepo, lakini sasa uongozi wa hospitali umevinunua,”anasema.

Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk. Julius Mwaiselage anasema vifaa hivyo vimenunuliwa moja kwa moja kutoka nchini Ujerumani kupitia mapato yake ya ndani ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kuimarisha huduma za afya nchini.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,277FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles